VIKWAZO VINAVYOWAKWAMISHA WANAWAKE WENYE ULEMAVU KUSHIRIKI KATIKA MICHEZO.

Wanawake wenye ulemavu uwe wa viungo, wasioona, viziwi, walemavu wa akili na aina nyingine za ulemavu wana haki na wanaweza kushiriki katika michezo mbalimbali kama vile Mpira wa miguu (Amputee Football), kuogelea, kukimbia, kurusha Tufe, Mishale, mbio za Baskeli za Maringi matatu (3) na michezo mengine kama walivyo wanawake wengine.

Tafiti zinaonesha kuwa njia pekee ya kuimarisha ustawi kwa jamii ya watu wenye ulemavu ni Elimu na Michezo, kwa upande wa elimu usawa wa kijisnia unazingatiwa vyema lakini upande wa michezo wanaume wenye hali hiyo wanaonekana zaidi viwanjani ikilinganishwa na wanawake.

Taasisi za serikali na wadau wa michezo wanahamasisha michezo kwa wote ikiwa ni moja ya njia ya kujenga afya ,kupata ajira na kuimarisha Uchumi kwa jamii hasa ya watu wenye ulemavu.

Baadhi ya jamii na familia za watu hao wanachukulia jambo hilo kuwa ni jambo lisilokubalika na kuwekezana jambo ambalo linarudisha nyuma na kupunguza idadi ya wanamichezo wanawake wenye ulemavu.

Makala hii inaangazia sababu mbalimbali zinazopelekea Wanawake wenye ulemavu kushindwa kushiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali Visiwani Zanzibar.

BAADHI YA WANAWAKE WENYE ULEMAVU WALIOJITOA KUSHIRIKI KATIKA MICHEZO.

Bi Zawadi Khamisi, Mkaazi wa Darajabovu, mwenye mwenye umri wa miaka 28 ni mke na mama wa watoto watatu, amejiunga na chama cha mpira wa miguu (Amputee Football) bila kujali hali yake ya ulemavu na chanagamoto anazokabiliana nazo

Kwa sasa mama huyo hachezi mchezo huo ipasavyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchache wa wanamichezo wanawake wenye ulemavu,lakini anaenda viwanjani na kufanya mazoezi kila chama hicho kinapohiaji.

Bi Zawadi alisema wanawake wengi wenye hali hiyo hawana mwamko wa kushiriki katika michezo ikiwemo amputee football kutokana na kutokuwepo na miundombinu rafiki ya Viwanja vya kufanyia mazoezi, pamoja na kukosa fedha kwa ajili ya nauli na kutafutia vifaa vya michezo.

“Tunaishi mbali na viwanja vya kufanyia mazoezi na wiki nzima tunatakiwa kuhudhuria mazoezi, baadhi yetu hatuna hata kazi za kutuingizia kipato nauli hiyo tutaitowa wapi na hali hizi tulizonazo? , kama hutukuwezeshwa wanawake wenye ulemavu kwa kweli hatuwezi kushiriki katika michezo.”alieleza Bi Zawadi.

Ameeleza kuwa kutokana na hali walizonazo wanahitaji usafiri angalau wa Bajaji ili kuweza kufika viwanjani kwa wakati na bila kuchoka kwani masafa yaliopo baina ya vituo vya Daladala hadi kufika eneo hilo ni mbali kulingana na hali zao.

“Mimi nina mguu mmoja, nashushwa tobo la pili, hata nikifika Maisara au Mnazimmoja nimechoka na mara nyengine kuchelewa na kushindwa kufanya mazoezi, mfano hai umeuona hapa,sisi tunatakiwa tufike saa 8 za mchana unaona hadi sasa hivi saa 10 hii watu hawajafika,tukiwa na usafiri wa uhakiki itasaidia kuongeza ushiriki wetu.”aliesema mama huyo.

Hivyo aliishauri Serikali kutambua uwepo wao na kubuni mbinu rafiki zitakazowasaidia watu hao wakati wanapotumia usafiri wa umma .

“hata kutotozwa nauli wakati tunapopanda daladala na kutushusha sehemu rafiki, itakuwa msaada mkubwa kwetu na kutasaidia kuongeza idadi ya ushiriki wetu, kwani baadhi ya gharama itakuwa zimetupungukia” aliomba Bi Zawadi.

Pia aliwashauri wanawake wengine wenye ulemavu kujitokeza kuungana nao ili kuweza kupata timu ya wanawake wenye ulemavu wa mpira wa miguu na waweze kupata fursa kupitia mchezo huo.

Bi Amina Daudi Simba ni mwanamichezo kwenye chama cha michezo ya watu wenye ulemavu wa viungo anaeshiriki michezo tofauti kama kuogelea, basketball wall chair, kurusha mishale pamoja na mbio za Baskeli ya maringi matatu ndani na nje ya Tanzania amesema mitazamo hasi kwa baadhi ya familia za watu hao ni kikwazo cha kushiriki katika michezo.

“Baadhi ya familia za watu wenye ulemavu haziwaungi mkono watu hao kushiriki katika michezo wakiamini kufanya hivyo ni sehemu ya kumdhalilisha msichana na mwanamke mwenye ulemavu” alisema mwanamichezo huyo.

Bi Amina, anaeishi na dada yake maeneo ya Fuoni nyumba moja amesema familia yake sio kikwazo cha yeye kushiriki michezo kama ilivyo kwa familia za wanawake wengine wenye ulemavu.

Bi Amina aliwashauri wazazi na walezi kutokuwaficha wanawake na wasichana wenye ulemavu na badala yake kuwatoa katika maeneo mbalimbaliya jamii ikiwemo viwanjani ili kujenga hamasa ya wao kushiriki katika michezo kama wanavyoshiriki wengine ili kuongeza idadi ya wanamichezo wanawake wakiwemo wenye ulemavu.

“Jambo lolote ni lazima ulipende na liwe ndani ya damu yako, ikiwa michezo haipo katika damu yako kamwe hutoweza kushiriki kwani changamoto ni nyingi sana hasa kwetu sisi wenye ulemavu.” Alimalizia Bi Amina

KAULI YA VYAMA VYA MICHEZO JUU YA USHIRIKI WA WANAWAKE WENYE ULEMAVU KATIKA MICHEZO.

Mjumbe wa kamati ya michezo kwa watu wenye ulemavu wa viungo Ali Abdalla Khatibu amesema kadiri siku zinavyokwenda mbele ushiriki wa wanawake wenye ulemavu katika michezo unapungua kutokana na jamii kutokuwaamini na kuwakatisha tamaa.

Bwana Ali aliwaomba wadau wamichezo kuendelea kutoa elimu ili kuondoa mitazamo hasi ya jamii juu ya ushiriki wa wanawake wenye ulemavu katika michezo ili kuongeza idadi ya ushiriki wao na kuweza kujipatia maendeleo kupitia sekta ya michezo.

Hata hivyo aliwaomba wadau wa michezo kuwashirikisha watu wenye uleamvu katika mabonaza mnbalimbali yanapofanyika ili kuongeza hamasa za wengine kujitoa na kushiriki katika michezo kwa maendeleo.

Bi Saada Hamadi Ali ni mwenyekiti wa chama cha michezo cha watu wenye ulamavu wa akili Zanzibar na mzazi wa watoto wenye ulemavu amesema ushiriki wa wanawawake wa kundi hilo bado upo chini kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha katika vyama vya michezo vya watu hao kuweza kuwasaidia kujitokeza viwanjani kwa wingi.

“vyama vyetu vinaendelea kuhimiza familia za watu hao kuwaleta katika michezo lakini bado baadhi ya familia hazipo tayari kujitolea,wanachotaka ni kuona chama kiwawezesha kwa kila kitu jambo ambalo ni gumu kutokana na uwezo mdogo wa kifedha tulionao.”

Ameeleza kuwa familia nyingi zinapopata mtu mwenye ulemavu huchukulia kama sehemu ya mkosi na kuamua kuwaacha nyuma katika mambo mbali mbali ikiwemo masuala yakushiriki katika michezo, hali hiyo inachangia wanawake na wasichana wenye ulemavu kushindwa kushiriki michezo hiyo.

Ameongeza kuwa ushiriki wa wanawake wenye ulemavu katika michezo ni mdogo ukilinganisha na wanawake wasio na ulemavu kutokana na mitazamo ya baadhi ya jamii kuwa kumshirikisha mwanamke mwenye ulemavu na hata asie na ulemavu ni sehemu ya uhuni.

Bisada ambae pia ni Mjumbe wa Kamati ya Jumuiya ya wanawake wenye ulemavu JUWAUZA alitoa rai kwa serikali, wahisani wafadhili na wadau wa michezo kuviwezesha vyama vya michezo vya watu wenye ulemavu ili kuongeza idadi ya ushiriki wao viwanjani.

WADAU WANAVYOWAUNGA MKONO WANAWAKE WENYE ULEMAVU KUSHIRIKI KATIKA MICHEZO

Tamko la sera ya michezo ni kuwa Serikali itahaskikisha watu wenye mahitaji maalum wanapatiwa fursa sawa za kushiriki katika michezo pamoja na kuweka mikakati ya kushajihisha watu kutowaficha watu hao na badala yake kuwashajihisha kushiriki katika michezo.

Mikakati ya sera hiyo ni pamoja na kuandaa utaratibu wa kuwapatia mafunzo watu hao,kuandaa program za uinuaji wa vipaji vyao kuanzia Shehia,Wilaya ,Mkoa hadi Taifa ili kujiendeleza kimichezo,kuandaa utaratibu wa kuwapatia tunzo wanaofanya vizuri pamoja na kuzisaidia timu za watu wenye ulemavu kushiriki katika mashindano ya ndani na nje ya nchi.

Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu Zanzibar ZFF Sleiman Mohammed Jabir amesema shirikisho hilo linatambua haki za watu wenye ulemavu kikatiba pamoja na kusaidia mahitaji yao pale yanapohitajika ili kurahisisha shughuli zao za kimichezo zinazopelekea kuwajenga kimwili na kiakili sambamba na kujipatia fursa mbalimbali za kimichezo.

“Hivi karibuni kulikua na timu ya wasichana iliyoanzishwa na taasisi ya WEZA lakini kama sisi ZFF ambao ni walezi wa wachezaji wa mpira wa miguu tuliishauri timu hiyo kuhakiksha wanawashirikisha wanawake wenye ulemavu kwenda kuiwakilisha Zanzibar nje ya nchi ambapo mchezaji mmoja mwenye ulemavu wa ngozi alikwenda nchini ufaransa kushiriki mashindano kupitia weza na zff,hizo ni miongoni mwa jitahada zetu” alisimulia Rais wa ZFF

Bwana Sleiman amesema licha ya juhudi hizo lakini bado ushriki wa wanawake wenye ulemavu ni mdogo kutokana na baadhi yao kutokujikubali na kujiskia aibu kutokana na hali zao.

Hali hiyo hururudisha nyuma jitihada za baadhi ya wanawake wenye ulemavu walioamua kushiriki katika mchezo na hata kuwakatisha tamaa na kushindwa kufikia malengo.

“hadi sasa hakuna timu ya mpira wa miguu ya wanawake wenye ulemavu wa viungo kutokana na uchache wa watu hao viwanjani, sheria za mpira huu ni lazima timu iwe na wachezaji 12 na waliojitokeza ni kidogo .”alibainisha rais huyo.

Rais wa ZFF ameitaka jamii kubadilika na kuwatoa wanawake wenye ulemavu kuweza kuonesha uwezo wao katika michezo na kuweza kunufaika .

Katiba ya shirikisho la mpira wa miguu ZFF ya mwaka 2018 toleo la 2021 inaonesha kuwa miongoni mwa wanachama wa shirikisho hilo ni watu wenye ulemavu wa viungo bila kujali jinsia. 

Related Posts