SAKATA LA ALIYECHOMA PICHA YA RAIS: Mawakili wajipanga na rufaa, michango yashika kasi X

Dar es Salaam. Ni siku ya pili Shadrack Chaula (24) ameanza kutumikia adhabu yake ya kifungo cha miaka miwili jela ama kulipa faini ya Sh5 milioni, baada ya kutiwa hatiani.

Chaula alihukumiwa adhabu hiyo kwa kosa la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa Tiktok, japo awali alikamatwa kwa kosa la kuchoma picha ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Chaula ambaye ni msanii wa sanaa ya uchoraji, alihukumiwa adhabu hiyo jana Alhamisi, Julai 4, 2024 katika Mahakama ya Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya na Hakimu Mkazi Mkuu Shamla Sheghailo baada ya kukiri kosa.

Hata hivyo, wakili wake Michael Mwangasa amesema kuwa kwa sasa wanakamilisha utaratibu wa rufaa na sasa kinachoendelea ni kukusanya fedha ili kulipa faini.

Tayari harakati za michango zimeanza kwenye mitandao ya kijamii baada ya Chaula kushindwa kulipa faini hiyo baada ya hukumu kusomwa.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Mwangasa amesema wameanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuomba nyaraka za hukumu na mwenendo wa kesi kutoka Mahakama ya Wilaya ya Rungwe ili kukata rufani Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.

”Tunawasiliana na wadau wengine tufanye juhudi zipatikane pesa ilipwe faini kijana huyo awe huru wakati rufaa yake ikiendelea ili kuweka rekodi sawa,” amesema Wakili Mwangasa.

Kuhusu Chaula kukiri kosa, Wakili Mwangasa amesema upo utaratibu wa kisheria ambao, lazima ufuatwe ili kuondoa uwezekano wa kuelezwa kuwa mtu alikiri kosa kumbe alikuwa kwenye shinikizo na si kwa hiyari yake mwenyewe.

Wakili Mwangasa anaungana na Wakili Michael Lugina kumtetea Chaula ikiwa ni maelekezo ya Wakili Peter Kibatala aliyesema ni muhimu kijana huyo apatiwe msaada wa kisheria.

Kibatala ambaye ni wakili kiongozi kwenye kesi ya Chaula, amesema kwa kuwa mchakato wa rufaa itachukua muda juhudi zinaendelea mitandaoni za kupata fedha kulipa faini.

“Kwa mujibu wa wanaochangisha michango, malengo yao hadi kesho itakuwa imekamilika na Jumatatu asubuhi tutaongozana na mawakili nikiongozana kwenda kulipa faini hiyo na kufanya mchakato wa kijana huyo kuachiwa,” amesema.

Amesema taarifa ya kukata rufaa kwa Chaula imeshawasilishwa mahakamani leo Julai 5,2024 akisisitiza hata kama mtu amekiri kosa nafasi ipo ya kukata rufaa.

“Hata kama mtu amekiri kosa sheria inaruhusu kukata rufaa unaweza kushambulia adhabu, lakini pia kuna tiba za kisheria pale ambapo kuna kukiukwa kwa mchakato wa uliosababisha mshitakiwa kupatikana na sheria, ikiwemo haki ya kusikilizwa, haki ya kuwakilishwa,” amesema Kibatala.

X yachangamka na michango

Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram na X, mwanaharakati wa haki za binadamu Godlistern Malisa ameitisha michango kwa ajili ya kumsaidia kijana huyo.

Kupitia mtandao huo aliandika kuwa kwa saa mbili pekee tayari wamekusanya zaidi ya Sh2 milioni kati ya Sh5 milioni zinazohitajika kwa faini ya Chaula.

“Lengo ni Chaula atoke leo. Tunaamini kufika saa 7 (mchana), litakua limetimia ili faini ilipwe na Chaula atoke leo. Tunamtaka Chaula akiwa huru leo. Pigia mstari neno LEO,”ameandika Malisa kupitia mtandao wake wa Instagram na kuongeza:

“Lakini kumbuka leo ni Ijumaa na ofisi nyingi za umma zinafungwa mapema. Hivyo, juhudi zetu ndio zitakazoamua Chaula atoke leo au aendelee kula mvua hadi Jumatatu. Tuendelee kusukuma ili kufikia lengo kwa haraka, na Chaula atoke leo kabla ofisi za hazijafungwa. Do something to set.”

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Malisa amesema michango hiyo wanaratibu na James Mbowe na wameshawasiliana na baba mzazi wa Chaula, Yusuph Chaula ambaye alikiri kuwa hakutaraji mwanae angekumbwa na adhabu kubwa kiasi kile.

Filamu ya sakata lilivyoanzia

Inadaiwa Juni 30, 2024 katika Kijiji cha Ntokela Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya, Chaula alidaiwa kuchapisha video ikimuonyesha akichoma picha ya Rais Samia Suluhu Hassan huku akitoa maneno makali dhidi ya kiongozi huyo.

Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera alitoa maagizo kwa Jeshi la Polisi mkoani humo kuhakikisha anatafutwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

“Nimeona video ikionyesha mwananchi mmoja wilayani Rungwe akimkashifu Rais Samia. Mimi kama mkuu wa mkoa sijaridhishwa na jambo hilo, kwanza sio utamaduni wa wana-Mbeya kukashifu viongozi wetu wa kitaifa tuwaache wafanye kazi za kutuhudumia ili walete mabadiliko makubwa kwenye jamii.

Shadrack Chaula akiwa chini ya ulinzi baada ya hukumu

“Jambo la pili namuelekeza Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga kuhakikisha anamsaka kijana huyo ambaye ametoa maneno ya kashfa kwa viongozi wetu wa nchi hasa Rais Samia,” amesema.

Polisi wamkamata/ahukumiwa

Baada ya agizo hilo, Julai 2,2024 Kamanda Kuzaga alitangaza kumkamata kijana huyo kwa tuhuma za kuchoma picha ya Rais Samia.

Julai 4, 2024 Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Rosemary Mgenije, aliyekuwa akisaidiana na Wakili Veronica Mtafya walimsomea shtaka linalomkabili kijana huyo.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, upande wa mashtaka ulidai ingawa hauna kumbukumbu ya makosa ya nyuma, uliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa, ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia ya kumdhalilisha Rais wa nchi.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo alipopewa nafasi ya kujitetea, alikaa kimya.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Shehagiro amesema anamhukumu kulipa faini ya Sh5 milioni au kutumikia kufungo cha miaka miwili jela. Hadi muda wa mahakama unamalizika alikuwa hajalipa faini, akapelekwa gerezani.

Related Posts