Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa yadhihirisha ukuaji wa Teknolojia Tanzania

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Mosses Kusiluka, amesema kuwa Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara ya mwaka 2024 yameonesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika ukuaji na matumizi ya teknolojia.

Amesema hayo Julai 4, 2024, alipotembelea maonesho hayo yanayofanyika katika Uwanja wa Mwalimu Nyerere, Barabara ya Kilwa. Dk. Kusiluka alibainisha kuwa teknolojia nyingi zilizopo kwenye maonesho hayo zimebuniwa na kutengenezwa nchini Tanzania.

“Watanzania wenyewe tumebadilika, tumechangamka kuwa wabunifu na kukumbatia teknolojia mpya. Naona fahari kuwa Mtanzania. Hata teknolojia za nje zinakuja kwetu kwa sababu wanajua kuna watu watashirikiana nao. Inawezekana ukaja bila wazo ukapata wazo la kibiashara,” amesema.

Amesema mwaka huu kuna washiriki wengi zaidi ukilinganisha na maonesho ya mwaka jana, ambapo ushiriki wa wenyeji ni zaidi ya 3200 na wageni wakiwa zaidi ya wafanyabiashara 400.

“Tumejionea mambo mengi. Tumepita kwenye mabanda ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali na watoa huduma. Tumeangalia teknolojia na ubunifu,” alisema.

Dk. Kusiluka ameongeza kuwa mabanda ya nchi mbalimbali yapo kwenye maonesho hayo, ikidhihirisha kuwa ni maonesho ya kimataifa yanayozidi kukua na kuonesha kuwa nchi inazidi kuaminika.

Amehimiza Watanzania kushiriki katika maonesho hayo ili kuona mabadiliko yaliyopo ukilinganisha na maonesho ya mwaka jana.

“Kuona ni kuamini. Sote tunafahamu ufunguzi umefanywa na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji akiwa mgeni rasmi, akiambatana na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Nawakaribisha Watanzania wote waje kuona maonesho haya,” ameongeza.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara alisema kuwa maonesho ya mwaka huu yamehusisha nchi mbalimbali za kimataifa, zikiwa ni 26 kwa jumla.

Amesema kampuni mbalimbali kutoka nje ya nchi zimeshiriki, zaidi ya 400, na washiriki wa Tanzania zaidi ya 3000, wakihakikisha kuwa maonesho hayo yanafanikiwa kwa kiwango kikubwa.

“Maonesho haya makubwa yameleta taasisi za kimataifa zinazojishughulisha na masuala ya kibiashara. Hivyo, kuna wawekezaji wakubwa wa Kitanzania na wa kimataifa,” alisema.

Ameongeza kuwa wakiwa na mratibu mzuri wa serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, shughuli zote zinaratibiwa. Katika maonesho hayo, kuna kliniki ya biashara na taasisi za kiserikali ambapo mtu akiingia anapata huduma zote.

Amesema maonesho hayo yataendelea hadi Julai 13, ambapo Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, atayafunga rasmi.

Aidha, ametoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi kuchangamkia fursa zilizopo ndani ya maonesho hayo.

Related Posts