Utekaji wazidi kuibua mjadala, Jaji Warioba, Chadema watia mguu

Dar es Salaam. Sakata la matukio ya utekaji na au utowekaji wa wananchi katika mazingira ya kutatanisha, limeendelea kuibua mijadala baada ya Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba kusema matukio kama hayo miaka ya nyuma hayakuwapo.

Mbali na Jaji Warioba, Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha),  limemshauri Rais Samia Suluhu Hassan kuwachukulia hatua Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camilius Wambura.

Bavicha limemtaka Rais ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu kujitokeza hadharani kutoa kauli nzito kwa vyombo vya ulinzi, ili kukomesha vitendo hivyo  vinavyoibua hofu kwa wananchi.

Jaji Warioba na Bavicha kupitia kwa Mwenyekiti wake, John Pambalu wamezungumzia matukio hayo leo Alhamisi, Julai 4, 2024 katika maeneo na nyakati tofauti jijini Dar es Salaam.

Wawili hao wanaungana na wadau wengine ambao Juni 2, 2024 walizungumza na Mwananchi wakiinyooshea kidole Serikali, kwa kushindwa kukomesha vitendo hivyo, huku wengine wakidai  vyombo vyake kuhusika navyo.

Hofu ya wananchi inaibuka katika kipindi ambacho kumekuwa na mfululizo wa matukio ya kutoweka kwa watu kutokana na kutekwa.

Edgar Mwakabela maarufu Sativa ni kielelezo cha matukio hayo, alitoweka Juni 23 jijini Dar es Salaam na Juni 27, mwaka huu akapatikana katika Hifadhi ya Katavi akiwa amejeruhiwa kwa risasi.

Kwa mujibu wa maelezo yake, alidai kutekwa na watu wasiojulikana ambao walimlaza katika karakana ya Polisi Oysterbay kisha wakampeleka Arusha na baadaye Katavi alikotupwa porini.

Tukio la Sativa limefuatana na la Kombo Mbwana, mwanachama wa Chadema, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga aliyetoweka Juni 29 mwaka huu na hadi sasa hajaonekana.

Kombo alitoweka baada ya kufuatwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake na kumchukua kwa nguvu kwa mujibu wa mkewe, Mariam Rajab.

Hiyo ni mifano ya karibunikati ya kadhaa ya watu waliotekwa, wengine wakipatikana hai, wengine hadi sasa haijulikani walipo na wengine miili yao kupatikana baadaye.

Vilio vya watu kutoweka, kwa siku za karibuni vilisikika mfululizo wakati wa ziara za aliyekuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda katika mikoa Simiyu, Singida, Mwanza, Mara, Mbeya, Rukwa na Kigoma, mapema mwaka huu.

Alichokisema Jaji Warioba

Jaji Warioba, ambaye alikuwa Mjumbe wa Tume ya Haki Jinai, leo Alhamisi amegusia matukio hayo wakati akizindua kitabu cha ripoti ya hali ya mwenendo wa vyombo vya habari kwa mwaka 2022/23, kilichoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Amejenga hoja hiyo, wakati akizungumzia uwepo wa uoga  katika vyombo vya habari, wananchi na viongozi, hadi kushindwa kuzisaidia taasisi za haki jinai.

“Tuna matatizo ya watu kutekwa na watu ambao wanaoitwa hawajulikani. Ni jamii hii, lakini kuna watu hawajulikani. Huko nyuma kulikuwa na wakati mtu akiingia katika kijiji chochote kulikuwa na utaratibu wa kumfahamu.”

 “Kulikuwa na utaratibu wa kufahamiana ili likitokea jambo tunasema inawekezana ni fulani, siku hizi huipati kwa sababu watu wana uoga,” amesema.

Amesema Rais Samia alimpomteua kuwa katika Tume ya Haki Jinai, alichukua muda kusoma ripoti za masuala ya jinai na kubaini sababu zinazofanya baadhi ya taasisi za haki jinai zisifanye kazi, kwa kuwa hazina ushirikiano na wananchi.

“Wananchi hawana ushirikiano na taasisi hizi kwa sababu ya uoga, mfano vyombo vya haki jinai vinatafuta habari na mwananchi anazo na anaogopa kuwapa, anasema akiwaambia atapata madhara,” amesema.

Bavicha wataka hatua zaidi

Wakati Jaji Warioba akisema hayo, Pambalu yeye alikuwa makao makuu ya Chadema, Kinondoni jijini Dar es Salaam akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali, likiwemo hilo la utekaji.

Katika mkutano huo, Pambalu alikuwa akifanya rejea ya magazeti ya Mwananchi ya Julai 2 na 3, 2024 yaliyoangazia matukio mbalimbali ya watu kutekwa na kauli ya Waziri Masauni aliyeitoa jana Jumatano, Julai 3, 2024.

Amesema amesoma makala moja ya Luqman Maloto anazungumzia  kuwa Tanzania yageuka pepo ya watekaji,  na kueleza hiyo ndio lugha moja wanayoweza kuisema kwa sasa.

Pambalu amesema taratibu nchi yetu inarejea tena kwa kasi katika kuwa pepo ya utekaji,  kwani ni hivi karibuni kumetokea matukio makubwa mawili.

Amesema wameona hatua ya Rais Samia kumchangia Sativa Sh35 milioni,  lakini wakaonesha kutoridhishwa na uamuzi huo wakisema angetoa kauli mara moja kama Rais ambaye pia  ni Amiri Jeshi Mkuu.

Pia amesema alitegemea Rais atoe kauli ya kukemea mambo hayo ikibidi awachukulie hatua wasaidizi wake.

“Rais hakuona kama sio muhimu sana kukomesha matendo ya utekaji kwani tukio la kutekwa Sativa ilitoa wajibu wa aina mbili mbili, mmoja ulikuwa ni wajibu wa kiutu na wajibu mwingine ulikuwa wa kimamlaka,” amesema.

Pambalu ametanabahisha  kukithiri kwa matendo hayo  katika Taifa huku Rais akiendelea kukaa kimya, akidai kuwa  yanaweka wazi udhaifu wa Serikali  kushindwa kulinda raia  ambao aliapa kuwalinda kama wajibu wake namba moja.

“Tulitegemea Rais azungumze, tulitegemea Rais akemee utekaji, lakini Rais yuko kimya, tulitegemea Rais awawajibishe wasaidizi wake, amwajibishe IGP, amwajibishe Waziri wa Mambo ya Ndani, amwajibishe Mkuu wa kituo  pale Oysterbay,” amesema Pambalu.

Kuhusu kauli ya Waziri Masauni, Pambalu amesema baraza hilo limekaa likatafakari na kufanya uchambuzi na kubaini ina udhaifu hususan alipoeleza ni matukio ya kawaida.

“Mnategemea Waziri mwenye dhamana atoe kauli, hata watekaji wakiisikiliza wadhani ya kwamba huku tunakokwenda hatutakuwa salama, Waziri anawaambia mbona jambo la kawaida,” amesema Pambalu.

Jana Jumatano, Masauni akiwa kwenye shughuli ya uzinduzi wa kitabu cha Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir Ally kinachoitwa ‘Mmomonyoko wa maadili nani alaumiwe? Waziri huyo alitumia jukwaa hilo kuzungumzia matukio hayo ya utekaji.

Waziri Masauni alikiri uwepo wa matukio hayo akisema katika kipindi cha miezi sita kuanzia Januari hadi Juni 2024 yameripotiwa matukio nane ya utekaji yakiwemo la Sativa, Kombo na mengine yaliyotokea maeneo mbaimbali.

Amesema katika matukio hayo wapo watuhumiwa waliokamatwa, kufikishwa mahakamani na mengine uchunguzi unaendelea.

“Uhalifu huu unahusishwa na wanasiasa na Serikali na kuna gazeti moja la Mwananchi limeandika suala hili pia kuna maswali  mengi ya nani mtekaji,  nihakikishe tu Tanzania iko salama,” amesema.

Waziri huyo amebainisha jukumu la Serikali ni kuhakikisha usalama wa wananchi wake na amewatoa hofu wananchi kwamba hali  hapa nchini iko salama.

Jumanne ya  Julai 2, 2024, Dk Anna Henga, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), alihoji  kwa nini Serikali inaonekana kushindwa kuwajua watekaji wakati ina nguvu na uwezo wa kufanya hivyo.

“Hata kama aliyetekwa hana simu janja, lakini Serikali ina mifumo yake ya kuangalia hali ya usalama hadi ngazi ya chini, hasa vijijini, tena katika mtaa akiingia mtu au mgeni anajulikana,” amesema.

Kwa mkono mrefu ilionao Serikali, Dk Henga amesema ni rahisi kufuatilia mwenendo wa usalama na kuwajua na  kuwamata wanaohusika na vitendo hivyo.

“Nadhani haijashindikana kuwakamata kwa haraka wanaodaiwa kuhusika na vitendo hivi. Kinachotakiwa ni Serikali kuweka kipaumbele zaidi, kwamba mtu anapopotea kuwepo na uharaka wa kumtafuta ili aliyetekwa asipate madhara ya kujeruhiwa,” amesema Dk Henga.

Related Posts