Chama cha Labour kimeshinda rasmi uchaguzi mkuu wa Uingereza 2024 uliofanyika jana Alhamisi baada ya kufikisha viti 326 vinavyohitajika. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa …(endele).
Katika matokeo yaliyopitiwa na mashirika mbalimbali ya habari yanaashiria kuwa chama cha Labour kinachofuata siasa za mrengo wa kati kushoto kimepata viti 410 kati ya 650 bungeni, huku wahafidhina wa mrengo wa kulia, Conservative, wakimudu kukusanya viti 131 ikiwa kiwango cha chini kabisa kwa chama hicho kwa zaidi ya miaka 100 sasa.
Hatua hiyo inahitimisha safari ya miaka 14 madarakani kwa chama cha Conservative kilicho chini ya Waziri Mkuu Rishi Sunak.
Akizungumza mjini London, Waziri mkuu mtarajiwa Keir Starmer amesema mabadiliko yanaanza sasa.
“Nahisi vizuri, lazima niseme ukweli,” aliuambia umati wa watu waliokuwa wakishangilia.
Akizungumza muda mfupi kabla ya Sir Keir, Waziri Mkuu anayeondoka madarakani Rishi Sunak alikubali kushindwa na kuwaambia wafuasi wake kuwa ulikuwa uamuzi wa kutisha.
Rishi Sunak amesema anakubali kuwajibika kwa kushindwa kwa kihistoria katika uchaguzi mkuu wa chama cha Conservative.
Sir Keir Starmer amekiongoza chama cha Labour kwa ushindi mkubwa na atachukua nafasi ya Sunak kama waziri mkuu wa Uingereza.
Sunak aliwaambia wafuasi wake: “Watu wa Uingereza wametoa uamuzi mzito usiku wa leo, kuna mengi ya kujifunza… na ninawajibika kwa kushindwa huko.”