YANGA imeanza kutoa ‘thank you’ kimyakimya, ambapo imeshawaaga nyota wawili akiwemo kipa, Metacha Mnata na kiungo mmoja, Zawadi Mauya.
Yanga imemuaga aliyekuwa kipa wa timu, Metacha Mnata ambaye hatakuwa sehemu ya kikosi cha msimu ujao wa 2024-25 baada ya kuitumikia kwa msimu mmoja na nusu.
Kipa huyo alijiunga na Yanga, Januari 2023 akitokea Singida Fountain Gate akiitumikia Yanga kwa vipindi viwili tofauti akianzia Agosti 2019 akitokea Mbao FC na baadaye kuondoka kisha kurejea tena 2023.
Metacha hakuwa na safari nzuri aliporejea Yanga, akikosa mechi nyingi, pia akidaiwa kuwa na makosa mengi ya utovu wa nidhamu.
Mbali na kipa huyo pia Yanga imemuaga kiungo Zawadi Mauya aliyemaliza mkataba na mabingwa hao wa soka Tanzania Bara.
Mauya amekuwa akikosa nafasi ya kutosha kuitumikia Yanga ambapo ripoti ya kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi iligoma kumuongezea mkataba.
Mauya aliyetua Yanga akitokea Kagera Sugar, inaelezwa tayari ameshajiunga na Singida Black Stars ambayo ataanza kuitumikia msimu ujao.
Habari kutoka Yanga zinasema, wachezaji hao tayari wameshapewa ‘thank you’ zao ili kuanza maisha mapya nje ya klabu hiyo.
Mabingwa hao mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho wanasemekana kuwa mbioni pia kuachana na Skudu Makudubela, Joyce Lomalisa na Augustine Okrah, miongoni mwa nyota wa kimataifa huku Gift Fred na Joseph Guede wakiwa njiapanda.