Taifa Stars yapewa DR Congo kufuzu Afcon 2025

Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, imepangwa Kundi H na DR Congo, Ethiopia na Guinea katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ‘Afcon’ 2025 ambazo zitafanyika Morocco.

Mchujo wa kuwania kufuzu michuano hiyo ulianzia hatua ya awali Machi 21 hadi 26 mwaka huu na sasa inakwenda hatua ya makundi yaliyopangwa leo Alhamisi huko Afrika Kusini.

Hatua hiyo ya makundi kuwania kufuzu Afcon 2025 zitaanza kuchezwa Septemba mwaka huu. Jumla ya timu 24 zitafuzu kucheza fainali hizo ambapo bingwa mtetezi ni Ivory Coast.

Tanzania ambayo ilikuwa katika chungu cha tatu kati ya vinne vilivyotengwa kulingana na viwango vya ubora wa soka, ilikuwa timu ya pili kupangwa katika Kundi H baada ya Ethiopia huku ikifuata Guinea kisha DR Congo.

Katika kundi hilo, DR Congo ndio timu inayoshika nafasi ya juu zaidi katika viwango vya soka vya FIFA vilivyotolewa Juni, mwaka huu ikiwa nafasi ya 61, Guinea ipo nafasi ya 77, Tanzania (114) huku Ethiopia ikishika nafasi ya 143.

Tanzania na DR Congo kupangwa kundi moja inatukumbusha ilivyokuwa katika mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2022 ambapo timu hizo zilikuwa Kundi J. Ugenini Tanzania ilipata sare ya 1-1, nyumbani ikafungwa 3-0.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana katika Kundi F la Afcon 2023 na matokeo kuwa 0-0.

Ikumbukwe kwamba vinara wawili katika kila kundi watajikatia tiketi ya kushiriki fainali hizo za 35 zitakazofanyika kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026 nchini Morocco.

Kundi A: Gambia, Comoros, Madagascar, Tunisia

Kundi B: Lesotho, Afrika ya Kati, Gabon, Morocco

Kundi C: Botswana, Mauritania, Cape Verde, Misri

Kundi D: Rwanda, Libya, Benin, Nigeria

Kundi E: Liberia, Togo, Guinea ya Ikweta, Algeria

Kundi F: Niger, Sudan, Angola, Ghana

Kundi G: Chad, Sierra Leone, Zambia, Ivory Coast

Kundi H: Ethiopia, Tanzania, Guinea, DR Congo

Kundi I: Eswatini, Guinea Bissau, Msumbiji, Mali

Kundi J: Zimbabwe, Kenya, Namibia, Cameroon

Kundi K: Sudan Kusini, Congo Brazzaville, Uganda, Afrika Kusini

Kundi L: Burundi, Malawi, Burkina Faso, Senegal

Related Posts