NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa amewasisitiza Viongozi na Watendaji wa CCM kufanya vikao kwa kufuata miongozo na Katiba ya CCM ya mwaaàka 1977 toleo la mwaka 2022.
Maelekezo hayo ameyatoa katika mwendelezo wa ziara yake na Wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC,CCM Taifa Zanzibar wakati akizungumza na Kamati ya siasa ya Wilaya ya Mjini Kichama.
Amesema Chama Cha Mapinduzi kimeweka utaratibu wa vikao ili Uongozi wa ngazi mbalimbali wapate nafasi ya kujadiliana masuala ya kiutendaji,mikakati na changamoto za maeneo husika ya kiutawala ndani ya Chama na Serikali zake.
Alisema Viongozi hao wanatakiwa kuendeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha Chama ili kuandaa mazingira rafiki ya upatikanaji wa ushindi katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025.
Dkt.Dimwa, amesema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha uhai wa Chama ikiwemo kukagua miradi ya Chama Cha Mapinduzi na kuzungumza na wanachama wa ngazi mbalimbali hasa wa ngazi za Mashina na Matawi.
“Fanyeni vikao kwa kufuata Katiba na miongozo yetu ili kuepuka migogoro na maamuzi yasiyofaa kwani Chama chetu kimeweka utaratibu wa kuhakikisha kila jambo linatafutiwa ufumbuzi kupitia vikao vya pamoja.
Pia nakupongezeni kwa kazi nzuri ya kuimarisha Chama chetu ndani ya Wilaya hii hasa kusimamia vizuri utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.”alisema Dkt.Dimwa.
Akizungumza na wanachama katika maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo alisisitiza ulipaji wa ada ili kupata Wanachama hai.
Alisema CCM inaelekea katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025 hivyo kila mwanachama anatakiwa kujiandaa kwa kuhakikisha anakuwa na kitambulisho Cha kupigia kura.
Naibu Katibu huyo Dkt.Dimwa, alisema CCM inaendelea kuamini mfumo wa ujamaa na kujitegemea hivyo ni muhimu Wanachama wake wafanye siasa na uchumi kwa kubuni na kuendeleza miradi ya kuwapatia kipato cha kila siku.
Aliwapongeza Viongozi wa majimbo ya Wilaya hiyo wakiwemo Wabunge,Wawakilishi na madiwani kwa kazi nzuri ya kuanzisha miradi ya ujasirimali inayowasaidia vijana wengi kujiajiri wenyewe ili kutimiza ahadi ya kutimiza ajira 300,000 kufikia mwaka 2025 iliyoanishwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.