Dar es Salaam. Kuelekea maadhimisho ya lugha ya Kiswahili Duniani Julai 7, Wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi na sekondari, walimu, wananchi pamoja na wadau wa lugha ya Kiswahili wamefanya matembezi ya mtaa kwa mtaa kunadi lugha ya Kiswahili.
Matembezi hayo ambayo yameandaliwa na Baraza la Kiswahili Taifa (Bakita) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Mwananchi Communications Limited (MCL) yamefanyika leo Julai 5 jijini Dar es Salaam na yalianza katika eneo la Kinondoni Biafra na kuhitimishwa katika viwanja vya Posta Kijitonyama.
Pia, yalipita katika maeneo ya Kinondoni Manyanya, Studio, Mwananyamala, huku yakisindikizwa na nyimbo mbalimbali zinazohamasisha matumizi ya Kiswahili Sanifu.
Matembezi hayo yalihitimishwa kwa kupekelewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ambaye alikuwa mgeni rasmi pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule.
Kilichowavutia wengi katika maandamano hayo ni namna ambavyo wanafunzi wa rika mbalimbali walivyojitokeza kwa wingi katika matembezi hayo.
Othman Mashaka ambaye ni mmoja kati ya wadau wa lugha ya Kiswahili walioshiriki maandamano hayo, anasema kujitokeza kwa wingi kwa wanafunzi ambao wengi wao ni watoto ni ishara njema kuwa Kiswahili kitaendelea kuenziwa kwani watoto hao ndio taifa la kesho.
Akizungumza baada ya kuhitimishwa kwa matembezi hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Bakita, Consolata Mushi amesema lengo la matembezi hayo ilikuwa kuinadi lugha hiyo pamoja na kuitangaza zaidi siku ya maadhimisho ya Kiswahili duniani.
“Maadhimisho haya ni ya tatu tangu dunia kuanza kuadhimisha Kiswahili hivyo baadhi ya watu bado hawana uelewa hivyo matembezi haya yamelenga kuwakumbusha na kuwahamasisha kushiriki,” amesema.
Vilevile alidokeza lengo la kuweka hamasa zaidi kwa watoto kushiriki matembezi kuwa ni kuwajengea uelewa juu ya fursa zinazopatikana kupitia kukua kwa lugha hiyo pamoja na kuwajengea uzalendo wa kuipenda lugha hiyo.
Akizungumza baada ya kupokea matembezi hayo Chalamila amesema kutambuliwa kwa lugha hiyo kimataifa ni suala ambalo Watanzania wanapaswa kujivunia na kuzungumza Kiswahili sanifu.
Pia amesisitiza Watanzania kutumia maadhimisho hayo kuitangaza nchi pamoja kuitangaza nchi pamoja na fursa zinazopatikana katika sekta mbalimbali.
“Kuna lugha nyingi duniani, kitendo cha Kiswahili kutengewa siku yake maalumu kuadhimishwa kitaifa ni jambo ambalo tunapaswa kujivunia,” amesema.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule aliyesema fursa ya Kiswahili kutambulika kimataifa itasaidia katika kukuza uchumi pamoja na kueneza utamaduni wa Tanzania kimataifa.
Mtambule amesema pamoja na kukuza uchumi pia itasaidia kuzalisha ajira kwa vijana kupitia fursa mbalimbali ikiwemo uuzaji wa maandiko ya Kiswahili mitandaoni, tafsiri na ukalimani, ufundishaji wa lugha hiyo kwa wageni sanaa na nyinginezo.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) Novemba 2021 ilitangaza rasmi Julai 7 ya kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani.