Kiungo mshambuliaji kutoka Mombasa – Kenya, Abdallah Hassan Abdallah, ametua rasmi katika klabu ya Coastal Union inayoendelea kujiimarisha katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya 2024/25.
Coastal Union imemtambulisha Abdallah leo Ijumaa Julai 05, 2025 ikiamini mchezaji huyo atafanikisha mipango ya klabu hiyo katika kusaka mafanikio kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Hata hivyo, Abdallah atatakiwa kuthibitisha ubora wake uwanjani atakapopata nafasi ya kucheza, ili kuendana na sifa alizomwagiwa wakati wa utambulisho wake kupitia kurasa za mitandao ya kijamii za Coastal Union.
“ABDALLAH HASSAN ABDALLAH: Winga ya kulia, winga ya kushoto, mjanja mjanja, anapiga kulia anapenya kushoto, baiskeli kama zote, ball control 900%, alianza kuwa mfungaji tangu darasa la pili, nyavu za viwanja vyote vya Ligi Kuu Kenya vinamtambua kwa jina lake, panga pangua timu ya Taifa, what a talented player!!!!!!
“Sasa rasmi ni Mangush, ni red fox na tutafaidi kipaji hiki ndani ya timu yetu, ahsanteni Kenya kwa kipaji hiki. Karibu Tanga fundi wa mpira,” imeeleza taarifa ya Coastal Union iliyoambatana na picha ya utambulisho wa mchezaji huyo.