Anayedaiwa kukodi watu kuua mke asomewa maelezo

Dar es Salaam. Serikali imemsomea maelezo ya awali ya kesi aliyekuwa Ofisa Usalama wa Taifa, Zaburi Kitalamo (50) anayedaiwa kuwatuma washtakiwa wenzake wawili kumuua mkewe kwa kumchinja.

Washtakiwa hao ni mfanyabiashara Roger Salumu (25) na mganga wa jadi Furaha Ngamba (47).

Kitalamo au kwa jina lingine Peter Alex Kitalamo, mkazi wa Uzunguni wilayani Urambo mkoani Tabora na wenzake Roger, maarufu Mayala, mkazi wa Utewe na Furaha mkazi wa Uyogo, wanadaiwa kumuua Atusege Kitalamo.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 234 ya mwaka 2022, washtakiwa wanadaiwa kumuua Atusege kwa kumchinja na kisha kuutupa mwili wake mtoni kwa madai ya imani za kishirikina.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 12, 2020 katika eneo la Kinzudi wilayani Ubungo, kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ua Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Washtakiwa wamesomewa maelezo ya kesi na Wakili wa Serikali, Neema Moshi, Julai 5, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Franco Kiswaga, aliyeongezewa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya mauaji.

Mahakama imeelezwa  Desemba 12, 2020 usiku, mshtakiwa Salumu na Ngamba walivamia nyumbani kwa Atusege, eneo la Goba walikovunja nyumba na kuingia ndani.

“Baada ya kuingia ndani, walimchukua Atusege na kumpeleka karibu na walikomchinja hadi kufa, baada ya kuagizwa na Zaburi kwa imani za kishirikina,” amedai wakili Moshi.

Amedai siku iliyofuata mwili wa Atusege ulipatikana ukiwa mtoni karibu na nyumbani kwake.

Upande wa mashtaka unadai tukio hilo liliripotiwa Kituo cha Polisi Goba na maofisa wa polisi walikwenda eneo la tukio ambako walichora ramani.

Mwili wa marehemu ulipelekwa Hospitali ya Mwananyamala, Desemba 15, 2020 ukafanyiwa uchunguzi na daktari.

“Ripoti ya uchunguzi ilionyesha chanzo cha kifo cha Atusege kilitokana na mshtuko uliosababishwa na kuvuja damu na majeraha makubwa,” amedai.

Washtakiwa walikamatwa na askari polisi wa Urambo na kuletwa Dar es Salaam, walikohojiwa. Walikana tuhuma hizo.

Katika mahojiano ya awali, Salumu na Ngamba walidai walitumwa na Kitalamo kumuua mkewe kwa imani za kishirikina.

Kitalamo na Salumu walikataa kuandika maelezo ya onyo polisi, hivyo walipelekwa kutoa maelezo ya ungamo kwa mlizi wa amani.

Baada ya kukamilika uchunguzi, washtakiwa walifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa moja la mauaji.

Moshi baada ya kusoma maelezo hayo amesema upande wa mashtaka unatarajia kuwa na mashahidi 24 na vielelezo 11 kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa.

Amevitaja baadhi ya vielelezo hivyo kuwa ni ripoti ya daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Atusege, mchoro wa ramani, maelezo ya onyo ya mshtakiwa Furaha, hati ya ukamataji na ripoti ya uchunguzi jinai.

Pia maelezo ya ungamo ya Kitalamo na Salumu kwa mlizi wa amani, hati ya ukamataji, simu mbili za mkononi, taarifa ya ziada ya Mahakama dhidi ya mshtakiwa Kitalamo na Salumu.

Washtakiwa baada ya kusomewa maelezo hayo walikana shtaka, wakikubali majina na taarifa binafsi.

Hakimu Kiswaga aliwauliza iwapo washtakiwa wanatarajia kuwa na mashahidi.

Kitalamo kupitia wakili wake, Selemani Matauka amesema watakuwa na mashahidi saba na vielelezo vitano, zikiwemo nyaraka.

Salumu kupitia wakili Ramadhani Makange amesema watakuwa na mashahidi watatu na vielelezo vitatu.

Mshtakiwa wa tatu anayetetewa na wakili Hilda Mushi, amesema watakuwa na mashahidi sita na vielelezo saba.

Mawakili hao waliomba mahakama iwape haki ya kutowataja majina mashahidi na vielelezo vyao hadi wakati wa usikilizwaji wa kesi.

Ombi hilo lilikubaliwa na mahakama. Hakimu Kiswaga alisema washtakiwa wataendelea kubaki rumande hadi Mahakama Kuu itakapopanga tarehe ya kuanza vikao kusikiliza kesi hiyo.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la mauaji linalowakabili kutokuwa na dhamana.

Related Posts