Uingereza. Chama cha Labour kimeshinda Uchaguzi Mkuu wa Uingereza 2024 baada ya kufikisha viti 409 kikipita idadi ya viti 326 vinavyohitajika.
Ushindi wa Labour umeacha pigo kubwa kwa Chama cha Conservative kilichopata viti 113, likiwa ni anguko kubwa katika historia yao.
Waziri Mkuu wa Uingereza, aliyepo madarakani Rishi Sunak amesema anakubali kuwajibika kwa kushindwa katika uchaguzi mkuu wa chama cha Conservative.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazji la Uingereza, Chama cha Conservative kimeshika nafasi ya pili kikipata viti 113, kikifuatiwa na Liberal Democratic kilichopata viti 70.
Vingine ni Scottish National Party viti vinane, Sinn Fein (SF) viti saba, Independent (4), Reform UK (4), Green (4), Plaid Cymru (4), Democratic Unionist Party (4), Social Democratic & Labour Party (2), Alliance Party (1), Ulster Unionist Party (1), Traditional Unionist Voice (1).
Vyama vingine vilivyobaki havijapata hata kiti kimoja.
Akizungumza mjini London, waziri mkuu mtarajiwa Keir Starmer aliwaambia wafuasi wake, “mabadiliko yanaanza sasa.”
Sir Keir aliwaambia wafuasi wa chama cha Labour waliokuwa wakishangilia kuwa nchi hiyo inaamka kwa “mwanga wa jua wa matumaini unaangazia kwa mara nyingine tena nchi yenye fursa baada ya miaka 14 ya kurejesha mustakabali wake.”
“Nahisi vizuri, lazima niseme ukweli,” aliuambia umati wa watu waliokuwa wakishangilia.
Kwa upande wake Waziri Mkuu anayeondoka, Sunak aliyezungumza muda mfupi kabla ya Sir Keir, alikubali kushindwa, na kuwaambia Tories wenzake ilikuwa “uamuzi wa kutisha.”
Dalili zilishaanza kuonyesha tangu awali kwamba Labouro inashinda. Kabla hata matokeo hayajatangazwa, Sir Keir Starmer alielekea Downing Street (Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza) akiwa tayari ameshapata viti 160.
Katika hotuba yake ya ushindi wa eneo bunge, kiongozi huyo wa Labour alisema ni “wakati wa sisi kutoa.”
Rishi Sunak amesema anakubali kuwajibika kwa kushindwa kwa kihistoria katika uchaguzi mkuu wa chama cha Conservative.
Sunak aliwaambia wafuasi wake: “Watu wa Uingereza wametoa uamuzi mzito usiku wa leo, kuna mengi ya kujifunza… na ninawajibika kwa kushindwa huko.”