Ingawa mambo mengi yatategemea duru ya pili ya uchaguzi wa siku ya Jumapili, tayari inaonekana wazi kuwa jukumu la Macron kama kinara wa ushirikiano wa Ulaya utapungua kwa kiasi kikubwa.
Matukio mawili yanayoweza kujitokeza; serikali inayoongozwa na Marine Le Pen, kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha National Rally, RN, au bunge ambalo hakuna chama cha kisiasa chenye viti vya kutosha kupata wingi wa jumla, lingewasilisha changamoto ambazo hazijawahi kushuhudiwa ndani ya Umoja wa Ulaya. Hata ikiwa bunge halitopata wingi wa kura kwa ujumla, na kusababisha muungano mbaya au vyama vinavyoshirikiana moja kwa moja, vitamkosesha Macron serikali inayojizatiti kwa sera zake.
Kwa vyovyote vile, swali kubwa litakuwa kuhusu baadhi ya mipango ya Macron yenye ujasiri zaidi, kuanzia ukopaji wa pamoja wa Umoja wa Ulaya ili kufadhili matumizi ya ulinzi kwa kuongeza mara mbili bajeti ya umoja huo, hadi kupeleka wanajeshi wa Ufaransa nchini Ukraine kutoa mafunzo kwa vikosi vya Kiev.
Wakati Ufaransa na Ujerumani kijadi zinatumia msingi unaouendesha Umoja wa Ulaya wenye nchi wanachama 27, umoja huo unaweza kukabiliwa na mkwamo wa kisiasa kwani viongozi wake wawili muhimu zaidi wanaounga mkono umoja huo watakuwa nyuma.
Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz ameona chama chake kikishindwa katika uchaguzi wa Bunge la Ulaya mwezi uliopita, anapambana kuiunganisha serikali yake ya mseto, na anatazamiwa kupata upinzani mkali kutoka kwa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia katika uchaguzi ujao wa majimbo.
Macron amedhoofika nyumbani
Elizabeth Kuiper, mkurugenzi msaidizi katika Kituo cha Sera cha Ulaya, anasema Macron amedhoofika sana nyumbani, jambo ambalo litakuwa na madhara kwa nafasi yake katika Umoja wa Ulaya na kwa uhusiano kati ya Ufaransa na Ujerumani.
Wakati vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia barani Ulaya bado viko mbali na lengo lao la kuudhibiti Umoja wa Ulaya na kurejesha mamlaka katika ngazi ya kitaifa, wana ujasiri na uhakika wa siasa wanazozifanya. Wamepata mafanikio katika uchaguzi wa Bunge la Ulaya, ambapo chama cha Waziri Mkuu wa Italia Georgia Meloni kilipata ushindi mkubwa.
Serikali mpya ya Uholanzi yenye ushiriki wa siasa kali za mrengo wa kulia imeingia madarakani. Waziri Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban amechukua nafasi ya urais wa zamu wa Umoja wa Ulaya na kutangaza kuundwa kwa “muungano wa kizalendo” wa Ulaya mpya. Kuiper anasema Ufaransa na Ujerumani dhaifu pamoja na Italia na Hungary zenye nguvu ni wazi zitaunda mustakabali wa Umoja wa Ulaya.
Maafisa wa Ufaransa wamesema Macron amewaambia wenzake wa Umoja wa Ulaya kwamba Ufaransa itaendelea kuwa na jukumu kubwa ndani ya umoja huo. Mmoja wa maafisa hao amesema Ufaransa itabakia kuwa Ufaransa yenye uzito wake. Lakini sera na matamshi ya chama cha RN yanaonyesha kuwa migongano kati ya Macron na Umoja wa Ulaya haitoweza kuepukika.
Harakati za kumteua kamishna wa Ulaya
Le Pen amesema serikali itakayoongozwa na RN itamteua kamishna ajae wa Ufaransa kwa ajili ya Ulaya, nafasi muhimu ndani ya Umoja wa Ulaya. Lakini kijadi hilo hufanywa na rais, na Macron tayari ameashiria kuwa anataka kumbakiza Thierry Breton.
RN pia inataka Ufaransa kupata punguzo kutoka kwenye bajeti ya Umoja wa Ulaya, jambo ambalo umoja huo hauwezakani kutoa. Na wakati sera za kiuchumi za RN zikibadilika mara kwa mara katika wiki za hivi karibuni, zinaweza kukiuka sheria za kifedha za Umoja wa Ulaya.
Karel Lannoo, mtendaji mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Sera ya Ulaya, anasema mipango ya kukuza ushindani wa kiuchumi wa Ulaya kama vile umoja wa masoko ya mitaji ya Umoja wa Ulaya pia itakuwa hatarini. Lannoo anasema tatizo la Umoja wa Ulaya ni kwamba ikiwa hakuna nchi wanachama wanaoiunga mkono kwa nguvu, basi ni ngumu sana kusonga mbele.
(Reuters)