Dar es Salaam. Tanzania inakadiriwa kuwa na kuku milioni 97.9, kati ya hao wa asili (kienyeji) ni milioni 45.1 na wa kisasa ni milioni 52.8.
Kutokana na kuku kuwa miongoni mwa chanzo cha mapato kwa jamii, wafugaji wamekuwa wakiachana na ufugaji wa asili na kufanya wa kisasa.
Katika kutekeleza hilo, jitihada zimekuwa zikifanyika kupata vifaranga bora ambavyo havitakuwa na shida kuvikuza.
Ofisa mifugo na mratibu wa ndege wafugwao kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wambura Messo akizungumza na Mwananchi amesema kuku wa asili huzalisha mazao machache wastani wa mayai 60 kwa mwaka na ukuaji wake unatumia muda mrefu ikiwa ni miezi minne hadi mitano.
“Sera ya mwaka 2006 iliruhusu vibali vya kuingiza mbegu za kuku wa kigeni ambao wataziba nafasi ya uzalishaji wa hapa nchini ambao walionekana wana uwezo wa kukua kwa haraka kuanzia kilo 1.5 hadi kilo mbili,” amesema.
Amesema awali walianza kwa kuingizwa kuku aina ya Kuroiler ambao wanataga mayai 150 hadi 200, ambao walifanikisha kuziba nafasi ya upungufu wa kuku wa kienyeji, akifafanua kuwa kuku chotara waliozalishwa ni milioni 14.
Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yakiendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam, miongoni mwa vivutio kwa wafugaji ni kuku aina ya Brahma.
Kuku hao ni wakubwa, wenye manyoya mengi, hasa kwenye miguu.
Kutokana na mwonekano wa kuku hao, kiwango cha utagaji mayai na uzito mkubwa, kifaranga kinauzwa kuanzia Sh30,000 na mkubwa huuzwa hadi Sh300,000.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Julai 06,2024 katika maonyesho hayo, Athumani Abdalla, maarufu Babu Tale anayehudumia na kuuza kuku hao amesema akishirikiana na wenzake walianza kuwafuga kwa kuagiza mayai 3,000.
“Tulipoagiza mayai hayo kufika uwanja wa ndege tulipata hasara ya kupoteza mayai 50, yaliyobaki tuliweka kwenye mashine ya kutotoa vifaranga na baada ya hapo tulianza uzalishaji wa kawaida,” amesema.
Amesema walianza kuuza kuku hao baada ya kufikia 6,800 kwa kuwa walishakuwa na idadi kubwa.
Kwa mujibu wa Abdalla, faida ya kuku hao wanatotoa mayai mengi yanafikia hadi 30 na kulalia ndani ya siku 21, huanguliwa yote.
Amesema wamekuwa wakifanya biashara ya kuku hao ndani na nje ya nchi baadhi wakiwanunua kwa ajili ya mapambo.
Amesema wamekuwa wakiwauza Kenya, Msumbiji na Malawi. Pia wapo wanaonunua mayai, ambayo huuza moja kwa Sh10,000.
Elizabeth Massawe, aliyetembelea banda la Abdalla amesema jirani yake hufuga kuku hao, akieleza mmoja humuuza kwa Sh100,000.
“Jirani yangu anauza hawa kuku na wale wa mapambo kwa Sh500,000,” amesema Elizabeth.
Utaratibu wa kuingiza kuku
Ofisa mifugo Messo akizungumzia kuku aina ya Brahma amesema wizara inahitaji mayai na nyama, hivyo kumekuwa na kuku wa aina nyingi ambao utaratibu wa uingizaji wake unatakiwa kupeleka cheti cha kukaguliwa kwa shamba la kuku kutoka nchi husika.
“Haturuhusu kuingiza kuku nchini kwa sababu ya kuzuia mafua ya ndege lakini tunafanya hivyo kwa utaratibu maalumu kutokana na mahitaji na kwa sasa tunaingiza kuku wazazi na kama kuna mtu anataka kuleta wa maonyesho na mambo mengine atakuja na cheti cha ukaguzi wa shamba lake,” amesema.
Kwa asili kuku Brahma inaelezwa ni kutoka nchini India, eneo la mto Brahmaputra, ambalo ndiyo lilipotokea jina la kuku hao.
Aina hii ya kuku baada ya kuendelezwa na kuboreshwa nchini Marekani ilipata umaarufu na kusambaa maeneo mengine, kutokana na ukubwa wao na sifa zao nzuri za uzalishaji wa nyama na mayai.
Brahma ni miongoni mwa aina za kuku wakubwa wenye uzito unaotofautiana kati ya majogoo na mitetea.
Majogoo wanaweza kufikia uzito wa kati ya kilo 4.5 hadi 5.5 na mitetea huwa na uzito wa kati ya kilo 3.5 hadi 4.5.
Uzito unaweza kutofautiana kulingana na hali ya lishe na mazingira wanayofugwa.
Changamoto zilizopo ni upatikanaji wa mbegu bora, gharama za ufugaji na elimu kuhusu mbinu bora za ufugaji.