Dar es Salaam. Muda wa zabuni iliyotangazwa kusaka mkandarasi atakayekifanyia matengenezo makubwa kivuko cha Mv Kigamboni umefika mwisho, kampuni mbili za Kitanzania zikijitokeza kuomba kazi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya zabuni hiyo namba X8/2023/2024/W/53 mkandarasi anayehitajika ni atakayekuwa na uwezo wa kufanya ukarabati mkubwa wa kivuko hicho, kwa maana ya kubadilisha zaidi ya asilimia 90 ya vifaa vilivyomo, zikiwamo injini nne.
Hatua ya kutangazwa zabuni imetokana na kivuko hicho kusimamishwa kutoa huduma na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac).
Hata hivyo kiliendelea kutoa huduma licha ya kupitiliza muda wa kufanyiwa matengenezo makubwa hadi pale ripoti maalumu ya uchunguzi ilipochapishwa na Gazeti la Mwananchi kuanzia Mei 25, mwaka huu ikibainisha kivuko hicho na vingine kuhitaji matengenezo makubwa ili kulinda usalama wa watumiaji.
Juni 6, 2024 kupitia kitengo chake cha Masoko na Uhusiano, Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) ilitangaza kusitisha huduma za kivuko hicho kuanzia Juni 7, ikieleza kinakwenda kufanyiwa ukarabati mkubwa.
Hata hivyo, taarifa ya Temesa haikuweka wazi kwamba ni lini hasa kivuko hicho kitapelekwa kwenye matengenezo. Kwa sasa kivuko hicho kimeegeshwa kikisubiri kufanyiwa matengenezo, huku huduma za uvushaji watu, magari na mizigo kati ya Kigamboni na Magogoni zikiendelea kutolewa na kivuko cha Mv Kazi, pamoja na vya Sea Tax vinavyomilikiwa na kampuni ya Azam Marine Ltd.
Meneja wa Vivuko Kanda ya Mashariki wa Temesa, Abdulrahman Ameir akizungumza na Mwananchi leo Julai 5, 2024 amesema zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa kukifanyia matengenezo makubwa kivuko cha Mv Kigamboni ilishatangazwa.
Kwa mujibu wa Ameir, kampuni mbili kutoka Tanzania zimeomba zabuni hiyo na hana uhakika iwapo tayari mchakato wa kukabidhiwa kazi umekamilika au la.
“Waliomba wazabuni wawili wa kampuni za Tanzania na nafikiri hivi karibuni mmoja atakabidhiwa kazi kwa ajili ya kwenda kwenye matengenezo hayo,” amesema.
Hata hivyo, taarifa za uhakika ambazo Mwananchi inazo bado mzabuni hajatangazwa ingawa kampuni mbili zimeomba kufanya kazi hiyo. Miongoni mwa kampuni hizo ni Songoro Marine Ltd.
Kwa mujibu wa tangazo la zabuni, mwisho wa kutuma maombi ilikuwa Julai Mosi, 2024.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Temesa kimeieleza Mwananchi kuwa wiki ijayo mzabuni atatangazwa na anatarajiwa kufanya kazi kwa miezi isiyozidi 10, hivyo inatarajiwa kivuko hicho kitarejea kutoa huduma mwakani.
Tangu kusimamishwa kwa kivuko hicho, huku kingine cha Mv Magogoni pia kikiwa kwenye matengenezo kumekuwa na adha ya usafiri, huku baadhi ya wananchi wakitumia boti za uvuvi kuvuka ng’ambo ya pili.
Mv Magogoni kipo kwenye matengenezo makubwa Mombasa, Kenya tangu Februari mwaka jana.
Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Kamanda wa Kikosi cha Polisi Wanamaji, ACP Moshi Sokoro ilisema ufuatiliaji maalumu uliofanywa na jeshi hilo kuanzia Mei hadi Juni, 2024 katika kudhibiti uhalifu ukanda wa Bahari ya Hindi uliwezesha kukamatwa faiba boti nane zisizo na usajili wala majina zikijihusisha na usafirishaji wa abiria kwa njia hatarishi kati ya fukwe ya Kigamboni na Soko la Kimataifa la Samaki Feri.
Huduma kwa sasa zinatolewa na Mv Kazi na Sea Tax, ambavyo kwa mujibu wa mkataba vinapaswa kufanya kazi kwa saa nane kwa siku.
Licha ya kuendelea kufanya kazi, kivuko cha Mv Kazi kina uwezo mdogo wa kubeba abiria 800 na magari madogo 12 pekee, hivyo kushindwa kuhudumia mahitaji makubwa ya wananchi yaliyopo ambayo ni takriban abiria 60,000 kwa siku.
Wenye magari wanatumia njia mbadala kupitia Daraja la Mwalimu Nyerere ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na Mv Kigamboni kutokuwepo.
Hata hivyo, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), imeshatangaza ruti mpya za daladala kutoka Kigamboni kwenda katikati ya jiji ikihusisha Kigamboni – Stesheni, Kigamboni – Mnazi Mmoja na Kigamboni Muhimbili.
Latra katika tangazo la ruti hizo lililotolewa Juni 21, 2024 kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram wa mamlaka hiyo ilisema daladala zinazotakiwa kuingia barabarani katika ruti hizo ni 20 kwa kila njia, huku vigezo vikiwa kuwa na uwezo wa kubeba abiria kuanzia 25.
Kampuni ya Azam Marine Ltd imesema ipo mbioni kutoa huduma za uvushaji kati ya Kigamboni na Magogoni.
Taarifa kutoka chanzo kinachoaminika zinaeleza kampuni hiyo imekubali kutoa huduma baada ya Serikali kulegeza masharti na kuiruhusu itoze Sh500 kama nauli kwa abiria watakaovushwa na vivuko vyake.
Awali, kikwazo cha uwekezaji huo kilitokana na Serikali kuitaka kampuni hiyo itoze nauli isiyozidi Sh300, hivyo Azam Marine Ltd kuona haina masilahi kibiashara.
Katika mazungumzo kati ya kampuni hiyo, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na Temesa, Azam Marine iliahidi kuwasilisha pendekezo la kufanya uwekezaji katika eneo hilo.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kampuni hiyo, kinaeleza wapo katika hatua za mwisho za makubaliano na kwamba, kabla ya Julai kuisha mikataba inaweza kuwa imesainiwa.
Baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo, Azam Marine Ltd itafanya ujenzi wa pande zote mbili kwa ajili ya maegesho ya boti zitakazotoa huduma na maeneo ya abiria kukaa na kupanda.
“Pia zitachongwa boti mbili au tatu ambazo ndizo zitakazotoa huduma ya uvushaji kati ya Magogoni-Kivukoni,” kimeeleza chanzo hicho.
Kuhusu muda wa kukamilika uchongaji wa boti hizo, chanzo hicho kimesema baada ya siku ya kupewa mkataba, itahitajika miezi minne hadi mitano kwa kazi hiyo.