SUMAJKT yaajiri vijana 16,000 kwenye ulinzi

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Zaidi ya vijana 16,000 wamepata ajira ya ulinzi katika Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) na kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza Julai 3,2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, amesema fursa hiyo ya ajira imewawezesha vijana hao kujikimu kimaisha na kutunza familia zao.

“Tunaanzisha kampuni ili kufanya biashara na kutoa huduma kwa nchi yetu, kampuni yetu ya ulinzi ni miongoni mwa kampuni bora Tanzania, tunatoa huduma sehemu mbalimbali na tunaendelea kupata wateja wengi, kwahiyo tumechangia kupunguza ukosefu wa ajira hasa kwa vijana.

Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, akiangalia bidhaa mbalimbali katika banda la jeshi hilo kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba).

“Tunayo pia kampuni ya usafi, Watanzania wanahitaji majiji yao yawe safi, tumewaajiri vijana wa Kitanzania kuhakikisha mazingira yanakuwa safi,” amesema Meja Jenerali Mabele ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa SUMAJKT.

Amesema biashara zinazofanywa kupitia shirika hilo zinachangia ukuaji wa uchumi nchini kama ambavyo wameshiriki kutoa gawio Serikalini hivi karibuni.

“Sisi ni wachangiaji wazuri katika mfuko mkuu wa Serikali na tunalipa kodi, katika kila vifaa vinavyotengeenzwa na kuuzwa tunalipa kodi. Tunachoangalia ni fursa, tumeona kuna fursa kubwa kwenye biashara ya bima, ni eneo ambalo litatoa fursa ya biashara na huduma kwa Watanzania,” amesema.

Amesema wanatumia maonesho hayo kuonesha bidhaa zenye ubora na bei rafiki kama vile samani na kuwashauri wadau mbalimbali kupita katika banda la Jeshi la Kujenga Taifa kupata bidhaa zenye ubora.

Amesema pia wamekuwa wakishiriki katika maonesho yanayofanyika nchi mbalimbali hatua iliyowawezesha kupata wateja wengi zaidi kutokana na bidhaa wanazozalisha.

Mkuu huyo wa JKT ameipongeza Serikali kwa kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini hatua iliyowavutia watu wengi kuja nchini kuwekeza.

Naye Mkuu wa Utawala wa JKT, Brigedia Jenerali, Hassan Mabena, amesema vijana wa kujitolea na wale wa mujibu wa sheria licha ya kufundishwa masomo ya ukakamavu na uzalendo pia wamekuwa wakifundishwa uzalishaji mali na baada ya kumaliza mkataba wao wa mafunzo wanatumia ujuzi walioupata kujitegemea.

“Vijana wamefundishwa kuanzisha bidhaa mbalimbali kuanzia bidhaa ndogondogo hadi kubwa, kupitia vikosi vyetu wameweza kutumia maeneo hayo kama shamba darasa ili kuwapatia ujuzi. Kuna kampuni ya kutengeneza bidhaa za ngozi, tuna kiwanda cha samani, nguo…tunawafundisha kwa nadharia na vitendo,” amesema Brigedia Jenerali Mabena.

Related Posts