TETESI ZA USAJILI BONGO: Kennedy, Singida BS bado kidogo, Yanga yatua kwa Mzimbabwe

KLABU ya Singida Black Stars, iko katika hatua za mwisho za kuinasa saini ya beki wa kati anayemudu pia kucheza kama kiungo, Kennedy Wilson Juma aliyetemwa hivi karibuni na Simba.

Beki huyo aliyejiunga na Simba, Julai, 2019 akitokea Singida United, aliwatumikia Wekundu wa Msimbazi kwa kwa misimu mitano mfululizo kabla ya kutemwa hivi baada ya kumaliza mkataba akiwa kati ya nyota saba waliopewa ‘thank you’ na kwa sasa ni mchezaji huru.

Jambo hilo limewavutia mabosi wa Singida kumtaka wakiwa mbioni kuipiga bao Coastal Union ya Tanga inayotajwa pia kumnyemelea kuimarisha kikosi kwa msimu ujao ambao itashiriki michuano ya CAF ya Kombe la Shirikisho Afrika.

MAAFANDE wa JKT Tanzania wameanza mazungumzo na mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Charles Ilanfya ili kupata huduma yake msimu ujao. Nyota huyo wa zamani wa KMC, Simba, Mwadui na Ihefu, msimu uliopita alifunga mabao manne katika Ligi Kuu Bara na tayari anataka kuondoka Manungu iliyoshuka daraja baada ya miaka 28 tangu ilipopanda 1996.

MABOSI wa Namungo, wameanza mazungumzo ya kupata saini ya aliyekuwa beki wa kushoto wa kikosi cha Geita Gold, Anthony Mligo.

Mligo ameonyesha kiwango bora msimu uliopita akiwa na Geita iliyoshuka daraja, kiasi cha kuwavutia mabosi wa Namungo wanaoisaka saini yake, huku mwenyewe akiwa yupo tayari kutua huko.

BEKI wa kati wa Mtibwa Sugar, Nassry Kombo ameziingiza vitani timu za Namungo, Pamba na Dodoma Jiji zinazohitaji saini yake.

Nyota huyo aliyeanzia timu ya vijana ya Mtibwa kisha kupandishwa kwa wakubwa, amekuwa na kiwango kizuri kwa msimu uliopita na licha ya kikosi hicho kushuka daraja, amezivutia klabu mbalimbali.

TANZANIA Prisons iko mbioni kukamilisha uhamisho wa aliyekuwa kiungo mkabaji wa Geita Gold, Selemani Ibrahim ‘Boban’.

Nyota huyo wa zamani wa Mbeya City, tayari amefanya mawasiliano na viongozi wa Prisons na inaelezwa kila kitu kimekamilika, hivyo kinachosubiriwa ni kusaini mkataba wa kukichezea kikosi hicho.

SIMBA Queens inaelezwa ipo hatua za mwisho kukamilisha dili la beki wa kushoto wa Yanga Princess, Wincate Kaari. Beki huyo raia wa Kenya amemaliza mkataba na Yanga hivi karibuni na Simba imemshawishi kujiunga nayo ikiwa na ofa mara mbili zaidi ya alichokuwa analipwa Yanga.

KIUNGO wa Fountain Gate Princess, Priviledge Mupeti, raia wa Zimbabwe ni kati ya majina ya nyota ambao wanatakiwa na kocha mpya wa Yanga, Edna Lema kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL). Ikumbukwe mchezaji huyo ameomba kuondoka klabuni hapo akidai malimbikizo la mishahara.

MFUNGAJI Bora wa Ligi ya Vijana (U-20) msimu wa 2022/23, Athuman Makambo yupo kwenye hatua za mwisho kujiunga na wanajeshi wa JKT Tanzania.

Kwa sasa straika huyo yupo huru baada ya kumaliza mkataba na Mashujaa aliowatumikia msimu uliopita.

Related Posts