Rais Samia: Mauzo ya Nje ya bidhaa yameongezeka kwa Trilioni 5

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa mauzo ya nje ya bidhaa za Tanzania yalipanda kutoka shilingi trilioni 12.3 mwaka 2019 hadi kufikia shilingi trilioni 17.3, sawa na dola za Marekani bilioni 6.56, mwaka jana.

Rais Samia alitoa taarifa hiyo, Julai 3, 2024, jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (DITF), maarufu kama Sabasaba, yaliyofunguliwa rasmi na Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi.

“Tutakamilisha miradi ya miundombinu ili bidhaa zinazozalishwa ziweze kufika kwa urahisi kwenye masoko yaliyokusudiwa,” alisema Rais Samia.

Amesema serikali itaendelea kujenga, kuboresha na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya miundombinu ili kuhakikisha uzalishaji wa bidhaa bora na nyingi unaongezeka.

Aidha, Rais Samia amesema maonesho ya Sabasaba kwa mwaka huu yamezikutanisha zaidi ya kampuni 3,486 za ndani na nje ya nchi, jambo linaloashiria ukuaji na mvuto wa tukio hilo.

“Mvuto huu umechangiwa na juhudi za serikali katika kusimamia misingi imara ya kujenga uchumi jumuishi na shindani katika nyanja mbalimbali ikiwemo biashara, viwanda, na uwekezaji,” alisema.

Rais Samia pia alihimiza wafanyabiashara kutumia maonesho hayo kukuza biashara zao na kutumia taasisi za serikali kufanikisha azma hiyo ya kufanya biashara katika nchi za nje, hasa kupitia eneo huru la biashara Afrika (AfCFTA).

“Wafanyabiashara wa Tanzania, kupitia maonesho haya, jifunzeni kutoka kwa wafanyabiashara kutoka nje ili muweze kukuza biashara zenu. Itumieni Tantrade kufanikisha biashara zenu kwa kutazama fursa zilizopo kwenye masoko ya kimataifa,” alisema.

Rais Samia alibainisha kuwa mwaka 2023, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilisajili miradi 504 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 5.68, kutokana na kuvutiwa na maonesho hayo na kuwekeza nchini.

Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi, akifungua maonesho hayo, aliishukuru serikali ya Tanzania kwa msaada wake katika kupambana na ugaidi, ambao ulikuwa unazorotesha uchumi wa nchi hiyo. Alisema Tanzania imekuwa bega kwa bega na watu wa Msumbiji katika kipindi hicho cha changamoto mpaka sasa ambapo hali imetulia.

Nyusi alisema utulivu na amani ni muhimu kwa matumizi ya fursa za nishati kati ya nchi hizo mbili zenye akiba kubwa ya gesi asilia katika mkoa wa Mtwara na jimbo la Delgabo, Msumbiji. Alibainisha kuwa biashara za nje kati ya nchi hizo mbili katika kipindi cha miaka 10 iliyopita zimefikia dola za Marekani milioni 250 tu.

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omary Saidi Shabani, alisema maonesho hayo yamebahatika kuwa na marais wawili, huku yakijumuisha washiriki 3,846, wa ndani wakiwa 3,433, kutoka nchi 26, ikilinganishwa na nchi 19 mwaka jana.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, alishukuru Rais Samia kwa kumkaribisha Rais Nyusi kuwa mgeni rasmi wa maonesho hayo. Alisema maonesho hayo yamekuwa yakikua kila mwaka na mwaka huu wamefikia washiriki 3,846.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Deudatus Mnyika, alisema maonesho hayo ni kipimo cha maboresho makubwa ya sekta ya viwanda na biashara ambapo makampuni 3,280 yameshiriki, yakiwemo ya ndani na nje ya nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisifu viongozi kwa kuonyesha uimara wao katika maonesho hayo na aliahidi kuendelea kuboresha na kuhamasisha ushiriki wa wananchi wengi zaidi.

Maonesho hayo yanaendelea kuvutia washiriki wengi kutoka nchi mbalimbali, na yamekuwa chachu ya maendeleo ya biashara na uwekezaji nchini Tanzania.

Related Posts