Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dk Doto Biteko amesema wafanyabiashara wengi wadogo wanaokua wanashindwa kujitangaza kutokana na kuogopa kudaiwa mapato ambayo wakati mwingine yanayowaumiza.
Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Julai 5, 2024 wakati akizindua kongamano la wajasiriamali wadogo, wa chini na wa kati (MSMEs) lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) likijadili mada isemayo ‘Kuboresha, kuendeleza ujuzi na kukuza biashara zinazochipukia, ndogo na za kati.’
Dk Biteko amewataka wafanyabiashara ndogo na kati kutumia mitandao ya kijamii kukuza biashara zao na kushirikishana fursa zilizopo ikiwemo namna ya kutatua changamoto na kupata mikakati bora kwa ajili ya maendelso endelevu ya biashara.
Pia ameitaka MCL wazalishaji wa magazeti ya The Citizen, MwanaSpoti, Mwananchi na mitandao ya kijamii kuweka utaratibu wa kufuatilia wale waliokua kutoka hatua moja kwenda nyingine, watangazwe, waonekane kule walipotoka na walipo.
“Tatizo wengi wanajificha kwa sababu mtazamo wa mamlaka za udhibiti mtu akiwa katika Gazeti la Mwananchi ameandikwa amefanikiwa, kwa mfano Simbachawene atoboa alianza na kichanja cha nyanya leo ana shamba anauzia wengine ni tatizo,” amesema Dk Biteko.
Amesema mfanyabiashara huyo aliyempa jina la Simbachawene anaogopa kwa sababu baada ya habari hiyo kutoka kuna ofisa mmoja wa mapato atapiga hodi mlangoni kwake kama vile kufanikiwa ni dhambi.
“Atakuja na hesabu zake atakuambia kwa hesabu hii…, siyo Serikali ni mtu mmoja tu na kwa hesabu hii tunarudi nyuma miaka minne anatengeneza taharuki ili mkae mzungumze watu wa namna hii wanaturudisha nyuma sana,” amesema Dk Biteko.
Amesema kuchukua fedha ya mtu maskini ambaye anaamka mapema akimuacha mkewe nyumbani akatoke jasho ili awalishe aliita ni kitendo cha laana.
“Mtu huyu akatafute pesa kwa ajili yake na familia yake, wewe umekaa ofisini na suti yako unataka uchukue pesa kwa mtu ambaye ametoka jasho utachukua hiyo fedha lakini kwa imani yangu unachukua laana ya watoto wako,” amesema Dk Biteko.
Amesema umefika wakati wale ambao wanafanikiwa waone fahari kwani wanakuwa mifano kwa wengine.
“Na katika mijadala kama hii wanapopatikana mwaka unaofuata wazungumzie changamoto wanazopitia fursa na mafanikio,” amesema Dk Biteko.
Amesema kufanya hivyo kutawasaidia wengine kujifunza kwani sifa inayompa mtu kufanikiwa mwingine hana hivyo wanapokutana wanabadilishana mawazo huku akieleza nidhamu ni moja ya jambo lakini mazingira gani ambayo mtu anaweza kufanya akafanikiwa kuliko mwingine ndiyo kitu kikubwa.
Katika hilo, Dk Biteko amesema wajasiriamali ni lazima watengenezewe mazingira wezeshi katika eneo hilo ili wapambane na umasikini ambao kila mmoja anauchukia.
Dk Biteko amesema wanachotaka watu hao ni mazingira bora na rafiki hivyo jukumu la Serikali ni kuwatengenezea mazingira hayo.
“Serikali inafanya juhudi mbalimbali kama kutoa mikopo kwao mfano imetoa mikopo yenye thamani ya Sh2.3 bilioni, kutengeneza ajira, na hadi kufikia Machi, Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ta Kilimo imetoa mikopo na kuwekeza katika eneo la kilimo na mifugo,” amesema Dk Biteko.