Ni Julai ambapo baadhi ya timu zimeanza rasmi kambi za maandalizi kwa ajili ya msimu mpya wa 2024/2025.
Kwa wale wachezaji ambao timu zao bado hazijaanza kambi za maandalizi ya msimu, kwa sasa wapo wanamalizia likizo zao ingawa hapana shaka nao muda sio mrefu wataenda kujiandaa kama ambao wenzao wameanza sasa.
Kuanza kwa maandalizi ya timu ni ishara ambayo haiachi shaka kwamba msimu unakaribia kuanza na timu muda mfupi ujao zitakuwa katika ushindani wa kusaka mataji ya mashindano mbalimbali.
Hapa nyumbani Tanzania maandalizi ya timu nyingi yatalenga zaidi kuziimarisha ziwe katika ubora wa kushindania mataji mawili makubwa kwa mfumo wa soka la nchi yetu ambayo ni Ligi Kuu pamoja na Kombe la Shirikisho la FA.
Kuna timu nne ambazo zenyewe pia zina taji la ziada la kuwania nazo ni Yanga, Simba, Azam FC na Coastal Union ambazo mwezi ujao wa Agosti zitacheza kugombea Ngao ya Jamii ambayo kwa sasa inachezwa kwa mfumo wa shindano la timu nne.
Katika namna ya kipekee timu hizo ambazo zitacheza kushindania Ngao ya Jamii, pia zitakuwa na kibarua cha kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya klabu Afrika msimu ujao.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Yanga pamoja na Azam FC watakuwa na jukumu la kuiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Simba na Coastal Union watakuwa na kibarua kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Ikumbukwe pia baadhi ya timu msimu ujao zitashiriki katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi na Kombe la Muungano ambayo hushirikisha timu za Tanzania Bara na Zanzibar.
Ni jambo la furaha kwa msimu kurejea na hasa kwa mashabiki ambao wamemaliza wiki kadhaa bila kuona mechi za mashindano baada ya msimu uliopita kumalizika.
Yapo mambo ambayo natamani kuyaona katika msimu unaofuata hasa kutoka kwa wachezaji iwe wa timu yangu ya Yanga au nyingine ambazo zinashiriki katika Ligi Kuu ya NBC.
Miongoni mwa hayo ambayo msimu ujao yatakuwa yenye tija ikiwa yataonekana ni wachezaji vijana kuonyesha viwango bora na vya kuvutia kuliko ilivyokuwa katika msimu uliomalizika.
Ukifanya marejeo ya msimu uliomalizika kwa haraka haraka utabaini kwamba hakukuwa na namba kubwa ya wachezaji wenye umri mdogo.
Timu nyingi zilitegemea zaidi mchango wa wachezaji wenye umri mkubwa wale walio na miaka 25 au zaidi lakini kwa wale wenye umri chini ya miaka 23 wengi hawakuwa na viwango vya kuvutia.
Matokeo yake wachezaji wengi wadogo hawakupata nafasi ya kutosha ya kucheza katika vikosi vya kwanza vya timu zao na kujikuta wakisotea benchi katika michezo mingi na baadhi wakitazama mechi wakiwa jukwaani.
Sio jambo zuri kuona wachezaji wenye umri mdogo wakikosa nafasi za kucheza katika klabu zao kwa vile umri walionao ndio ambao wanapaswa kutumika sana kwa vile miili yao ina nishati na nguvu za kutosha kuwawezesha kukimbia kilomita nyingi ndani ya uwanja na kutimiza majukumu mengi ya kiufundi.
Iko mifano ya wachezaji wengi duniani ambao wana umri mdogo lakini wamekuwa tegemeo katika vikosi vya timu zao kuliko hata wale ambao wana umri mkubwa.
Katika kikosi cha Manchester City ambayo imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England (EPL) msimu uliomalizika, mchezaji tegemeo zaidi alikuwa ni mshambuliaji wake Erling Haaland kutoka Norway ambaye kwa sasa umri wake ni miaka 23.
Ukiondoa Haaland, mchezaji mwingine ambaye alikuwa ni mhimili wa miamba hiyo ni Phil Foden mwenye miaka 24.
Arsenal ambayo ilimaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ilitegemea zaidi mchango wa winga wake Bukayo Saka ambaye ana miaka 22.
Kama wenzetu wanaweza ina maana na hapa kwetu kama wachezaji watajituma na kuonyesha ufanisi mzuri na mkubwa katika viwanja vya mazoezi watapata nafasi.
Kumekuwa na athari kadhaa kwa wachezaji wengi wenye umri mdogo kutopata nafasi katika vikosi vya timu mbalimbali zinazoshiriki Ligi Kuu katika msimu uliomalizika.
Mojawapo ni timu yetu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 23 kushindwa kufuzu Michezo ya Olimpiki ambayo itafanyika kati ya Julai 26 hadi Agosti 11 mwaka huu huko Ufaransa.
Tanzania ilitolewa katika raundi ya pili tu ya mashindano ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 23 ambayo timu nne zilizotinga nusu fainali zilijihakikishia tiketi ya kushiriki michezo ya Olimpiki mwaka huu.
Yaliyopita si ndwele tugange yajayo hivyo ni mategemeo yetu kuona vijana wengi wanajenga imani kwa makocha kwenye klabu zao hadi wakawashawishi wawape nafasi ya kutosha ya kucheza katika msimu ujao.
Wafahamu kwamba vipaji wanavyo na kinachowafanya wasipate nafasi ya kutosha ya kucheza ni kutoweza kutekeleza maelekezo kadhaa ya kimbinu kutoka kwa mabechi yao ya ufundi. Bila shaka msimu ujao watakuja kitofauti.
Mwandishi wa uchambuzi huu ni meneja wa timu ya Yanga.