WAFANYAKAZI Wastaafu wa Shirika la Umeme Tanzania-TANESCO (UWAWATA)wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kutambua uwezo na taaluma zao katika kuendeleza na kukuza Maendeleo nchini.
Akitoa rai hiyo Leo Julai 04,2024 Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa UWAWATA, Boniface Njombe amesema kwa kutambua taaluma za umoja huo bado wanaimani wanamchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza uchumi wa Taifa la Tanzania katika nyanja mbalimbali.
Hata hivyo ameongeza kuwa umoja huo umejumuisha wastaafu wenye taaluma tofauti tofauti ikiwemo Wahandisi,Madaktari, Wahasibu, Mafundi na kutoka mikoa Mbalimbali nchini ikiwemo Kigoma, Mbeya,Tanga,Dar es Salaam,Kagera .
Njombe amesema kutokana na taaluma zao wamemuomba Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwapa majukumu ili waendelee kutumia ujuzi na maarifa katika kusukuma gurudumu la uchumi wa Taifa.
Kwa Upande wake Katibu wa Umoja huo James Elijachinula amesema Umoja huo umekuwa na manufaa mengi kutokana na kukusanyika kwa fani tofauti tofauti .
“Umoja huu umejitosheleza Kuna Wahandisi, wataalamu wa Rasilimali watu,Wanasheria na fani nyingine hivyo umoja huu unaweza kufanya Kazi na upo tayari Kumsaidia Mama Kuendana Kasi ya Kukuza uchumi hivyo tupo tayari Mama yetu Dkt.Samia Suluhu Hassan kutupa Majukumu tuyafanyie Kazi ipasavyo wala asiwe na Wasiwasi na Umri wetu.” Amesema.
Pia ameongeza kuwa umoja huo una wanachama zaidi ya 141 na wanatambulika kisheria.
Katibu wa Umoja wa Wafanyakazi wastaafu Shirika la Umeme Tanesco (UWAWATA) James Elijachinula akizungumza machache mara baada ya kufunguliwa rasmi kwa Mkutano wa umoja ukijumuisha wastaafu wa fani mbalimbali kutoka nchini nzima