Serikali yatoa msimamo sakata la Sukari

*Yasema haina mpango wa kuhujumu sekta hiyo

*SBT yasema milango iko wazi kwa wanye malalamiko

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu hali ya sukari nchini na kueleza kuwa haina mpango wa kuhujumu sekta hiyo. Serikali inafanya jitihada kuhakikisha sukari inapatikana ya kutosha kwa bei nafuu.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa, Julai 5, 2024, na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Profesa Kenneth Bengesi, mbele ya waandishi wa habari. Tamko hilo limekuja baada ya mjadala mkubwa uliibuka Bungeni na malalamiko ya wazalishaji wa sukari nchini.

Profesa Bengesi amesisitiza kuwa sukari inayozalishwa nchini bado haitoshelezi mahitaji, na serikali haina nia ya kuingilia mfumo wa uagizaji sukari kama inavyodaiwa. Amesema matumizi ya sukari kwa mwezi ni tani 46,000, hivyo ni muhimu kuwa na kiwango cha kutosha. Hali ya bei ya sukari ilianza kuimarika Februari baada ya serikali kutoa bei elekezi kwa wafanyabiashara.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Profesa Kenneth Bengesi,akizungumza na Wahariri na Waandishi wa habari kuhusu hali ya sukari nchini.

“Serikali itaendelea kulinda uwekezaji kwa maslahi mapana ya nchi, ikitambua umuhimu wa sekta ya sukari katika kukuza uchumi wa wananchi. Pia, itaendelea kulinda walaji, wazalishaji, na wakulima wa miwa ili kuhakikisha kuwa tasnia hii inasalia imara,” amesema Profesa Bengesi.

Ameongeza, “Tunafahamu zinaweza kuwepo changamoto, lakini njia bora zaidi ni kuzitatua. Tutakuwa na historia mbaya sana kama tutaivuruga tasnia yetu. Hoja ya sukari imeibuka tena na sisi, kama wasimamizi wa sukari nchini, tumeona tuje tujibu hoja hizi.”

Profesa Bengesi ameeleza kuwa serikali imekuwa ikifanya mabadiliko ya kanuni za mfumo wa uagizaji sukari tangu mwaka 2015, ambapo ilihamisha jukumu la uagizaji sukari kutoka kwa wafanyabiashara kwenda kwa wazalishaji. Hii ilifanywa ili kuhakikisha kuwa uzalishaji wa ndani hauathiriki.

“Tuliona tuhame kutoka kwa wafanyabiashara kwenda kwa wazalishaji ndio wawe waagizaji. Walipatiwa jukumu hilo la kuagiza sukari kwa mujibu wa sheria, lakini changamoto zilianza kujitokeza mwaka 2022/23,” amesema.

Amefafanua kuwa madai kwamba bodi hiyo ilichelewesha kutoa vibali vya kuagiza sukari kwa wazalishaji wa ndani hayana ukweli wowote. Amesema kamati inayojumuisha wadau kutoka TBS, TPA, Wizara ya Kilimo, na NFRA imekuwa ikishughulikia masuala ya sukari. Changamoto zilianza wakati kampuni mbili ziliposhindwa kuchukua vibali vya kuagiza sukari, hali iliyosababisha bei ya sukari kupanda.

“Tulipofika Oktoba, tulipata taarifa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuwa kutakuwa na El Niño. Tukawaandikia wazalishaji. Tusichafuane bila sababu. Tukiona mtu amepotosha na anajua ukweli, ni wajibu wetu kutoka na kukanusha upotoshaji huo. Ni vizuri kuweka taarifa vizuri na kuweka taarifa sawa.”

“Vivutio ambavyo vimekuwa vikitolewa na serikali ni pamoja na msamaha wa kodi kwenye mitambo na vilainishi, na misamaha katika maeneo mengine. Juhudi hizi zote ni kwa ajili ya kusaidia wawekezaji hawa,” amesema.

Amesema pamoja na kutoa vibali mapema, kampuni hizo za wazalishaji zilichelewa kuingiza sukari kwa muda uliotakiwa na kusababisha uhaba. Profesa Bengesi amesema kuwa serikali haijatoa msamaha wa kodi kwa wafanyabiashara na amewataka watu kusema ukweli.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Profesa Kenneth Bengesi,akizungumza na Wahariri na Waandishi wa habari kuhusu hali ya sukari nchini.

Amesisitiza kuwa Bodi ya Sukari iko wazi na inakaribisha mazungumzo na wadau wote ili kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo. Aidha, amewahakikishia wananchi kuwa endapo hali itaendelea kuwa nzuri bila kutokea changamoto za mvua kama ilivyokuwa mwaka jana, mwaka 2025/2026 hakutakuwa na uhaba wa sukari kwani kuna uboreshaji unaendelea katika viwanda na vipo vipya vinajengwa.

Related Posts