TANZANIA, QATAR KUSHIRIKIANA SEKTA YA UTALII

Na Happiness Shayo- Dar es Salaam

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nchi ya Qatar ziko mbioni kusaini Hati ya Makubaliano (Memorandum of Understanding-MOU) kushirikiana katika nyanja mbalimbali za Sekta ya Maliasili na Utalii.

Hayo yamebainika leo Julai 4,2024 wakati wa kikao kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb) na Balozi wa Qatar nchini Tanzania, Mhe. Fahad Rashid Al Marekhi kilichofanyika Makao Makuu ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) jijini Dar es Salaam ambapo wamekubaliana kukamilisha Hati hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kairuki amesema kuwa kupitia mkataba huo Tanzania na Qatar zitafaidika na hivyo kutoa wito kwa nchi zote mbili kutumia fursa hiyo katika kuimarisha utalii.

“Tunaamini tutapata fursa ya kuonesha vivutio vyetu vya utalii wakati wa hafla mbalimbali zilitakazofanyika nchini Qatar ikizingatiwa kwamba Qatar ni mojawapo ya soko la kimkakati la utalii kwa Tanzania lakini pia kwa kuzingatia uhusiano, umbali kati ya nchi zetu mbili, tofauti za kiutamaduni na mengi tunayofanana” Mhe. Kairuki amesisitiza.

Ametaja maeneo mengine ambayo nchi hizo mbili zitanufaika ni uhusiano kati ya Bodi yetu ya Utalii Tanzania na Qatar Tourism, kuuunganisha wadau wa utalii kama vile Wakala wa Biashara za Utalii wa Tanzania na Qatar, vyama vya wasafiri, vyama vya hoteli n.k.

Aidha, Mhe. Kairuki ametumia fursa hiyo kuomba ushirikiano kati ya Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) na vyuo vya elimu vya nchini Qatar katika kutoa mafunzo mbalimbali na kubadilishana uzoefu.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki amekubaliana na wazo la kuanzishwa kwa wiki ya Qatar na Tanzania katika kukuza utalii na utamaduni katika pande zote za nchi hizo mbili.

Pia, Waziri Kairuki ameomba ushirikiano katika kutangaza utalii kupitia vyombo vya habari na mashirika ya ndege ikiwemo Aljazeera na Qatar Airways.

Amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Qatar kuwekeza katika huduma ya malazi kwa kujenga hoteli kwenye baadhi ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji ndani ya hifadhi yaliyo chini ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) pamoja na maeneo mengine nje ya ardhi inayomilikiwa na Serikali.

Kwa upande wake na Balozi wa Qatar nchini Tanzania, Mhe. Fahad Rashid Al Marekhi amesema atahakikisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Qatar unaendelezwa.

“Tunashirikiana na Tanzania na nitahakikisha tunakamilisha na kusaini mikataba yote ya makubaliano kwa faida ya nchi zetu ” Mhe. Marekhi amesema.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bw. Ephraim B. Mafuru, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Mhe. Abdalah A. Kilima na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Related Posts