Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania, Exhaud Kigahe amesema licha ya biashara ndogo na kati nchini kutoa ajira nyingi na kuchangia katika pato la Taifa lakini bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo masoko na kukosa mikopo.
Ili kutatua changamoto hizo, amesema wako mbioni kupitia upya sera inayosimamia viwanda vidogo na biashara ndogo ya mwaka 2003 ili iweze kuendana na mazingira ya sasa na kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili.
Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Julai 5, 2024 katika kongamano la wajasiriamali wadogo, wa chini na wa kati (MSMEs) lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) likijadili mada isemayo kuboresha, kuendeleza ujuzi na kukuza biashara zinazochipukia, ndogo na za kati.
Kongamano hili linalofanyika katika ukumbi wa Mlimani City ni la pili kufanyika tangu kuanza kwake na limefunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.
Kigahe amesena sekta ya viwanda vidogo na biashara ndogo ni sekta muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa nchi inatambulika katika kutoa ajira na kuchangia katika uchumi wa nchi.
Amesema kwa mujibu wa takwimu asilimia 95 ya biashara nchini ni biashara ndogo na za kati huku ikiwa ni sekta ya pili katika kutoa ajira nyingi ikiwa ni baada ya kilimo.
Pia amesema sekta hiyo inachangia asilimia 40 ya ajira zote nchinu na asilimia 35 ya pato la taifa.
Pamoja na ufanisi huo lakini bado sekta hiyo inayokabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa dhamana kwa ajili ya kupata mikopo, miundombinu duni ya shughuli na matumizi ya teknolojia duni za uchakataji maligjafi.
“Pia watu hawa wanakosa elimu ujuzi juu ya usimamizi wa biashara, ukosefu soko la uhakika za bidhaa zinazozalishwa,” amesena Kigahe.
Kufuatia suala hilo amesema Serikali imeendelea kutatua changamoto hizo kwa kuhakikisha hatua mbalimbali zinachukuliwa ikiwemo ile iliyofanyika mwaka 2003 ambapo ilitungwa sheria ya viwanda vidogo na biashara ndogo kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa biashara hizo’
“Lakini pia kupitia maagizo yenu kama viongozi wa nchi tunaangalia namna ya kupitia na kuhuisha sera hiyo ili iendane na mahitaji ya sasa na kutatua changamoto hapo juu,” amesema Kigahe.
Amesema tayari afua mbalimbali zimeanza kutekelezwa ikiwemo kuhakikisha Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (Sido) inakwenda wilayani na baadaye katika tarafa na kata walipo kwa wingi.
“Huko kwenye tarafa na kata ndiyo wapi kwa wingi hili linalenga kuhakikusha huduma nzuri inatolewe kwa wananchi ikiwemo utoaji mikopo, mafunzo ya biashara na kusambaza teknolojia rafiki za bei nafuu zitakazosaidia uchakataji malighafi katika maeneo ya chini kuboresha miundombinu katika maeneo ya kazi ili kuendana na mahitaji ya soko,” amesema Kigahe.
Mbali na hilo pia amesema Sido wameanza jukumu la kuhakikisha wanatafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wadogo hao.
“Lakini jukumu hili ni kubwa haliwezi tekelezwa na serikali pekee bali inahitaji ushiriki wa watu wengine ili kusaidia mapambano hayo,” amesema Kigahe.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko amesema wataendelea kufanya kazi na wajasiriamali katika wilaya zote ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
“Tunawakaribisha wadau tuweze kushirikiana ili kutengeneza wajasiriamali wanaoweza kukua kutoka hatua moja kwenda nyingine,” amesema Bomboko.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu amesema wajasiriamali wanaofanya biashara ndogo na za kati kwa Tanzania wanachangia asilimia 95 za biashara zote.
Mbali na mchango wao huo mkubwa, Machumu amesema kuna changamoto kadhaa zinazowakabili ambao kama Kampuni ya Mwananchi wameamua kuja na kongamano hilo lenye lengo la kutafuta suluhisho.
“Urasimishaji, mitaji, masoko, ujuzi, ubora wa bidhaa na matumizi yasiyo sahihi ya faida ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili, hivyo kama Mwananchi tukaona tuje na kongamano hili kuibua hoja zitakazotupatia sera rafiki katika eneo hili,” amesema.