Bodi ya Sukari yajibu hoja za wazalishaji utoaji vibali

Dar es Salaam. Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), imejibu hoja za wazalishaji wa bidhaa hiyo nchini walizoziibua Julai Mosi, wakidai hatua yao ya kuchelewa kuagiza sukari, ilitokana na kucheleweshewa vibali na SBT.

Pia waliilalamikia SBT kwamba ilitoa vibali vya uagizaji sukari kwa kampuni zisizostahili, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa SBT, Profesa Kenneth Bengesi, wazalishaji ndiyo waliochelewa kufuata vibali hivyo na hata walipovipata hawakuagiza sukari kama walivyopaswa.

“Tuliwaandikia wazalishaji kuja kuchukua vibali vya kuingiza sukari tangu Machi 20, mwaka jana. Kampuni ya kwanza ilikuwa Kilombero ilichukua kibali Machi 30, 2023,” amesema alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Julai 5, 2024.

Amesema kampuni mbili za Kagera na Mtibwa zilichukua Aprili 14, 2023 na Kampuni ya TPC ilichukua kibali Mei 3, 2023 huku Kampuni ya Bagamoyo haikuchua kabisa kibali.

Ameeleza licha ya kampuni hizo nne kuchukua vibali, ni Kilombero pekee iliyoagiza sukari kwa msimu huo kiasi cha tani 2,380, zingine hazikuagiza.

Kuhusu kampuni zisizostahili kupewa vibali vya kuagiza sukari, Profesa Bengesi amesema kampuni zote zilizopewa zilikuwa na leseni halali za biashara ya chakula, hivyo hoja ya jina la kampuni haina msingi na imelenga kuichafua Serikali.

“Tuliangalia pia uwezo wa kampuni kuleta sukari katika kipindi ambacho kilikuwa kigumu sana kwetu. Cha ajabu ni kuwa kampuni hizo ambazo zimebezwa na zinaitwa kuwa ni za vocha ndizo zilizoingiza sukari na kutuvusha katika kipindi hiki kigumu na sukari kuuzwa kutoka Sh6,500 kwa wastani hadi Sh2,800,” amesema.

Akizungumza na waandishi wa habari Julai Mosi, Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Sukari Tanzania (TSPA), Balozi Ammi Mpungwe, alisema hawakuwahi kufanya makusudi ya kutengeneza nakisi ya sukari kwa masilahi yao.

Badala yake, alisema wamekuwa wakiikumbusha bodi hiyo mara kwa mara kuhusu kuwapatia vibali vya uagizaji wakijua changamoto inayotarajiwa kujitokeza.

Mpungwe alisema pamoja na lawama zilizotupwa dhidi yao, hawakuwahi kupewa nafasi ya kusikilizwa.

Katika hatua nyingine, Profesa Bengesi amesema msingi wa mabadiliko ya Sheria ya Sukari ya mwaka 2001 ni kubaini gharama halisi za uzalishaji wa sukari nchini, hivyo kuwezesha kujulikana kwa bei ya bidhaa hiyo yenye tija na shindani katika soko isiyomuumiza mlaji wa mwisho.

Pia kuweka utaratibu wa upimaji wa ufanisi wa viwanda vya sukari kwa kuzingatia mipango ya maendeleo iliyopo katika sekta ya sukari.

Mabadiliko ya sheria hiyo amesema yamelenga kuhakikisha kunakuwa na uwazi katika mfumo wa usambazaji sukari.

“Tumelenga kuhakikisha nchi wakati wote inakuwa na hifadhi ya sukari kwa ajili ya dharura na kuondoa changamoto zilizopo katika uagizaji wa sukari ya kuziba pengo kwa kuiwezesha Mamlaka ya Hifadhi ya Chakula (NFRA), ambayo haina mgongano wa kimasilahi katika biashara,” amesema.

Amesema kwa mwenendo wa uzalishaji sukari nchini, kufikia mwaka 2025/26 Taifa litajitosheleza kwa bidhaa hiyo.

Profesa Bengesi amesema kama si mvua za El-Nino zilizoathiri uzalishaji wa bidhaa hiyo, kulikuwa na uwezekano wa nchi kujitosheleza mwaka huu.

Ametoa kauli hiyo wakati mahitaji ya sukari kwa nchi ni tani 552,000 bila ziada, huku mahitaji na ziada ni tani 650,000.

Ameeleza hayo leo Ijumaa, Julai 5, 2024 katika mkutano na waandishi wa habari akijibu malalamiko ya wazalishaji wa sukari nchini.

“Kufikia mwaka 2025/26 Tanzania tutajitosheleza kwa uzalishaji wa sukari nchini, hali hiyo ingefikia mwaka huu kama isingekuwa changamoto ya mvua za El-Nino,” amesema.

Kwa mujibu wa Profesa Bengesi, Serikali itaendelea kulinda uwekezaji katika tasnia ya sukari kwa masilahi mapana ya nchi, na kulinda uwekezaji katika sekta hiyo na wadau wengine wakiwemo wakulima wa miwa, walaji na taasisi za kifedha.

“Serikali iko tayari wakati wote na itaendelea kufanya majadiliano na wadau wote wakiwemo wawekezaji katika tasnia ya sukari, ili kupata suluhu ya changamoto zinazowakabili na kutafuta namna bora ya kuzipatia ufumbuzi kwa ajili ya uendelevu wa tasnia ya sukari,” amesema.

Related Posts