Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewataka wananchi wasikubali kudanganywa kuvuruga amani, kwani ikitoweka hakuna atakayebaki salama na uchumi wa Taifa utadidimia.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Juni 6, 2024 katika hafla ya kilele cha maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislamu Zanzibar katika msikiti wa Jamiu Zinjibar.
Dk Mwinyi amesema amani na utulivu kimsingi ndiyo kiini cha kila mafanikio ya nchi yoyote duniani.
“Imani ikijengeka vizuri katika nyoyo zetu na tukaifuata kwa matendo yetu, basi amani na utulivu vitatawala katika maisha yetu yote. Hivyo, niwaombe wananchi wenzangu tuzingatie umuhimu wa kujifunza na kuifanyia kazi dini yetu kama inavyotakiwa ili imani itawale katika nyoyo zetu na hatimaye amani izidi kutawala katika nchi yetu,” amesema.
Amesema misingi ya kuimarisha uchumi wa nchi kuna vyanzo vya uchumi na katika dini ni vingi ikiwemo zaka, sadaka, wakfu na kodi zinazoendana na kipato cha mlipakodi.
“Nachukua fursa hii kuwaomba wafanyakazi wote, walioajiriwa na wanaojiajiri, wafanyabiashara wakubwa na wajasiriamali wadogo waongeze bidii na wajitahidi katika kufanya kazi kwa bidii,” amesema.
Rais Dk Mwinyi amesema: “Tuzingatie kufanya kazi kwa bidii ni ibada, hivyo ili tuweze kupata fadhila katika kutafuta mapenzi na radhi za Mwenyezi Mungu hatuna budi kufanya kazi kwa bidii kwa madhumuni ya kuinua uchumi wa nchi na ustawi wa watu.”
Amekumbushia malezi mema kwa watoto, akisema kuyumba maadili katika jamii unasababishwa na ukosefu wa malezi mema yanachangia kwa kiasi kikubwa vitendo viovu vya udhalilishaji.
Amewataka wazazi kuzingatia malezi mema kwa watoto wao kwa mujibu wa mafundisho ya dini ili kuondokana na mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Dk Mwinyi amesema ni wajibu wa kila mmoja kushiriki mapambano dhidi ya vitendo hivyo ambavyo vinaiaibisha jamii.
Awali, Sheikh Muhamed Mussa amesema wazazi wamejisahau kwa kiasi kikubwa, hivyo kuwaacha watoto bila kuwa na malezi yanayostahili.
Amesema ni wajibu wa wazazi wote wawili kushirikiana katika malezi kwani kila mmoja ana mchango wake, badala ya kutelekezewa mzazi mmoja asimamie malezi ya watoto