Same. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema licha ya Wilaya ya Same kulima zao la tangawizi kwa wingi, bado wananchi wake wameendelea kuwa na hali mbaya kiuchumi kutokana na zao hilo kukosa soko.
Amesema maji ya tangawizi nchini Marekani yanauzwa Dola 12 (Sh31,200), hata hivyo kukosekana kwa masoko kumesababisha bidhaa hiyo kutowanufaisha wananchi wa Same ambao ndio wakulima wa zao hilo.
Lema ameyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho leo, Ijumaa Julai 5, 2024, kwenye Operesheni +255 katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Amesema hali ya maendeleo kwa wananchi wa wilaya hiyo ni mbaya ikiwemo kwenye miundombinu ya barabara, upatikanaji wa huduma ya maji safi na hata umeme.
Lema amesema katika wilaya hiyo, baadhi ya wakulima wameshindwa kuvuna tangawizi zao shambani na kuziacha chini ya ardhi kutokana na bei kuwa chini huku akieleza kuwa zao hilo linaweza kujenga uchumi wa wananchi na hata wa wilaya kwa kuwa bei yake katika nchi za nje ni kubwa.
“Hali yenu kiuchumi ni mbaya, mnalima tangawizi kwa wingi lakini hakuna masoko, nimeenda Same Mashariki wanalalamika soko la tangawizi…Wana tangawizi chini ya ardhi hawataki kuzivuna kwa sababu bei iko chini. Tangawizi inaweza kujenga uchumi wa Same kuliko hata ngano, kwa sababu matumizi yake siyo chai tu, inatengeneza hadi dawa zinazopunguza maumivu ya magonjwa sugu kama saratani.
“Tangawizi ina matumizi mengi, ingebadili maisha yenu kiuchumi kwa sababu ni bidhaa na ni kama dawa ya matibabu mbalimbali maana hata wakati wa korona, watu walishauriwa kutumia tangawizi, huku upareni kwa kilimo cha tangawizi tu, hakuna kijana ambaye angeenda mjini kuendesha bodaboda,” amesema.
Amesema uchumi unahitaji maarifa huku akidai kuwa wabunge waliopo wameshindwa kufahamu zao hili lilivyona muhimu kwenye kuboresha uchumi wa wananchi wa maeneo hayo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amesema chama hicho kinaendelea kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu 2025 ambapo katika Mkoa wa kilimanjaro wanahitaji kushinda majimbo yote tisa ya uchaguzi.
“Mwaka 2015, Kilimanjaro tulifanya uamuzi mgumu ambapo Chadema tulishinda majimbo saba kati ya tisa na CCM walishinda mawili, sasa tunarudi kwenye mechi, tukijiamini sana na tuamue leo wenzetu wa Same hamtarudi tena kuibeba CCM ili ifahamu kwamba katika uchaguzi ujao tunawapiga tisa bila,” amesema.
Amesema katika Wilaya ya Same ambayo ina majimbo mawili la Same Mashariki na Magharibi, wanaingia miguu miwili kuhakikisha wanajipanga vizuri ili kuweza kushinda majimbo yote.
Chadema kipo kwenye ziara maalumu ya Operesheni +255 katika Kanda ya Kaskazini kwenye mikoa ya Arusha, Mabyara, Kilimanjaro na Tanga ambapo katika Mkoa wa Kilimanjaro watafanya mikutano katika wilaya zote sita za mkoa huo.