Rais Samia awaomba viongozi wa dini kuhimiza wanaume kuhudumia familia zao

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameshauri mawaidha yanayotolewa kwenye nyumba za ibada yaguse pia wajibu wa mwanaume.

Mbali na hilo, Rais Samia amesema katika dini, Mwenyezi Mungu amewapa nafasi kubwa, wamependelewa na ni walinzi wa nyumba za waume zao na hata kwa wale ambao wanalea watoto peke yao (single mothers) nao ni walinzi wa nyumba zao.

“Kidini Mungu katupa nafasi kubwa, tuna sura yetu peke yetu ambayo wanaume hawana, pia katika Quran Tukufu tumetukuzwa Mungu alitupendelea.”

Hayo ni maneno ya Rais Samia leo Ijumaa Julai 5, 2024 akiwa mgeni rasmi kwenye kongamano la wanawake wa Kiislamu Zanzibar.

Kongamano hilo ambalo ni moja ya matukio yanayofanywa na waumini wa dini hiyo katika kuelekea kwenye maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislamu unaotarajiwa kuadhimishwa Jumapili ijayo kutegemea na mwandamo wa mwezi limefanyika Visiwani Zanzibar likiwa na mada mbalimbali ikiwamo umuhimu wa kulipa kodi katika dini ya Kiislamu, kuwaheshimu viongozi na athari za fitina na uchochezi.

Akichambua mada moja moja zilizokuwa zimewasilishwa awali, Rais Samia amegusia namna ambavyo nyumba za ibada zimekuwa zikiwasema zaidi wanawake na kushauri pia nyumba hizo zitoe mawaidha yatakayowakumbusha wanaume wajibu wao.

Huku akishangiliwa kwa nguvu, Rais Samia amesema hotuba ambazo zinatolewa kwenye nyumba za ibada badala ya kumuelekea mwanamke tu, ni vyema wajibu wa wanaume nao usemwe.

“Ukisikiliza hotuba nyingi ni za wanawake wanafanya hivi mara vile, lakini kuna mengi hapa ya kusemwa, watu hawatunzi nyumba zao lakini hawaambiwi.

“Watu hawatupi raha majumbani tukastarehe, lakini hawaambiwi, sasa zile hotuba za Ijumaa misikitini badala ya kumuelekea mwanamke tuuuu, ni sawa wanawake tusemwe, lakini na wajibu wa wenzetu nao usemwe ili kumpa raha huyo mwanamke katika yale anayopaswa kufanya,” amesema.

Amesema, huwezi kutarajia mwanamke aamke asubuhi, wengi wao hawaendi ofisini na hawana mshahara wa kila mwezi, lakini huyo huyo ahangaike, ajue watoto watakula nini? Watakwenda vipi shule.

“Wakiumwa ahangaike kuwatibu, wewe baba umetoka asubuhi unaaga unatoka, ukiambiwa haya unatoka lakini mchele hakuna unajibu Inshallah Inshallah, hiyo Inshallah haiingii chunguni.

“Unarudi jioni na ukirudi unauliza changu kiko wapi unategemea mwanamke huyu afanyeje? Watu hawatupi raha majumbani tukastarehe, lakini hawaambiwi,” amesema Rais Samia akishangiliwa kwa nguvu hali iliyoondoa utulivu kwa muda na yeye kutamka takbir! Takbir, huku akiwataka washiriki kurudi kwenye mstari wa utulivu.

Rais Samia amesema, mwanamke ni chuo chema akiandaliwa kuwa mwema na kukumbushia historia ya Kiislamu ambayo mwanamke amepewa nafasi maalumu ingawa katika utekelezaji mambo hayaendi sawasawa.

“Kidini Mungu katupa nafasi kubwa, tuna sura yetu peke yetu ambayo wanaume hawana, pia katika Quran Tukufu tumetukuzwa Mungu alitupendelea,” amesema Rais Samia na kutoa hadithi ya Mtume Muhammad.

Amesema, Mtume alipoulizwa nani amheshimu zaidi alisema mwanamke, alipoulizwa mara ya pili akasema mama na mara ya tatu akasema mama.

“Huo sio utukufu jamani? Lakini papo hapo tumepangiwa jukumu la kubeba mimba miezi tisa na kunyonyesha miaka miwili, ingawa wengine hawafikishi, lakini tunatakiwa tuifikishe.”

Pia, Rais Samia waliwapa mbinu ya mbinu ya malezi wanawake wanaolea watoto peke yao (Single Mothers) akisisitiza kama huwezi, kulea peke yako mshirikishe mjomba kwani naye anaweza kukusimamia kwenye nyumba na watoto wakaenda vizuri.

Amesema, mwanamke ni mchunga wa nyumba ya mumewe akisisitiza katika wajibu ambao mwanamke amepangiwa na mwenyezi Mungu ni pamoja na hilo.

“Wale ambao hatuna waume tuko single mother ni wachunga wa nyumba zetu sababu si tuko na watoto hivyo ni wachunga wa nyumba zetu.

“Matendo ya watoto wetu tutakuja kusimamishwa sisi tujibu ilikuaje? Kwa hiyo ndugu zangu tujitahidini, kama upo single mother huyawezi, tumeambiwa hata mjomba anaweza kukusimamia kwenye nyumba yako, watoto wakaenda vizuri,” amesema.

Rais Samia pia aligusia amani, akiwasisitiza Watanzania kuendelea kuilinda iliyopo nchini kwani bila amani amesema hakuna kitakachofanyika.

Akitolea mfano nchi ya jirani bila kuitaja jina, Rais Samia amesema wiki nzima wamekuwa wakipambana kuituliza amani.

Hata hivyo, hivi karibuni nchini Kenya ndiko kulizuka maandamano wananchi wakipinga muswada wa sheria ya fedha wakidai ni wa kibabe na utawatwika Wakenya mzigo zaidi wa ushuru.

“Mungu anatutaka tuishi kwa amani na utulivu, niwambie tu wananchi wenzangu tuendelee kuitunza tunu hii ya amani ili tufanye ibada zetu kwa utulivu.

“Angalieni mifumo ya jirani zetu hapo, wiki nzima wanapambana kuituliza amani ndani ya nchi na hakuna kinachoendelea, kwa hiyo sisi tusifike huko,” amesema Rais Samia.

Amesema, hata mada zilizowasilishwa kwenye kongamano hilo, zimewasilishwa kwa umahiri na weledi akieleza namna ambavyo migogoro inayoendelea kwenye maeneo mbalimbali duniani zimehusiana na mada hizo.

Amesema mada hizo zina mafunzo si tu ya kiimani hata mienendo ya watu katika jamii akisisitiza ni wajibu kuchukua hatua kupambana nayo.

Katika hotuba yake, Rais Samia amegusia wale wanaopiga ramli chonganishi, akisisitiza Serikali haina tatizo na tiba asili, ni nzuri na zimesaidia watu wengi lakini tatizo lipo kwa wale wanaojifanya kutoa tiba asili lakini wakijihusisha kupiga ramli zinazochanginisha, kuleta fitina na mitafaruku kwenye jamii.

“Kupiga ramli chonganishi ni sehemu ya imani potofu, ni dhuluma inayotakiwa kukemewa kwa nguvu hivyo nikuombe mufti na viongozi wote wa dini nchini kuendelea kutoa elimu kwa watu wetu ili wasishawishike na wapiga ramli,” amesema.

Amesema, Serikali itaendelea kuchukua hatua, kwa kuwa mambo hayo ndiyo yanayopelekea hadi watu kuuana.

“Mtu kaambiwa ni bibi yako mchawi, hiki kinachokuuma ni mjomba wako, naye akitoka hapo panga mkononi na kuchinja chinja, tusifike huko, viongozi wa dini endeleeni kufundisha watu,” amesema.

Katika mada ya kuheshimu na kuwatii viongozi, Rais Samia amesema amefurahi mada hiyo imeibuliwa kutoka kwa waliotoa mawaidha.

“Tungeibua sisi viongozi wangesema eeeh wanajiwekea ngao, tusiseme tusiwambie lakini nafurahi imetoka kwa wahadhiri wetu.

“Kwa kuwa imejadiliwa, na mimi nichangie kidogo nijuavyo kwamba qudra na qadar vyote vinatoka kwa Mwenyezi Mungu, yeye akisema lisiwe au liwe linakuwa kama anavyotaka,” amesema.

Amesema anapokuwa akisoma mitandao ya kijamii au kusikiliza hotuba za wanasiasa wenzake jinsi wanavyowachambua na kuwadhalilisha viongozi anapata mashaka kama wamepata malezi ya dini au wanazifanya dini kama ni utamaduni au mila bila kufuata na kuwa na imani ya kweli nazo.

“Mtu aliyesimama na kupata mafunzo ya dini hawezi kusimama akamtusi au kumkashifu kiongozi wake, wale wanaofanya ni kwasababu hawakupita kwenye malezi ya kidini, wito wangu ni viongozi wa dini zote wakae na kufundisha vijana wetu,” amesema.

Amesema majukwaa ya kisiasa yana hamasa na ushawishi, hivyo kuna watu akishakaa kwenye jukwaa hilo maneno yanamtoka.

“Naikumbuka hadithi ya Mtume wetu isemayo ni juu yenu kuwa wasikivu na watiifu kwa viongozi wenu hata kama mtaongozwa na mtu anayetoka kabila la chini, Mungu kaona kuna kitu ndani yake, ndiyo maana kampa uongozi.

Amesema kumheshimu kiongozi sio awe wa juu, hata kwenye makundi ya kawaida kama amechaguliwa kuwa kiongozi heshima iwe pale pale kwa kuwa Mungu kaona kitu ndani yake.

“Lipo funzo kubwa kuhusu umuhimu wa kuheshimu na kuwatii viongozi wetu, sio wa kisiasa hata wa dini na sisi viongozi tunao wajibu wa kuendelea kuishi katika misingi ya uongozi bora.

“Ukisema liwe, ndilo liwe sio leo unasema hili, kesho lile watu watakuwa wanajiuliza mara tatu tatu mbona ana kauli nyingi huyu, pia uwe mweledi wakija watu na shida zao wasikilize na kupata utatuzi ili wananchi waendelee kutuheshimu na kutuamini,” amesema.

Rais Samia alimfananisha kiongozi na mti wa kivuli, akieleza kwamba kwenye huo mti watu wenye shida zao wanatakiwa wafike pale wapumue, japo alisema hiyo pumua ina maana nyingi na wakati mwingine inazidi uwezo.

Katika kongamano hilo, Rais Samia alieleza pia namna alivyofurahishwa na mada ya umuhimu wa kulipa kodi, ambayo alisema inapozungumzia kodi yanazungumzwa maendeleo ya nchi kiuchumi na kijamii.

“Hakuna Serikali inayoendeshwa bila kodi, tunapokusanya zaidi tunapunguza kukopa,” amesema kigusia pia namna jitihada ambazo Serikali inazifanya namna zilivyoweza kupandisha mapato ya kodi Bara na Zanzibar kwenye mwaka wa fedha 2023/24 na kufanikisha kutekeleza huduma za jamii na miradi ya maendeleo.

Awali, Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid  Ally Mfaume akitoa taarifa ya mwaka mpya wa Kiislamu, amesema hii ni mara ya tatu wanafanya madhimisho, walianza mwaka 2022.

Tunakwenda kuadhimisha mwezi 28, mfungo tatu, 1445, maadhimisho haya mwaka huu yalianza Juni 29 kwa kufanya kongamano la mikoa mitatu iliyoshirikisha wilaya zote ya Unguja.

Juni 30, kongamano hilo lilifanyika kwenye mikoa miwili ya Pemba na kushirikisha wilaya zote za huko.

“Julai Mosi, tulifanya matembezi kule Pemba na siku hiyo hiyo tulikuwa na duwa ya kitaifa ilifanyika Gombani, tumekuwa na vipaji vya wasomaji Quran na leo tuna kongamano la wanawake.

Amesema kesho Jumamosi itakuwa ni kilele cha maadhimisho yatakayoongozwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

“Jumapili kama mwezi utaandama, kwani kesho ni mwezi 29 kutakuwa na matembezi makubwa kuelekea viwanja vya Mnazi Mmoja na mgeni rasmi atakuwa ni Spika wa Baraza la Wawakilishi.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Harun Ally Suleiman amemshukuru Rais Samia kwa kuwa mgeni rasmi kwenye kongamano hilo akisisitiza kwamba wanamuomba mwakani pia awepo.

“Pia 2026, 27, 28 hadi 2030 Inshallah utaendelea kuwa pamoja na sisi tunakuombea Mungu atakujalia utaendelea kuwa pamoja na sisi,” amesema waziri huyo.

Kongamano hilo pia liliudhuliwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na wa dini akiwamo Mufti na naibu Mufti wa Zanzibar.

Related Posts