Hali imeanza kurejea ya kawaida katika jiji kuu la Nairobi kufuatia siku kadhaa za purukushani na maandamano yaliyowaua zaidi ya 40. Tofauti na ilivyokuwa Jumanne wiki hii pale polisi walipovurugana na waandamanaji, eneo la katikati ya jiji lilikuwa tulivu huku maafisa wa usalama wakipiga doria.
Waandamanaji 187 waliokamatwa wakati wa purukushaniwameachiliwa kwa dhamana. Kwa mujibu wa chama cha mawakili nchini, LSK, waliokuwa na umri wa chini ya miaka 18 waliachiliwa kwa dhamana na shilingi alfu kumi za Kenya na watu wazima walilipishwa kiwango kilicho mara ya tano ya hicho. Kwa upande wake, viongozi wa dini ya kiislamu wanairai serikali kuwaachilia wanaozuiliwa na pia kuzisaidia familia za waliofiliwa.
Hayo yamejiri baada ya kikao na waandishi wa habari. Familia ya Wilson Sitati, aliyekuwa mwanafunzi wa chuo cha ufundi cha Olimpik mtaani Kibera ilifika kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha City ili kuchukua mwili wa mpendwa wao aliyeuawa wakati wa maandamano akielekea kwenye shughuli zake mjini.
Yote hayo yakiendelea, Rais William Ruto ameusisitizia umuhimu wa taifa kuchukua mkondo mpya kufuatia maandamano hayo ya vurugu. Kwenye kikao cha kwanza tangu purukushani kuanza na baraza lake la mawaziri, Ruto alielezea kuwa sharti yawepo mabadiliko ila hakufafanua. Baraza lilifahamishwa kuhusu hali halisi ya usalama nchini na kwamba idara za usalama zilipongezwa kwa mienendo yao katika mazingira magumu. Hata hivyo wahalifu watachukuliwa hatua kali lilisiistiza baraza la mawaziri la Kenya.
Kwengineko, mjini Kisii biashara nyingi zilifungwa kwa kuhofia ghasia nao polisi waliendelea kudhibiti usalama. Mjini Emali, hali ilichafuka kwa muda na usafiri kutatizika kwenye barabara kuu ya kutokea Nairobi kuelekea Mombasa.
Soma pia:Blinken akaribisha hatua za rais wa Kenya kutuliza mvutano
Katika hali ambayo haikutarajiwa, wandani wa Rais William Ruto katika baraza la Senati wameziongezea nguvu shinikizo za kutaka mabadiliko uongozi na kulikosoa hadharani baraza la mawaziri. Kiongozi wa chama tawala kwenye Senate Aron Cheruiyot na wenzake wanamtaka Ruto kulivunjilia mbali baraza hilo, kumtimua Inspekta mkuu wa polisi Japheth Koome na kufanya mabadiliko serikalini.Kauli hizo zinaungwa mkono na mbunge wa Nyaribari Masaba Daniel Ogwoka Manduku anayebainisha wako tayari kushirikiana kwa manufaa ya wakenya.
Ifahamike kuwa Rais William Ruto aliahidi kukutana na vijana walioshinikiza maandamano kwenye jukwaa la mtandao kabla ya wiki hii kufikia kikomo.