Rais Samia atoa sababu kumwondoa Kidata TRA, wadau wafunguka

Dar es Salaam. Uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kumuondoa Alphayo Kidata kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), umetajwa na wadau, unalenga kumuweka karibu zaidi na Rais kwa ajili ya kumshauri namna ya kuyaenenda masuala ya kikodi.

Ingawa wengine wanayatazama mabadiliko hayo kwa sura hiyo, baadhi ya wadau wameona kilichofanywa na Rais ni kupunguza vita aliyokuwa akipigwa, licha ya kazi nzuri aliyokuwa akiifanya.

Msingi wa hoja hizo ni kauli ya Rais Samia wakati akiwaapisha wateule wake Ikulu ndogo Tunguu, Zanzibar leo Ijumaa, Julai 5, 2024 alipomsifu Kidata akisema alifanya vizuri TRA.

Kidata aliyekuwa kamishna wa TRA, juzi Rais Samia amemteua kuwa mshauri wake, huku nafasi yake ikirithiwa na Yusuph Mwenda aliyekuwa bosi wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA).

“TRA chini ya Kidata imefanya vizuri sana, mapato yameongezeka, sitegemei kama yatashuka. Nilimuondoa Kidata niliona mwisho atadata.

“Kazi amefanya vizuri sana niliona mwisho atadata, sasa nakupeleka kijana mtoto wa mjini uhuni wote wa TRA umefanywa na wewe humo humo,” amesema Rais Samia alipowaapisha wateule hao.

Kwa mujibu wa Rais Samia, hivi sasa TRA wanacheza ngoma na kula pilau baada ya Kidata kuondoka na watafurahi endapo Mwenda akifika katika ofisi hizo kwa sababu wanamfahamu.

“Kama unataka kudumu kwa muda mrefu TRA kageuze uso. Jingine Kidata huyu hakuwa mpenzi hata kwa sisi huku, kwa sababu mzigo wangu unakuja Kidata pitisha mzigo, hapitishi hadi ulipiwe kodi.

“Hawezi kuwa mpenzi wa watu, hata sisi huku tulikuwa hatumpendi kabisa,” amesema mkuu huyo wa nchi na kusisitiza kodi italipwa hata kama atakwenda mtu anasema anaitwa Suluhu.

Kutokana na kauli hiyo ya Rais Samia, Mwananchi limezungumza na Mhadhiri wa Biashara wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Omar Mbura aliyetaja sura mbili zinazobeba uamuzi wa Rais kumuondoa Kidata TRA.

Pamoja na ufanisi ulioonyeshwa na Kidata katika utendaji wake, alieleza kuondolewa kwake kumelenga kuwekwa karibu zaidi na mkuu wa nchi ili amshauri kuhusu masuala ya kikodi.

“Kama tunavyoona wakati huu kuna changamoto nyingi za wafanyabiashara kuhusu masuala ya kodi, Rais alihitaji mtu wa kuwa naye karibu kwa ajili ya kumshauri namna ya kuyaenenda mambo hayo,” alisema.

Kwa mtazamo wa Profesa Mbura, Kidata hakuondolewa isipokuwa amewekwa karibu na Rais ashauri na asimamie utekelezaji, hivyo bado yupo lakini kwa nafasi ya ushauri.

Kwa upande wa Mwenda, amesema kuteuliwa kwake ni baada ya kujaribiwa visiwani Zanzibar na kuonyesha umahiri kiasi cha kuongeza mapato.

“Kwa taarifa zilizopo Zanzibar imeongeza mapato yake maradufu, hiyo ni kazi ya Mwenda, kama alikwenda kule kupimwa basi amepimika na amethibitisha uwezo wake, kwa hiyo anakwenda kusimamia eneo kubwa zaidi huku Kidata akisimama kumshauri,” amesema.

Mtazamo wa Profesa Mbura unashabihiana na kilichoelezwa na Mhadhiri wa Fedha, Uhasibu na Kodi wa Chuo cha Serikali za Mitaa Dodoma, Charles Matekele   anayedhani uamuzi huo umelenga kumweka Kidata karibu zaidi na Rais.

Ukaribu huo kwa mujibu wa Matekele, utarahisisha ushauri kuhusu masuala ya kikodi ambayo kimsingi hayatoki TRA pekee, hata katika halmashauri.

“Katika kuboresha utendaji wa TRA atakuwa anapata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwa mtu aliyewahi kuwepo katika mamlaka hiyo,” amesema.

Kwa upande wake,  Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita,  amesema kauli hiyo ya Rais inaashiria changamoto ya kuwajibishana ndani ya Serikali.

Hoja yake hiyo inatokana na kile alichoeleza, haiwezekani anayedaiwa kufanya vizuri umuondoe, akidai huko ni kuoneana haya.

Kwa mujibu wa Mchinjita, katika mazingira ya kawaida anayefanya vizuri, mara nyingi huachwa kwenye nafasi yake ili aboreshe zaidi.

Rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Vincent Minja amesema Rais ana sababu nyingi za kumuondoa mtu kwenye wadhifa wake.

Lakini, amesema kinachoangaliwa na chemba hiyo ni iwapo Mwenda atakuwa na manufaa kwa wafanyabiashara.

“Tunachoangalia uteuzi huu uliokuja una manufaa kwetu wafanyabiashara au hauna manufaa, kama anavyosema sisi tunaona amemuondoa.Unajua unaweza ukawa mzuri lakini ukawa unapigwa vita yule aliyekuteua anaamua akuondoe ili msiendelee kupigana vita,” amesema.

Rais Samia alisema kwa kiasi fulani bosi huyo wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRA) alijitahidi kunyanyua mapato ya Zanzibar na kwamba hivi sasa anapelekwa TRA.

Amemtaka Mwenda kuziba mianya yote ya ukwepaji wa kodi akisema bosi huyo wa TRA anaijua vema kwa sababu alikuwa huko awali.

“Tunakopa tunanyanyasika, twende tukanyanyue za kwetu. Serikali imefanya yote imeweka mazingira mazuri wawekezaji wanakuja, biashara zinafanyika lakini kodi hazilipwi.

“Kariakoo pale tatizo ni kulipa kodi, pale kuna mapato yakikusanywa vizuri kwa mwaka yanaweza kuendesha hata wizara tatu. Lakini mapato hayakusanywi kuingia Serikali, inawezekana yanakusanywa yanaingia mfukoni, nenda kazibe huo mwanya.

Amemtaka Mwenda aliyewahi kuwa Meya wa Kinondoni jijini Dar es Salaam 2010/2015 na wakati huohuo akiwa mtumishi wa TRA kujiandaa na hilo, sio kujifanya mwema kwa kumridhisha kila mtu.

“Yaani kuwa mzuri kwa sisi, kuwa mzuri kwangu niliyekuteua. Nenda kanikusanyie fedha, ukitaka kumridhisha kila mtu hutafanya kazi.

“Nimemuondosha Kidata anakuja ofisini kwangu kazi yake kubwa kukufuata mgongoni, kwa sababu vichochoro vya TRA anavijua. Sasa hivi msaidizi na mshauri wangu katika ukusanyaji wa mapato.

Amemwambia Mwenda asitake kupendwa bali ahakikishe watu wanalipa kodi, hata ikitokea mtu anaitwa Suluhu anataka kupitisha mzigo au chochote alipe kodi, hakuna kukwepa kodi.

Rais Samia amemtaka Dk Jafo kwenda kusikiliza na kutatua kero za wafanyabiashara na kuhakikisha Kariakoo inafanya kazi saa 24 kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali.

Amemtaka Dk Jafo kuhakikisha wafanyabiashara wanakuwa marafiki zake, akisema hataki kusikia wadau hao wanamtafuta waziri hapatikani hasa kama mbunge huyo wa Kisarawe mwenye uwezo wa kuongea na kutembea.

“Ulikuwa ofisi ya Makamu wa Rais, umefanya kazi nzuri, lakini nimeona nikutoe nikupeke biashara maana pilikapilika ni nyingi mno.

“Pale ofisini ulipokuwa ukikaa sitaki ukae, lakini naelewa kwa nini waziri (Dk Kijaji) alikuwa hatoki kwa kazi ninayotaka kukupa ni kushinda Kariakoo panda shuka panda shuka, si rahisi kwa mtoto wa kike na sio kazi rahisi,” amesema.

Rais Samia amemtaka Dk Jafo katika majukumu yake, arejee katika Ilani ya uchaguzi ya CCM inayozungumzia sekta ya biashara na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ili kutoa mchango kwa Serikali.

“Lakini ukarejee kauli yangu kuhusu Serikali kuendelea kufanya kila linalowezekana kusikiliza na kutatua changamoto za wafanyabiashara, ndiyo maana nakwambia uwe karibu nao,” amesema.

Rais Samia amesema Kariakoo ndilo eneo zuri la biashara na muhimu kwa biashara, ndilo linalofanya Dar es Salaam, iitwe kitovu cha biashara, mataifa yote yanakwenda Kariakoo.

“Tumewekeza fedha nyingine kujenga masoko yakikamilika huduma zitakuwa saa 24 Kariakoo, nataka ukaifanye Kariakoo itoe huduma saa 24 yenye usalama wa biashara.

“Utakaa vipi na Jeshi la Polisi au kujipanga hiyo ndio kazi yako, lakini nataka Kariakoo liwe soko la kimataifa, changamoto zilizopo zitatuliwe,” amesema.

Ili kuhakikisha biashara inastawi nchini, Rais Samia amemueleza Dk Jafo kila miezi mitatu anatakiwa ampelekee ripoti kuhusu mwenendo wa biashara Kariakoo na maeneo mengine.

Mbali na hilo, Rais Samia amefichua Kariakoo kuna siasa akisema wakati mgomo uliodumu kwa siku nne kuanzia Juni 24, 2024 alituma timu yake kimyakimya kuzungumza na wafanyabiashara waliosema hawajui kwa nini wamegoma bali wameambiwa kufanya hivyo.

“Tumeambiwa tufunge maduka, tumefunga, tumeambiwa tusiuze hatuuzi, lakini kuna nini ndani hawajui, ukiangalia kwa undani kuna siasa.

“Sasa ili kuondoa siasa, nenda ukakae nao uwasikilize, shida zao na uwasaidie kuzitatua ili Kariakoo kuwa eneo salama la biashara. Biashara ni ‘field’ viatu unavalia njiani sio kazi ya ofisini,” amesema.

Amemtaka pia Dk Jafo kukaa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kuangalia na kujipanga kuhusu ujio wa Kariakoo utakuaje ikiwemo masuala ya usalama.

“Lakini pia kuna suala la machinga wanaoleta kero wakati mwingine wanapanga bidhaa zao mbele ya maduka ya watu wengine.

“Kaeni na mkuu wa mkoa (Chalamila) na polisi kujua mnajipangaje kama mtafunga baadhi ya barabara ili usiku wafanye biashara, lazima wawapishe wenye maduka wanaolipa kodi,” amesema.

Kuhusu Dk Kijaji, Rais Samia amesema anaelewa kulikuwa na uzito fulani ndiyo maana ameamua kumpeleka Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.

“Dk (Kijaji) nimekupa ahueni na mzigo huu wa biashara najua kwa haya usingeyaweza, nimekupeleka kwenye Muungano na Mazingira, kama ulisema mazingira hayakuhusu sasa yanakuhusu tena utafanya kazi kwelikweli,” amesema.

Rais Samia amemtaka Dk Kijaji kulivalia njuga ajenda za nishati safi ya kupikia hususan yeye (Kijaji) akiwa mwanamke wakashirikiane na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Christina Mndeme.

Related Posts