WIZARA YA ARDHI YAENDELEA KUTOA HUDUMA KWA WANANCHI SABASABA

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kutoa huduma kwa wananchi katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba kwenye Viwanja Vya Mwalimu barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho hayo, Afisa Mipango miji na Mratibu wa Urasimishaji wa Mkoa wa Dar es Salaam, Laurent Mswami amesema huduma wanazozitoa ni pamoja na kupanga, kupima na umilikishaji wa Ardhi ambapo hati utaweza kupata ndani ya siku moja.

Aidha Mswami amesema katika maonesho hayo Wizara ya ardhi inashirikiana na Mamlaka za upangaj za mkoa wa Dar es Salaam, tuna wataalamu kutoka manispaa ya Temeke, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Halmashauri ya manispaa ya Kinondoni, Halmashauri ya manispaa ya Kigamboni na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo hivyo wananchi watapata nafasi ya kusikilizwa na kupata huduma kwa uharaka zaidi.

“Kutokana na fursa hii ya sabasaba, wizara ya Ardhi imeamua kuweka kambi hapa ili kutoa huduma kwa wananchi wake kwa ukaribu zaidi hivyo tunawahasa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mikoa ya jirani, wafike kwenye maonesho ya sabasaba hususani kwenye Banda la wizara ya Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi waweze kupata huduma mbalimbali kuhusiana na ardhi, wakija hapa watasikilizwa changamoto zao zozote zinazohusiana na Ardhi pia Mipango miji, upimaji na umilikishaji”

“Tunatambua kuwa wananchi wanachangamoto mbalimbali za ardhi hasahasa migogoro hivyo mwananchi anapata fursa ya kusikilizwa changamoto yake yoyote kwa kupewa ushauri wa  utaalamu kwaajili ya utatuzi wa changamoto yake au pia kutatuliwa kabisa hiyo changamoto yake” amesema Mswami 

Kuhusu umilikishaji Ardhi, Mswami amesema mwananchi atakapofika katika Banda lao akiwa na nyaraka zote zinazohitajika, ataweza kupata hati ndani ya siku Moja.

Pia ameongeza kuwa Wizara hiyo imeboresha mfumo wake wa huduma wa utoaji hati, hivyo hati zinatolewa kidigitali.

“Kwa upande wa umilikishaji, wananchi tunawakaribisha kwasababu wengi huwa wanalalamika kwamba kuna changamoto za upatikanaji wa hati, lakini wakifika hapa sabasaba tunawaambia wanaweza kupata hati yao ndani ya siku Moja la msingi awe na nyaraka zote zinazohitajika na kujaza fomu zetu namba 19 ya maombi ya umilikishaji”

“Mwananchi anakuja hapa na nyaraka zake, zinachakataliwa, zinaingizwa kwenye mfumo, hata bili pia zinatolewa control namba, mwananchi anapokea bili yake ya gharama za hati kwenye simu yake akishalipia taratibu zingine za umilikishaji zinaendelea” ameeleza.

Related Posts