Bodi ya sukari, wazalishaji jino kwa jino

MVUTANO wa utoaji wa vibali za sukari na nakisi umeendelea kushika kasi, baada ya Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) kueleza kuwa wazalishaji hawasemi ukweli juu ya hali iliyotokea mwaka jana na mwaka huu. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Balozi Ami Mpungwe

Kauli hiyo ya SBT inakuja siku chache baada ya Umoja wa Wazalishaji Sukari Tanzania (TSPA), wakiongozwa na Balozi Amme Mpungwe kuitupia lawama Serikali kwa kuchelewa kuwapa vibali vya kuagiza sukari.

Sakata la sukari liliibuliwa bungeni na mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina aliyemtuhumu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kutoa vibali vya kuagiza sukari kwa kampuni zisizo na sifa na kuingiza sukari kwa kiwango kikubwa kuliko nasiki iliyopo.

Mkurugenzi Mkuu wa SBT, Profesa Keneth Bengesi

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa SBT, Profesa Keneth Bengesi amesema kuwa nchi iliingia kwenye tatizo la uhaba wa sukari kutokana na wazalishaji kutoagiza sukari hiyo licha ya kupewa vibali.

Amesema tatizo lililojitokeza mwaka huu lilianza tangu mwaka jana ambapo wazalishaji hawakuleta sukari kama walivyotakiwa kwa kile walichodai hakukuwa na nakisi ilhali uzalishaji wao haukidhi mahitaji.

Amesema mahitaji ya sukari kwa mwaka ni tani 552,000 (bila kujumlisha akiba) ambapo kila siku nchi huhitaji tani 46,000 na uwezo wa uzalishaji wa viwanda vya ndani hazizidi tani 300,000 hivyo huhitajika kuagiza nyingine nje ya nchi.

Amsema kuwa kwa mujibu wa sheria ya sukari ya 2020 na kanuni zake wazalishaji ndiyo wenye jukumu la kuagiza nakisi ya sukari lakini wameshindwa kufanya hivyo hadi Januari mwaka huu na baadhi yao hawakuchukua vibali walivyopewa.

Amesema kutokana na mwenendo huo usioridhisha serikali iliamua kuingilia kati kwa kutumia sheria ya usalama wa chakula kwa kutoa vibali kwa kampuni binafsi kuagiza sukari ili kunusuru wananchi.

Hussein Bashe, Waziri wa Kilimo

“Ukweli hadi Machi 2024 wazalishaji walikuwa wameleta tani zisizozidi 17,000 wakati mahitaji ni makubwa, hizi kampuni za vocha wanazozisema zilikuwa zimeshaleta tani zisizopungua 60,0000”

“Kimsingi serikali haina ugomvi na wazalishaji na wawekezaji, inatambua na kulinda uwekezaji wao lakini si busara kutoa tuhuma za jumlajumla, kama kuna tatizo ningependa waje tukae tuzungumze badala ya kupeana majina yasiyofaa.

Profesa Bengesi amesema mabadiliko yaliyofanyika kwa kuwapa mamlaka ya kuagiza sukari ya akiba Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kunalenga kutatua tatizo la nakisi ya sukari linalojitokeza mara kwa mara.

“Mwezi uliopita tumefanya marekebisho sheria ya sukari ya mwaka 2020, sasa NFRA itakuwa na uwezo wa kuagiza sukari na kuhifadhi kwa ajili ya akiba, tunaamini pia maboresho yaliyofanywa na viwanda vya sukari nchini muda ndani ya miaka miwili ijayo nchi itakuwa inajitosheleza kwa uzalishaji,” amesema

Itakumbukwa kuwa suala la sukari limeshatolewa uamuzi na Bunge ambapo lilijiridhisha kuwa hakuna sheria, kanuni zilizokiukwa katika utoaji wa vibali na waziri Bashe hakusema uongo hivyo.

Bunge lilimuadhibu Mpina kuhudhuria vikao 15 kutokana na kulidharau Bunge na Spika kwa kuuanika hadharani kwa waandishi wa habari ushahidi ambao aliuwasilisha kwa Spika kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Related Posts