Vyama vyaitupia lawama Takukuru rushwa za uchaguzi

Dar es Salaam. Baadhi ya vyama vya siasa vimeeleza mikakati yao ya ndani ya kukabiliana na rushwa, vikielekeza lawama kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwamba haina utashi wa kuikabili.

Vyama hivyo vimetolewa kauli hiyo, wakati Takukuru ikisema kuna viashiria vya rushwa vimeanza kujionyesha wakati Taifa likielekea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu 2025.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni ameitaka jamii kuripoti vitendo vya rushwa katika uchaguzi.

Hamduni alisema mbali na kuelimisha wananchi, wanachukua hatua za kudhibiti rushwa kwa kuendesha mashtaka kwa watakaobainika.

Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu leo Alhamisi Julai 4, 2024 amesema Takukuru bado haijaonyesha dhamira ya kukabiliana na rushwa kwenye uchaguzi.

“Bado hatujaona nia na utashi wa Takukuru wa kupambana na rushwa tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa.

“Tumeshapeleka malalamiko Takukuru, lakini hayafanyiwi kazi na mara nyingi tumekuwa tukiilalamikia CCM kwa vitendo vinavyoashiria rushwa,” amesema Ado.

Amesema katika uchaguzi ujao wamejipanga kurekodi na kuhifadhi matukio ya vitendo vya rushwa.

“Tutavitangaza vitendo vya rushwa kwenye vyombo vya habari kwa sababu navyo ni mhimili wa nne wa dola,” amesema.

Madai dhidi ya CCM yamekanushwa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), John Mongella aliyesema suala hilo wamekuwa wakilipinga tangu enzi za TANU.

“Sisi kwenye imani yetu tangu wakati wa TANU hadi sasa CCM inasema, rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea. Kwa hiyo, mwanachama akijiunga leo atakula kiapo na kutaja ahadi za mwanachama, ikiwemo hiyo. Hata viongozi wa kila awamu wamekuwa wakipambana na tatizo hilo,” amesema.

Hata hivyo, Mongella amesema rushwa ni tatizo la kibinadamu, hivyo inawezekana wakawepo baadhi ya wanachama wanaolalamikiwa.

“CCM ina wanadamu siyo kuku, hivyo kinakemea rushwa ndani na nje. Rushwa si tu tatizo la kitaifa, ni tatizo la kidunia,” amesema.

Mongella amesema, “CCM ni chama kikubwa kina wanachama zaidi ya milioni 12, hata nyumbani kwako kuna watoto wawili, lakini wanalalamikiana, sembuse wanachama wote hao?” amehoji na kusema wanachukuliana hatua hasa nyakati za uchaguzi.

“Watu wanaoomba uongozi wakibainika kujihusisha na rushwa wanakatwa. Hata kutuhumiwa tu unaondolewa,” amesema.

Mkurugenzi wa Uhusiano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema bado Takukuru haijaonyesha dhamira ya kupambana na rushwa kwenye uchaguzi.

“Takukuru wakiamua wanaweza kupambana na rushwa kwenye uchaguzi kwa sababu wanajua na wanazo taarifa, lakini hawachukui hatua,” amesema.

Mrema amesema miongoni mwa viashiria vya wazi vya rushwa ni makada wa upinzani wanaohamia CCM na kupewa madaraka haraka-haraka.

“Mtu anatoka Chadema anahamia CCM anapewa madaraka au anapitishwa kugombea, hiyo ni rushwa na Takukuru wanaona,” amesema.

Kuhusu mikakati ya kupambana na rushwa ndani ya Chadema, amesema kuna mwongozo waliouzindua mwaka 2012, wanaotumia kupambana na vitendo hivyo.

“Tumekuwa tukiengua wagombea kwa tuhuma za rushwa. Tulivunja Uchaguzi wa Baraza la Vijana (Bavicha) wa mwaka 2014 baada ya kupata taarifa ya mtu aliyekuwa akitoa rushwa na wapo pia viongozi waliosimamishwa uongozi kwa tuhuma hizo,” amesema.

Akizungumzia hoja zinazoelekezwa kwa Takukuru, mkurugenzi kuu wa taasisi hiyo, Hamduni amesema imejielekeza kuzuia vitendo vya rushwa kabla havijatokea.

“Mahakamani mnakwenda kama kumefanyika uchunguzi. Sisi mkakati wetu ni kuzuia kabla kosa halijatokea, maana Watanzania wamezoa ile reactive approach yaani unasubiri mpaka kosa litokee ndipo udhibiti,” amesema.

Kuhusu wanaohama upinzani na kupewa vyeo baada ya kujiunga na CCM, amesema suala hilo ni la kuchunguza kama kuna rushwa ndani yake.

“Hilo siwezi kulizungumzia kwa sababu sina taarifa za kutosha, nalichukua kama taarifa ya kuchunguza. Kwa sababu hao nao wana uhuru wa kuhama vyama wanavyotaka wanapohamasika na sera za vyama vingine,” amesema.

Related Posts