Mafundi nguo wenye ulemavu wapata dili Sabasaba

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Kuona ni kuamini ndivyo unavyoweza kusema kutokana na umahiri unaooneshwa na vijana wenye ulemavu waliohitimu fani ya ushonaji, ubunifu na teknolojia ya nguo kutoka vyuo vya Veta ambao wamepata fursa ya kuwashonea washiriki na watembeleaji wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba.

Vijana hao Riziki Ndumba na Abdi Kipara wenye ulemavu wa viungo ambao wako katika banda la Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA) mbali ya kueleza namna walivyonufaika na mafunzo pia wameweza kuaminiwa na baadhi ya washiriki na watembeleaji wa maonesho hayo kwa kuwashonea nguo na kujiongezea kipato.

Mwandishi wa habari hii alipofika katika banda la Veta walipo vijana hao, alishuhudia Ndumba akishona shati lililokuwa na nembo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Kipara alikuwa akishona suruali.

Mhitimu wa fani ya Ushonaji, Ubunifu na Teknolojia ya Nguo, kutoka chuo cha Veta Songea, Riziki Ndumba mwenye ulemavu wa viungo akimpima mteja kwa ajili ya kumshonea nguo katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba.

“Hili (anamwonesha mwandishi) ni shati la mshiriki kwenye maonesho haya amelileta nimrekebishie na kuna wengine wanataka niwashonee nguo,” amesema Ndumba.

Ndumba ambaye ni mhitimu kutoka Chuo cha Veta Songea amesema alianza mafunzo mwaka 2020 na kuhitimu 2021 na sasa anaweza kushona nguo zote.

“Wakati naanza kusoma nilikuwa sina ujuzi wowote lakini baada ya kufika Veta Songea nilipewa ushirikiano mzuri na walimu wangu, baada ya kuhitimu masomo nimekuwa fundi ambaye nina uwezo wa kushona nguo za aina zote.

Mhitimu wa fani ya Ushonaji, Ubunifu na Teknolojia ya Nguo, kutoka chuo cha Veta Singida, Abdi Kipara, akionesha mabegi aliyotengeneza ambayo anayauza katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba.

“Hakuna kitu kinachoshindikana, kama mtaani kuna mtu mwenye changamoto kama niliyonayo muibue, mpe fursa itakayomsaidia aweze kujitegemea mwenyewe…naamini kila kitu kinawezekana,” amesema.

Amesema jamii inapaswa kuachana na dhana potofu dhidi ya watu wenye ulemavu kwani wana uwezo wa kufanya kazi hivyo kitendo cha kuwaficha kinawatengenezea misingi mibaya ya maisha yao ya baadaye.

“Mashine ninayotumia anaweza kutumia mtu yeyote hata asiye na ulemavu, kazi ninazozifanya anaweza kufanya mtu yeyote na nguo ninazoshona anavaa mtu yeyote, kwahiyo mlemavu anaweza kikubwa ni kumpa ushirikiano na si kumficha ndani,” amesema Ndumba.

Fundi huyo ameishukuru Serikali kwa jitihada za kuwekeza miundombinu katika vyuo vya ufundi stadi hatua iliyowezesha watu wenye ulemavu kunufaika kwa kupata mafunzo.

“Tunaomba Serikali itupatie mtaji na kama inaweza ituajiri, nina uwezo wa kushona nguo zote hata wakiniajiri katika taasisi,” amesema.

Naye Kipara ambaye ni mhitimu kutoka Chuo cha Veta Singia na aliyebobea katika utengenezaji wa mikoba, mabegi amesema awali alianza kusoma fani ya umeme lakini baadaye aliamua kubadilisha na kujifunza ushonaji.

“Vitu ninavyotengeneza ni ubunifu nilioupata Veta ambao umenieletea mafanikio makubwa, mashine ninayotumia ni matunda ya Veta, niliinunua mwenyewe na nimeweza kujenga nyumba ya vyumba viwili,” amesema Kipara.

Baadhi ya watembeleaji wamesema umahiri unaooneshwa na vijana hao ni uthibitisho kwamba watu wenye ulemavu wanaweza na kushauri jamii kuacha kuwabeza.

“Kwa kweli nilipofika hapa nimeshangaa, hivi walivyo (yaani mafundi hao) lakini wanafanya maajabu makubwa. Watu waje Veta waone…naumia sana nikiona mama anazunguka na mtoto mwenye ulemavu na kumtumia kuombaomba wakati angeweza kumleta Veta akajifunza ufundi,” amesema Dina Ibrahim mkazi wa Dar es Salaam.

Naye Agnes Joseph ambaye ni mshiriki katika maonesho hayo amesema; “Kwenye taasisi yetu tunatakiwa tuvae sare kila siku wakati wa maonesho, nilipewa sare za wiki nzima lakini kutokana na mwili wangu ulivyo zote zikawa kubwa. Niliwaza nitapata wapi fundi wa kuzirekebisha lakini wenzangu waliniambia nije banda la Veta kuna mafundi…nimekuja hapa Kipara amezirekebisha vizuri.

Related Posts