Ushahidi kinzani wa mtoto ulivyomnusuru mfungwa maisha jela

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imemuachilia huru mkazi wa Nyarugusu wilayani Kasulu Mkoa wa Kigoma, Alonda Ekela aliyekuwa akitumikia kifungo cha maisha jela kwa kosa la ubakaji, baada ya kubaini kuwa ushahidi uliotolewa na mashahidi wawili ulikuwa ukipishana.

Katika kesi ya msingi, Alonda alishtakiwa kwa kosa la ubakaji chini ya kifungu cha 5(2) (e) cha Sheria ya Makosa ya Kujamiana (Sospa) namba 4 ya mwaka 1998, akidaiwa kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 7, ambaye alikuwa ni ndugu na majirani.

Alidaiwa kuwa kutenda kosa Januari 16, 2007 muda wa saa 5 asubuhi, eneo la kambi ya wakimbizi Nyarugusi Nyarugusu wilayani Kasulu mkoani Kigoma na alikutwa na hatia na kufungwa maisha jela.

Hata hivyo, alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora rufaa namba 01/2014, akipinga hukumu hiyo ya Mahakama ya Wilaya.

Mahakama hiyo katika kikako chake ilichoketi Kigoma kusikiliza rufaa aliyoikata Alonda imemuachilia huru baada ya kushinda rufaa hiyo ambayo ni ya pili, ikiwa ni miaka 17 baadaye, akiwa jela akitumikia adhabu hiyo.

Hukumu hiyo imetolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Mwanaisha Kwariko (kiongozi wa jopo), Zephrine Galeba na Dk Benhajj Masoud, Juni 28, 2024 baada ya kukubaliana na rufaa yake hiyo.

Kilichomnusuru ni kusigana kwa ushahidi wa mashahidi wawili muhimu yaani mtoto mwathirika mwenyewe na dada yake mkubwa, kuhusu namna mshtakiwa/mrufani alivyomchukua na kwenda naye kwake alikodaiwa kumfanyia ukatili huo, hasa usahidi wa dada ambao ulitofautiana na wa mdogo wake.

Katika hukumu hiyo, majaji hao wamesema kuwa ni kanuni ya kisheria kwa panapokuwa na mkanganyiko katika ushahidi wa upande wa mashtaka, mahakama inaamuriwa kuujadili mkanganyiko huo iwapo ni jambo dogo au la.

Imesema kuwa kwa mtizamo wake mkanganyiko huo kutoka kwa mashahidi hao muhimu si jambo dogo kwa kuwa unaathiri kuaminika kwa mashahidi kwa mashahidi hao iwapo mrufani alimchukuwa mtoto huyo nyumbani kwao na kwenda kumbaka na kuibua mashaka kwa ushahidi wa upande wa mashtaka.

“Kutokana na uchambuzi huu, tunaamua kuwa sababu ya tano ya rufaa ina mashiko. Hatimaye tunaamua kuwa kesi ya upande wa mashtaka haikuthibitishwa bila kuacha mashaka”, imesema Mahakama ya Rufani katika hukumu yake hiyo na kuhitimisha:

“Hivyo tunaikubali rufaa, tunatengua hatia na kutupilia mbali adhabu kifungo cha maisha jela iliyotolewa kwa mrufani. Mwishowe tunaamuru kuachiliwa huru kwa mrufani kutoka gerezani isipokuwa kuendelea kushikiliwa kwake kunahusiana na sababu nyinye halali.”

Mtoto huyo kwa mujibu wa ushahidi wake siku ya tukio Januari 16, 2007, alikuwa nyumbani pamoja na dada yake mkubwa. Wazazi wao walikuwa msibani kwenye mazishi na mshtakiwa alifika nyumbani kwao hapo na akamkuta akiwa na dada yake mkubwa.

Mshtakiwa alimuomba amfuate nyumbani kwake kumsaidia kuchota maji naye kwa kuwa mshtakiwa ni ndugu yao alikubali akaambatana naye kwenda nyumbani kwake na alimuacha dada yake nyumbani.

Baada ya tukio hilo lililodaiwa la kubakwa alirejea nyumbani akamkuta dada yake mkubwa lakini hakumweleza kuhusu suala hilo.

Lakini dada yake kwa mujibu wa ushahidi wake, siku hiyo ya tukio Januari 16 majira ya saa tano alikuwa nyumbani na mdogo wake na wazazi wake walikuwa wamekwenda kuhudhuria mazishi.

Akiwa hapo nyumbani alibaini kuwa mdogo wake huyo alikuwa haonekani nyuimbani na akaanza kumtafuta. Watoto wadogo waliokuwa wakicheza nje ya nyumba yao walimweleza kuwa walimuona mshtakiwa akiwa na mdogo wake huyo na kwamba walikuwa wakielekea nyumbani kwa mshtakiwa.

Hivyo alimfuata mdogo wke huyo nyumbai kwa mshtakiwa ambako alikuta mlango ukiwa umefungwa. Aligonga mlango lakini mshtakiwa hakufungua mlango. Hivyo aliamua aliamua kurejea nyumbani na kisha akaenda huko kwenye mazishi.

Baadaye alirejea nyumbani saa mbili usiku akamkuta mdogo wake huyo amesharudi nyumbani.

Mahakama baada ya kurejea ushahidi huo mahakama imesema kuwa unaonesha maelezo tofauti kabisa ya matukio baina ya mtoto na dada yake.

Imesema kuwa wakati mtoto alisema kuwa mshtakiwa/mrufani alimchukua nyumbani kwao mbele dada yake, lakini ni tofauti kwa dada yake ambaye hakusema kuwa alimuona mrufani nyumbani kwao siku hiyo.

Mahakama pia imesema kuwa mtoto huyo alisema kuwa wakati mrufani anambaka alilikuwa analia kuomba msaada, lakini hakusema kwamba alisikia mtu akigonga mlango wa nyumba ya mrufani, kwa vile dada yake alisema kuwa alikwenda nyumbani kwa mrufani na akagonga mlango bila majibu.

Imeongeza kwamba na wakati mtoto huyo alisema kuwa aliporudi nyumbani baada ya tukio hilo, alimkuta dada yake nyumbani, dada yake alisema alikuwa amekwenda kwenye mazishi na kwamba aliporejea ndipo alipomkuta mdogo wake nyumbani.

Katika kesi ya msingi, Alonda alidaiwa kuwa alimchukua mtoto huyo nyumbani kwao na kwenda naye kwake ili kumsaidia kuchota maji lakini alipofika kwake alifunga mlango akampeleka mtoto huyo kitandani chumbani kwake, akamvua nguo na kumbaka.

Mtoto huyo alihisi mauvumi akatokwa damu sehemu zake za siri huku akilia kuomba msaada na baada ya kumaliza mshtakiwa alimpa Sh50 akamtaka asiseme kwa mtu yeyote kuhusu tukio hilo.

Baada ya kurejea nyumbani dada yake alibaini kuwa nguo zake zilikuwa na damu na alipomuuliza mtoto huyo alielezea kile alichofanyiwa na mshtakiwa/mrufani na dada yake alikwenda msibani kumweleza baba yao kuhusu tukio hilo.

Suala hili liliripotiwa kwa walinzi wa kimila ambapo mtuhumiwa alikamatwa na kupelekwa kituo cha polisi, kisha mtoto huyo alipelekwa hospitalini ambako alifanyiwa vipimo na ikathibitishwa kuwa alikuwa amefanyiwa ukatili wa kingono.

Katika kituo cha polisi mtuhumiwa alihojiwa na Ditektivu Koplo (DC) Alusante (shahidi wa nne) akakiri tuhuma hizo na DC Alusante aliandika maelezo yake mtuhumiwa ambayo yalipokewa mahakamani kuwa kielelezo cha upande wa mashtaka.

Baadaye mtuhumiwa alifikishwa mahakamani akapandishwa kizimbani na kusomewa shtaka hilo.

Mshtakiwa kwa upande wake, ambaye alikuwa shahidi pekee wa upande wa utetezi, katika utetezi wake alidai kuwa siku ya tukio hilo alikuwa nyumbani mpaka kwenye saa 2:00 usiku alipokamatwa na walinzi wa jadi kwa tuhuma za ubakaji.

Hata hivyo Mahakama ya Wilaya ilimtia hatiani mshtakiwa na ikamhukumu adhabu hiyo ya kifungo cha maisha jela.

Alonda alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora rufaa namba 01/2014, akipinga hukumu hiyo ya Mahakama ya Wilaya.

Mahakama Kuu iliihamisha rufaa hiyo kwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Kigoma, kusikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Anna Magutu, aliyepewa mamlaka ya ziada kusikiliza rufaa hiyo.

Hakimu Magutu katika hukumu yake ya Agosti 5, 2016, aliitupilia mbali rufaa hiyo kwa kile alichoeleza kuwa sababu za rufaa hiyo hazikuwa na mashiko.

Alonda alikata rufaa hii ya pili Mahakama ya Rufani, rufaa namba 223/2022, akitoa sababu sita, lakini mahakama hiyo imekubaliana na sababu moja tu hiyo ya mkanganyiko wa ushahidi huku ikitupilia mbali sababbu nyingine tano.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, Alonda alijiwakilisha mwenyewe. Hivyo aliiomba mahakama izingatie sababu zake za rufaa kama alivyoziwasilisha kwenye hati ya sababu za rufaa na hakua na lolote la kuongeza, lakini mawakili wa Serikali walipinga rufaa hiyo na sababu zote za rufaa.

Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Shabani Juma Masanja, akisaidiwa na mawakili wa Serikali Antia Julius Muchunguzi na Naomi Joseph Mollel

Related Posts