SILAA -NITAFUATILIA WATENDAJI NA MAOFISA ARDHI WATAKAOTAJWA KUWA MWIBA NA CHANZO CHA MIGOGORO YA ARDHI

Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo

Waziri wa Ardhi ,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa ,ametoa rai kwa watendaji na maofisa idara ya ardhi katika Halmashauri nchini ,wafanye kazi kwa weledi na kujiepusha kuwa sehemu ya kukuza migogoro kwenye maeneo yao.

Ametoa tahadhari kwa watendaji wa ardhi watakaobainika kuwa mwiba, ndani ya Halmashauri zao hatosita watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Akifanya majumuisho ya ziara yake mkoani Pwani, katika Samia ardhi klinik ya kutatua migogoro ya ardhi Wilayani Bagamoyo, Silaa aliomba ushirikiano kwa jamii ,kutoa taarifa ya watendaji mwiba ambao wamekuwa sehemu ya migogoro badala ya kutatua migogoro.

“Sijawahi kupata taarifa wala malalamiko ya watendaji wangu kujihusisha na vitendo hivyo, Nachelea kusema kuwa nawapendelea ila nawafuatilia na kama kuna malalamiko nileteeni majina yao ,nitayafuatilia na hatua zitachukuliwa ili kuboresha sekta ya ardhi nchini” alifafanua Silaa.

Silaa alielezea, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akikemea migogoro mipya ya ardhi na kuhimiza suluhu ili kuimaliza migogoro hii, hivyo atahakikisha anaitendea haki wizara ya ardhi kusimamia watendaji kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

“Kutakuwa na Kamishna msaidizi wa ardhi Kaskazini ambayo itabeba wilaya ya Kibaha, Bagamoyo na Kisarawe, ambapo kwa kusini itakuwa wilaya ya Mafia,Mkuranga,Kibiti na Rufiji.

“Nimpongeze sana sana Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Abubabari Kunenge kwa namna anavyoshughulikia migogoro ya ardhi katika mkoa huu, kwani utatuzi wa baadhi ya migogoro hii ni moja ya kazi yake kubwa anayofanya na kampeni ya Tokomeza migogoro Pwani “

Akielezea Kliniki za Ardhi zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini( Samia ardhi Kliniki), Silaa alieleza anatarajia kufanya ziara ya kikazi katika majimbo 30 yenye migogoro mikubwa.

Aliwataka wananchi wajitokeze katika klinik hizo ,ili kusikilizwa na kupata ufumbuzi wa migogoro yao ambapo hata kama yeye hatokuwepo watamkuta Kamishna Msaidizi wa ardhi na wataalamu wa ardhi.

Related Posts