Dar es Salaam. Wakazi wa Magomeni Kota, jijini hapa wamemuomba Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuridhia ombi la kufunga mita kila nyumba katika mradi huo ili iwe rahisi kwao kulipia bili za huduma ya maji, wakieleza ilivyo sasa ni changamoto.
Wakizungumza baada ya Waziri Aweso kutembelea eneo hilo, leo Alhamisi, Julai 4, 2024 wamesema mfumo uliopo si rafiki kwao, kwani kila jengo wanatumia mita moja na bili ikija inakuwa kubwa na baadhi ya watu wanakaidi kulipia huduma hiyo kwa kuwa wapo wengi.
“Baada ya kuona hali hiyo, Waziri Aweso tulisitisha mpango huo kwa kuwaomba Dawasa wasituletee maji kwa kuwa malalamiko mengi unakuta mtu ana familia kubwa na anatumia maji lakini hataki kulipa bili,” amesema Mkazi wa Magomeni Kota, Razaki Johanes.
Naye, Asha Shamir amesema katika majengo hayo wanaishi wananchi wenye vipato tofauti ili kutenda haki kunapaswa kuwa na mita kila nyumba.
“Kuna mwingine hatumii maji mwisho wa siku unampelekea bili nani anaweza kulipa, lazima atagoma, na kuna wengi wanahama hapa kwa changamoto ya maji, Waziri tusaidiwe tufungiwe mita kila nyumba,” amesema.
Akilitolea utatuzi suala hilo, Waziri Aweso amewataka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba waketi pamoja na wakubaliane ili kila nyumba iwe na mita yake.
“Nawaomba Dawasa, TBA na mbunge au viongozi wa Magomeni Kota mkubaliane kwa pamoja ili kila nyumba iwe na mita kuondoa changamoto iliyopo. Maji ni muhimu kwa kila mwananchi na Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa kujenga majengo haya,” amesema.
Vilevile, Waziri huyo ameuomba uongozi wa bonde la Ruvu kesho kwenda kuangalia na kupima katika makazi hayo ili kuangalia sehemu wanazoweza kuchimba visima vya kuwawezesha kupata maji.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba amesema kwa sasa wananchi hao wanapitia changamoto ya maji na hata visima viwili wanavyotumia aliwachimbia yeye.
“Waziri umetoa maagizo nakuahidi nitasimamia kuona mazungumzo haya yanafanyika pande zote ili tatizo la maji liishe katika eneo hili na watu wafurahie maisha,” amesema Tarimba.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule amesema wamekuwa wakifanya mikutano ya mara kwa mara kutafuta muafaka, lakini walio wengi hawataki kutoa fedha kulipia huduma.
“Kulikuwa na kampuni ya ulinzi katika eneo hili lakini juzi imeondoka kwa kuwa ilikuwa hailipwi fedha kulingana na makubaliano waliyoingia,” amesema.
Katika hatua nyingine kabla ya kufika kwenye kota hizo, Waziri Aweso alizungumza na wananchi na wafanyakazi wa Magomeni ambapo, Tarimba amesema baadhi ya maeneo mfumo wa majitaka ni changamoto hasa Kijitonyama.
“Tunaomba waboreshe mifumo ya majitaka, mtusaidie kwenye eneo la majitaka watu waache kutiririsha ovyo kwani wanakamatwa na kupigwa faini,” amesema.
Naye, Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima amewasilisha kero ya kumwagika ovyo katika maeneo yake na imekuwa chanzo cha uharibifu wa barabara wananchi wake wakitoa taarifa watendaji hawaendi kudhibiti.
“Mabomba yamepasuka mengi maji yanatoka kila kona, ni muhimu kutengeneza mfumo wa kugundua mabomba yaliyopasuka maana inawezekana bili hizo zinahamishiwa kwa watu wengine,” amesema.
Katika maelezo yake amesema kusifiana mara kwa mara hakuwezi kuwa suluhisho la kupata maendeleo yanayohitajika, hivyo ameona aeleze ukweli ili hatua zichukuliwe.
Akijibu kero ya maji kumwagika, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mkama Bwire amesema wanaenda kujipanga kwa kutumia teknolojia mpya kuweza kukabiliana na mivujo ya maji ili kulifanya jiji la Dar es Salaam kuwa na mazingira safi na watu kufikiwa na huduma.
“Malalamiko ya wabunge nimepokea. Tunaenda kujipanga kwa kutumia teknolojia kudhibiti mivujo ya maji, na nikuahidi tutakuwa tunashirikiana na viongozi wote ikiwemo nyie wabunge,” amesema.