Utafiti wabaini miti yenye uwezo wa kuua wadudu waharibifu wa mazao

Dar es Salaam. Uhifadhi wa mazao baada ya kuvunwa, yakiwamo mahindi huenda ukawa rahisi baada ya utafiti kubaini aina ya miti inayoweza kutumika kuua wadudu.

Miti hiyo inayopatikana maeneo tofauti nchini baadhi imebainika kuwa na uwezo wa kuua wadudu na kuwafukuza  ndani ya muda mfupi kama ilivyo kwa dawa za viwandani.

Utafiti huo umefanywa na Imani Macha kutoka Idara ya Sayansi Asilia na Hisabati Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (Muce),  ukilenga kupunguza kiwango cha mazao kinachoharibika baada ya mavuno.

Akizungumza na Mwananchi kwenye Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba, Macha amesema utafiti huo uliofanywa katika aina 11 za mimea uliangalia usalama wake na ufanisi, ukiwemo uwezo wa kuhifadhi mazao baada ya kuvunwa.

“Katika mimea tuliyoifanyia utafiti, kuna baadhi inaweza kuua wadudu kwa haraka na ufanisi wake ni sawa na zile dawa za viwandani na baadhi ya mimea tulibaini haiui,  lakini inaweza kulinda mazao yasishambuliwe na wadudu,” amesema Macha.

Amesema dawa ambazo haziui wadudu zimeonyesha ufanisi katika kuwafukuza  wasiwe na uwezo wa kusogelea mazao kabisa.

Macha amesema anaamini utafiti huo  utasaidia watu kuondokana na kuharibika kwa mazao baada ya mavuno jambo ambalo limekuwa likiumiza wakulima wengi katika maeneo tofauti nchini.

Ameitaja baadhi ya mimea iliyobainika kuwa na uwezo wa kuua wadudu kwa kupitia majina yanayojulikana zaidi na watu wa mikoa ya kusini mwa Tanzania ni chimuhumbila, mkungu, msegesi, majegejo na lipuda.

“Hiyo ni kwa mujibu wa majina yanayotumiwa na watu wa kusini lakini kila mmea nilioutaja una jina lake la kisayansi ambalo linatumika dunia nzima,” amesema Macha.

Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (Tari) Kituo cha Kihinga, Dk Filson Kagimbo amesema upo uwezekano wa mimea kuua wadudu, akikiri kuwa wapo baadhi ya watu ambao wameshafanya tafiti eneo hilo.

“Inawezekana na wapo watu tunawajua wamefanya utafiti eneo hili na dawa zao zinafanya vizuri sokoni,” amesema Dk Kagimbo.

Wakati huohuo, kilimo cha muhogo kimebadilisha mitazamo ya wananchi wa Kanda ya Ziwa baada ya kufanyika utafiti wa matumizi mengine ya zao hilo tofauti na yanayotumiwa na wengi hivi sasa ikiwamo kutengenezea mikate, keki na biskuti.

Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Kalwiza Kihenza amesema awali wananchi walikuwa wanalima mihogo kama zao la ziada kwa sababu halihitaji mvua nyingi.

“Watu walikuwa wanatumia zao hili kipindi ambacho kuna ukosefu wa mvua kwa ajili ya kupunguza njaa lakini sasa imekuwa ni fursa na limepewa thamani kubwa kwa Kanda ya Ziwa,” amesema.

Amesema zao hilo limepanda thamani baada ya kupatikana mbegu mpya ya Taricass4 ambayo inatumia miezi tisa hadi 12 hadi kuvuna.

“Kwa kuwa kumekuwa na hamasa kwenye kilimo cha mihogo, Simiyu wameanzisha kiwanda ambacho kinasaga unga wa muhogo na kusambaza katika maeneo mbalimbali,” amesema Kihenza.

Amesema wapo wafanyabiashara wanaosafirisha unga wa muhogo kwenda nje ya nchi zikiwamo Uganda, Congo (DRC) na Burundi.

Hata hivyo, amesema kumekuwa na changamoto ya uwepo wa mashine za kusaga mihogo, hivyo wanaojishughulisha na biashara hiyo wanajikuta wakitumia muda mrefu kukata vipande vidogovidogo (makopa).

Mkulima wa mihogo mkoani Geita, Edward Misungwi amesema ameanza kilimo cha mihogo mwaka 2022 na amekuwa akiwauzia mbegu wananchi na Halmashauri ya Geita.

Amesema mwaka 2023 alilima ekari moja na alipata faida ya Sh4 milioni, akahamasika kuongeza ekari nyingine tano ambazo anatarajia kuvuna mwaka huu.

“Utafiti wa mbegu mpya ni chanzo cha hamasa ya ulimaji mihogo kwa wingi kwa sababu ya upatikanaji wa mashina 12 hadi 14 kwenye muhogo mmoja hivyo kunakuwa na faida ya kutosha tofauti na mihogo ya awali,” amesema Misungwi.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka amesema maonyesho hayo ni kielelezo kuwa Tanzania imepiga hatua katika ukuaji na matumizi ya teknolojia.

“Watanzania wenyewe tumebadilika, tumekumbatia ubunifu na teknolojia mpya. Naona fahari, hata teknolojia za nje zinakuja kwa sababu wanajua wapo watakaoshirikiana nazo, inawezekana ulikuja bila wazo lakini ni inawezekana kushirikiana na wengine kupata mawazo,” amesema.

Related Posts