Aliyetakiwa Simba atambulishwa Mamelodi | Mwanaspoti

BAADA ya kukwama kujiunga na Klabu ya Simba, Kocha Steve Komphela ametua Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Komphela ataungana na Monqoba Mngqithi kukikonoa kikosi hicho kuchukua mikoba ya Rhulani Mokwena aliyefutwa kazi siku chache zilizopita. Ikutakumbukwa kwamba Komphela amerejea Mamelodi alikowahi kufanya kazi kuanzia 2020 hadi 2023 akisaidiana na Mokwena.

Kabla ya kutambulishwa Mamelodi, Komphela alikuwa chaguo la Simba iliyoamini atakuwa mbadala sahihi wa Abdelhak Benchikha aliyeachana na timu hiyo Aprili, mwaka huu.

Simba ilifanya mazungumzo na Komphela na kufikia hatua ya kumleta nchini kwa ajili ya kusaini mkataba wa kuwanoa Wekundu wa Msimbazi hao, lakini baadaye ikashindikana.

Mwanaspoti linajua sababu kuu ya Simba kushindwana na Komphela ni ishu ya maslahi, ikielezwa kocha huyo alitaka pesa ndefu ambazo Wanamsimbazi hawakuwa tayari kulipa.

Jambo lingine lililokwamisha kutua ‘Unyamani’ ni hisia hasi za viongozi wa Simba baada ya kudokezwa kuwa kocha huyo hana historia nzuri ya kukaa na timu pale anapokosa mahitaji yake kwa wakati.

Baada ya dili hilo kushindikana, Simba iliamua kumpa kazi kocha raia wa Afrika Kusini, Fadlu Davids aliyemaliza msimu uliopita akiwa kocha msaidizi wa Raja Casablanca ya Morocco.

Tayari Fadlu ametambulishwa Msimbazi akiambatana na wasaidizi wake Darien Wilken (kocha msaidizi), Riedoh Berdien (kocha wa viungo), Mueez Kajee (mtathimini mchezo) na sasa wanajiandaa kwa maandalizi ya msimu mpya.

Simba inaendelea kuboresha kikosi kwa ajili ya msimu ujao ikisajili wachezaji wapya na kuachana na baadhi ya nyota wake wa msimu uliopita.

Related Posts