Dk Jafo mguu wa kwanza Kariakoo

Dar es Salaam. Siku moja baada ya kuapishwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Suleiman Jafo ameanza kushughulikia changamoto za wafanyabiashara, akianzia eneo la Kariakoo jijini hapa.

Hivi karibu wafanyabiashara katika baadhi ya maeneo nchini waligoma kushinikiza Serikali kutatua madai yao ambayo wanaeleza yalitatiza ustawi wa biashara zao.

Miongoni mwa hayo ni ukaguzi wa risiti za EFD na ritani za kodi, mambo ambayo Serikali imeyasitisha kwa muda.

Asubuhi ya leo Julai 6, 2024 Dk Jafo alifika Karikaoo alikofanya kikao na viongozi wa wafanyabiashara na kutembelea baadhi ya mitaa ya eneo hilo kuzungumza na wafanyabiashara na kusikiliza changamoto zao.

Hili limefanyika ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa jana Julai 5, alipomwapisha Dk Jafo na viongozi wengine aliowateua hivi karibuni, akimtaka kuwasikiliza wafanyabiashara ili aweze kutatua changamoto zao.

Mbali na kusikiliza kero hizo pia Rais Samia alimtaka Dk Jafo kuhakikisha Kariakoo inafanya kazi saa 24 kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali.

Alimtaka Jafo kuhakikisha wafanyabiashara wanakuwa marafiki zake, akisema hataki kusikia wadau hao wanamtafuta waziri hapatikani hasa kama mbunge huyo wa Kisarawe mwenye uwezo wa kuongea na kutembea.

“Ulikuwa ofisi ya Makamu wa Rais, umefanya kazi nzuri, lakini nimeona nikutoe nikupeke Biashara maana pilikapilika ni nyingi mno,” alisema Rais Samia.

Saa chache baada ya kupewa agizo hilo, Dk Jafo alifika Kariakoo ambako Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Taifa, Khamis Livembe amesema kwa kile alichokifanya  wanaona mwanga katika ufanyaji wa shughuli zao za kila siku ambao unaashiria yanayolalamikiwa yanafanyiwa kazi.

“Ameanza vizuri, kwa hili tunaamini changamoto ambazo tulikuwa tunalalamikia zitatatuliwa na kupatiwa suluhisho la kudumu na zile mpya zitakazojitokeza zitafanyiwa kazi kwa wakati,” amesema Livembe.

Katika hili, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kariakoo, Martin Mbwana amesema mbali na kufanya kikao pia wamekubaliana kuangalia namna ya kuwapanga wamachinga.

“Katika hili tutakuwa na Mkuu wa Mkoa pamoja na wakuu wa wilaya wote ili kuangalia namna ya kuwapanga machinga ndani ya Jiji la Dar es Salaam, tunaona mwanga mzuri mbele kwa sababu ameanza kuchukua hatua ndani ya muda mfupi tu tangu kuapishwa kwake,” amesema Mbwana.

Alipokuwa akiendelea kuhutubia, Rais Samia alisema pale ofisini ulipokuwa ukikaa sitaki ukae, lakini naelewa kwa nini Waziri (Dk Ashatu Kijaji) alikuwa hatoki kwa kazi ninayotaka kukupa ni kushinda Kariakoo panda shuka panda shuka, si rahisi kwa mtoto wa kike na siyo kazi rahisi,” alisema.

Katika uteuzi wa Rais, Dk Kijaji wamebadilishana wizara na Dk Jafo.

Rais Samia pia alimtaka Dk Jafo katika majukumu yake, arejee katika ilani ya uchaguzi ya CCM inayozungumzia sekta ya biashara na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ili kutoa mchango kwa Serikali.

“Lakini ukarejee kauli yangu kuhusu Serikali kuendelea kufanya kila linalowezekana kusikiliza na kutatua changamoto za wafanyabiashara,” aliagiza.

Muda mfupi baada ya kuapishwa Dk Jafo aliahidi ushirikiano kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa viwanda hasa katika kutatua changamoto mbalimbali za kibiashara ili kuhakikisha wanafanya biashara vizuri chini ya uongozi wake.

Katika hilo Dk Jafo aliahidi kuendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda na sekta binafsi kwa ujumla inayoajiri watu wengi zaidi nchini ili kuongeza ajira, pato la Taifa na kujenga uchumi imara na shindani wa viwanda.

“Nikiwa pamoja na wataalamu wangu nitaendelea kukutana na wafanyabiashara kupitia mabaraza ya biashara katika mikoa yote nchini kwa lengo la kusikiliza changamoto zao  na kujipanga jinsi ya kuzitatua ili kuhakikisha  sekta ya viwanda na biashara inakua na kuongeza ajira, pato la Taifa na kujenga uchumi imara na shindani,” amesema Dk Jafo.

Related Posts