THRDC yataja maeneo sita yanayoongoza kwa uvunjifu wa haki za binadamu

Dar es Salaam. Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa ametaja maeneo matano yanayoonyesha viashiria vya uvunjifu wa haki za binadamu likiwemo eneo la uhuru wa habari na kujieleza, akisema bado kuna sheria kandamizi.

Maeneo mengine ni pamoja na haki ya kukusanyika, na kujumuika, ushiriki wa wananchi, kutobaguana na kujumuisha na haki za binadamu na utawala wa sheria.

Akizungumza leo Julai 5, 2024 wakati wa kuwasilisha ripoti ya hali ya watetezi wa haki za binadamu na nafasi ya kiraia nchini ya mwaka 2023 jijini Dar Salaam, Olengurumwa amesema licha ya nia nje ya viongozi wa Serikali, bado zipo sheria kandamizi zinazokwaza haki ya Watanzania kuwa na uhuru wa habari na kujieleza.

“Tumelifuatilia uhuru wa habari na kujieleza, tumeona tunayumba kwa sababu viongozi wana nia njema lakini sheria bado zimebaki vilevile,” amesema.

Amezitaja Sheria ya Makosa ya Mitandao, Sheria Huduma za habari, Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui Mitandaoni), Kanuni za Mawasiliano ya kielektroniki na Posta na Sheria ya Takwimu akisema zinakwaza uhuru wa watu.

“Sheria hizo zinawapa mamlaka wenye mamlaka kukandamiza upinzani na kupunguza uwezo wa raia kujieleza, kushirikiana na wengine na kukusanyika kwa amani,” amesema. 

Kuhusu haki ya kukusanyika, amesema licha ya Serikali ya awamu ya sita kuruhusu mikutano ya hadhara pamoja na kuzipa uhuru asasi za kiraia, bado uhuru huo unaathiriwa na mfumo wa kisheria, mazingira ya kisiasa na mambo ya kijamii na kiuchumi.

“Rais alifanya juhudi za makusudi kuhakikisha kwamba haki ya uhuru wa kukusanyika inatekelezwa, tumeshuhudia kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara nchini, hata hivyo haki hiyo ya kikatiba imenyimwa kwa wananchi wa eneo la Mamlaka ya Ngorongoro,” amesema.

Kuhusu ushiriki wa wananchi, amesema licha ya juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na makundi mbalimbali ya wananchi, bado mifumo ya sheria siyo shirikishi.

“Bado watu wanalalamika hakuna ushirikishwaji wananchi, kwa mfano katika utungaji wa sheria. Hivyo ushirikishwaji wa wannchi uko chini,” amesema.

Kuhusu Haki za binadamu na utawala wa sheria, amesema licha ya Rais Samia kuunda Tume ya Haki za Jinai ili kuboresha utoaji wa haki, bado kuna haja ya kufikia mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

“Badala ya kurekebisha sheria moja moja, tunaweza kuua ndege wengi kwa jiwe moja kwa kubadilisha Katiba na hapo sheria zitabadilishwa,” amesema.

Kwa upande wake Ofisa Program wa THRDC, Paul Kisabo amesema taasisi hiyo imekuwa ikisaidia watetezi wa haki za binadamu, ambapo kwa mwaka 2023 jumla ya watetezi wa haki za binadamu 100 walisaidiwa kwa kupewa uhamisho wa muda mfupi, matibabu, msaada wa kisheria na msaada wa kisheria.

“Jumla ya watetezi 42 walio hatarini yaani wanawake sita na wanaume 36 walipata msaada wa kisheria wa moja kwa moja kutoka THRDC na watetezi 15 milioni mwao waliachiliwa na mahakama kwa kushinda kesi.

“Kesi dhidi ya mtetezi mmoja aliyeshindwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini ya Sh7 milioni. Hata hivyo Julai 2 aliachiliwa kutoka gerezani baada ya kulipa faini ambayo alichangiwa na marafiki zake kutoka mtandao wa X,” amesema.

Related Posts