Mwanza. Takwimu zinaonyesha sekta ya bima Kanda ya Ziwa imechangia Sh47 bilioni pekee kwenye Pato la Taifa, sawa na asilimia 0.084. Ukosefu wa elimu, ugumu wa maisha, na mwamko mdogo wa jamii umetajwa kama sababu za mchango mdogo wa sekta hii katika pato hilo.
Akizungumza na Mwananchi, Meneja wa Mamlaka ya Bima (Tira) Kanda ya Ziwa, Richard Toyota amesema kuwa licha ya kanda hiyo kuwa na idadi kubwa ya watu zaidi ya milioni 16, ni asilimia tano tu ya wakazi wake, sawa na watu 800,000, wamejiunga na huduma za bima.
Toyota amebainisha kuwa sababu nyingine inayochangia idadi ndogo ya wananchi wanaotumia huduma za bima ni idadi ndogo ya watumishi wa Tira, jambo linalopunguza ufanisi katika utoaji wa elimu ya bima hasa vijijini ambako inahitajika zaidi.
“Sekta ya bima inachangia kama asilimia 2 tu kwenye pato la taifa, sisi Kanda ya Ziwa tunachangia asilimia 0.084, kuna haja ya kupeleka elimu kwa wananchi ili kuwaongezea mwamko wa kujiunga na huduma za bima kwa sababu matatizo wanayopitia ni kwa sababu wengine hawana bima,” amesema Toyota.
Amesema Serikali imeielekeza TIRA kuongeza mchango wake katika pato la taifa angalau hadi asilimia tano ifikapo 2030. Ili kufikia lengo hilo, tayari wameanza kampeni mbalimbali ikiwemo kutumia vyombo vya habari na mawakala wa bima kuhamasisha jamii kujiunga na huduma hiyo.
Kwa mujibu wa Toyota, takwimu zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya waliojiunga na huduma za bima wanatumia bima za lazima kama vile bima ya afya na bima ya vyombo vya moto (magari na pikipiki). Amebainisha kuwa wanapaswa pia kujiunga na bima ya moto na kilimo iliyogawanywa katika bima ya mseto, hali ya hewa, na bima ya maeneo.
“Takwimu zinaonyesha takribani asilimia 15 pekee ya watanzania (watu milioni 6) ndiyo wana uelewa wa masuala ya bima. Sasa unakuta mkulima ama mfugaji amechukua mkopo Benki ili kufanya kilimo bahati mbaya hali ya hewa inabadilika na kusababisha asipate mavuno.”
“Ukishakosa mavuno tafsiri yake utashindwa kuvuna na kulipa mkopo uliochukua benki ama kwenye taasisi ya mikopo ndipo wanapokuja na kuuza dhamana uliyoweka ikiwemo nyumba ama kiwanja na hatimaye kukuacha ukiwa maskini, lakini kama mkulima amekata bima tafsiri yake atafidiwa hasara na kuendelea kufanya marejesho na kilimo chake kama kawaida,” amesema Toyota.
Amesema nchini kuna watoa huduma wa bima 1,600 huku Kanda ya Ziwa ikiwa na watoa huduma 114 pekee na kutaja mkakati uliopo kuwa ni kuongeza idadi ya watoa huduma wakiwemo mawakala wa bima, benki na mawakala wa bima mtandao watakaofikisha huduma hiyo hadi vijijini.
“Tunatamani watanzania wengi wanunua bima zisizokuwa za lazima, mfanyabiashara awe na bima hata bima ya ajali uwe nayo ili yakikukuta basi usiongeze mzigo kwa watu unaowategemea. Tumeamua badala ya kutumia nguvu basi tutawashawishi watu kuelewa umuhimu wa bima,” amesema.
Wakati Toyota akieleza hali ilivyo kanda ya ziwa, takwimu hizo zinaonyesha soko la bima nchini lilikua kwa asilimia 26.7 mwaka 2022 huku likichangia Sh1.158 trilioni kwenye pato la taifa ikilinganishwa na mchango wa Sh911 bilioni kwenye pato la taifa mwaka 2021.
Akitoa takwimu hizo za kitaifa Desemba 7, 2023, Kamishna wa Bima nchini alisema kampuni 40 zilikuwa zimesajiliwa kutoa huduma za bima mwaka huo ikilinganisha na kampuni 36 mwaka 2022.
Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Stella Marwa amewataka wakulima, wafugaji na wavuvi kuunganisha shughuli zao na huduma ya bima ili kujihakikishia ulinzi na kuepuka hasara wanazoweza kuzipata kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
“Kwa mfano NIC tuna bima ya kilimo ambapo mkulima aliyekopa fedha kwa ajili ya kilimo chake, ikitokea usipate mavuno utafidiwa pale ambapo majanga yanatotea, pia itakuhakikishia uwekezaji wa uhakika kwenye kilimo,” amesema Stella.
Ametaja faida ya kuwa na bima kuwa ni kupunguza msongo wa mawazo na tatizo la afya ya akili kwa mhusika pale janga linapotokea huku akiishauri Tira kuongeza nguvu kwenye utoaji wa elimu kwa Umma kwa kile alichodai wananchi hawajiungi kwa sababu hawana elimu kuhusiana na tija ya bima.
Wakati huohuo, Ofisa wa Bima kutoka Kampuni ya Bima ya Reliance jijini Mwanza, Mwiru Ghati akitolea mfano bima ya nyumba amesema endapo nyumba ya mteja ina thamani ya Sh50 milioni na ripoti ya uchunguzi ikafanyika na kubaini janga hilo limesababishwa na Mungu ‘act of God’ basi atafidiwa Sh40 milioni.
“Nyumba za makazi zote tunamtoza mteja asilimia 0.15 ya thamani ya nyumba husika kwa mwaka mfano kama nyumba ina thamani ya 50 milioni basi atakuwa analipia Sh88,500 kwa mwaka ikitokea imeungua basi tutamlipa fidia Sh40 milioni na yeye atalipia Sh10 milioni,” amesema Ghati.
Amewataka wananchi kutojiunga na bima za lazima peke yake badala yake wajiunge na aina nyingine za bima ikiwemo bima ya jengo la biashara, bima ya madhara kwa jamii na bima ya fedha inayohusisha wafanyabishara wa miamala ya fedha na wenye maduka.
Derewa bodaboda wilayani Nyamagana mkoani Mwanza, Jackson Warioba ametaja changamoto ya ugumu wa maisha kumkwamisha kujiunga na huduma za bima ikiwemo bima ya lazima.
“Sasa hivi maisha ni magumu kila sehemu, hata fedha ya kula kuipata ni changamoto hivi utaweza kutoa fedha kwa ajili ya kulipia bima ambayo hata hivyo unaweza usinufaike nayo endapo hautapata changamoto au janga,” amehoji Warioba.
Kwa upande wake, Mkazi wa Butimba jijini Mwanza, Hilda Mombeki ametaja ukosefu wa elimu kuhusu umuhimu wa kujiunga na huduma za bima ili kupunguza athari na utegemezi pale janga linapotokea.
“Ukipatwa na janga ndiyo utakumbuka umuhimu wa bima lakini kama halijakupata huwezi kujua umuhimu wake, kwa sababu hiyo ndiyo maana unaona bima imekuwa kitendawili kigumu kuteguliwa kuanzia kwa Serikali ama wananchi. Niombe Tira waimarishe utoaji wa elimu kwa Umma itasaidia,” amesema Hilda.