Mahakama Kuu Geita kuendelea kusikiliza kesi leo, ikiwemo ya mauaji ya Masumbuko

Geita. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Geita inaendelea kusikiliza kesi za mauaji na leo upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili Zephania Ndalawa, anayeshtakiwa kwa kosa la kumuua mtoto Thobias Masumbuko (12) wanaendelea kutoa ushahidi wao.

Tayari mashahidi saba kati ya 12 wametoa ushahidi na miongoni mwa usahidi uliovutia wengi ni ule wa shahidi wa tatu, Salome Cheyo (9) kumtambua Jaji anayeendesha kesi hiyo kama mtuhumiwa.

Tukio hilo lisilo la kawaida lilitokea Julai 3, 2024 wakati shahidi huyo alipotakiwa kwenda kumuonyesha mtuhumiwa aliyemkimbiza siku ya tukio kama anamkumbuka.

Wakati kikao cha pili cha Mahakama Kuu Masijala ndogo ya Geita kikiendelea, tayari kesi mbalimbali zimesikilizwa na kutolewa hukumu ikiwemo ya Anold Shemasi aliyedaiwa kumuua mtoto wake mchanga kwa kutofanana naye.

Mahakama hiyo ilimhukumu kunyongwa hadi kufa Shemasi baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumuua kwa kukusudia mtoto wake, Anna Shemas mwenye umri wa mwezi mmoja kutokana na mtoto huyo kutofanana naye.

Kikoa hicho cha pili cha Mahakama Kuu kilianza Juni 18, 2024 ambapo kwa wiki mbili mfululizo ilisikilizwa kesi ya washtakiwa watano wanaodaiwa kumuua kwa kumpiga na kitu chenye ncha kali Milembe Suleman (43) aliyeuawa Aprili 26, 2023.

Katika kesi hiyo iliyokuwa chini ya Jaji Mfawidhi Kevin Mhina, mshtakiwa mmoja aliachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha makosa yake huku washtakiwa wanne wakisubiri hukumu inayotarajiwa kutolewa Julai 19, 2024.

Washtakiwa katika kesi hiyo namba 39/2023 ni Dayfath Maunga, Safari Lubingo, Genja Pastory na Musa Pastory waliokutwa na kesi ya kujibu baada ya ushahidi wa watu 29 na vielelezo 19 kutolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka huku washtakiwa hao wakijitetea wenyewe.

Mahakama hiyo pia imemuachia huru Stephano Mlenda (31), mkazi wa Chigunga, Wilaya ya Geita aliyekuwa akishtakiwa kwa kosa la kumuua mtoto wake mwenye umri wa miaka tisa kwa kutokukusudia baada ya kumchapa kwa fimbo alipoiba Sh700 na kwenda kununua soda.

Kesi hiyo namba 12,387 ya mwaka 2024 ilikuja mahakamani hapo kwa ajili ya upande wa mashtaka kuleta mashahidi na kabla ya ushahidi kuanza kutolewa, mshtakiwa alikiri kutenda kosa la kuua bila kukusudia.

Akitoa hukumu hiyo, Jaji Mhina ameeleza kilichotokea siku hiyo ilikuwa lengo la mzazi kumuadhibu au kumuonya mtoto kwa kuwa aliiba pesa na siyo kuua.

Katika kikao hicho, pia kesi iliyokuwa ikiwakabili washtakiwa wanne waliyoshtakiwa kumuua Alphonce Mawazo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita waliachiwa huru baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo.

Juni 18, 2024, kesi hiyo ilianza kusikilizwa upya baada ya Mahakama ya Rufani iliyoketi Mwanza mbele ya majaji watatu, Ferdinand Wambali, Issa Maigena na Leila Mgonya kutengua hukumu ya kesi hiyo na kuamuru ianze kusikilizwa upya baada ya kubaini kasoro za kisheria katika mwenendo wa kesi hiyo Mahakama Kuu.

Mahakama hiyo pia imemuachia huru mshtakiwa Bahati Shija aliyekuwa akikabiliwa na shitaka la kumuua mkewe, Grace Daud kwa kukusudia kwa kumpiga na chuma kichwani baada ya mkewe huyo kukataa kurudiana naye.

Mshtakiwa huyo aliachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kama kweli yeye ndiye aliyemuua.

Leo, kesi inayomkabili Zephania Ndalawa inaendelea kwa upande wa mashtaka kuendelea na ushahidi na wanatazamiwa kufunga ushahidi wao leo na upande wa utetezi wenye mashahidi watatu kuanza kujitetea.

Ndalawa anashtakiwa kwa kosa la kumuua Thomas Masumbuko kwa kumfunga mikono na miguu kisha kumuingizia matambara mdomoni na puani, kitendo kilichosababisha akose hewa na kufariki.

Endelea kufuatilia mitandao ya Mwananchi kwa habari zaidi.

Related Posts