Dar es Salaam. Utafiti umeonyesha asilimia 81 ya Watanzania wanahitaji mabadiliko katika huduma za kijamii, hasa uboreshaji wa huduma za afya.
Katika maoni hayo yaliyokusanywa na Tume ya Mipango kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kutoka kwa Watanzania zaidi ya milioni moja, asilimia 81 ya waliohojiwa walipendekeza uboreshaji wa huduma za afya huku asilimia 19 wakitaka upatikanaji wa huduma hizo.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi, Julai 6, 2024 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo wakati akizindua kongamano la kitaifa la wadau wa sekta ya afya kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Tumeshakusanya maoni ya Watanzania kuhusu dira waitakayo kufikia mwaka 2050, walipoulizwa wataje changamoto kubwa tatu cha kwanza ilikuwa gharama za maisha na pili huduma za afya.
“Walipoulizwa tena mambo makubwa matatu wayatakayo walisema wanataka kuona uchumi mzuri, huduma bora za jamii, tulipowauliza ni zipi za kwanza ilikuwa afya na zikafuata zingine. Na hapa asilimia 81 walisema wanataka uboreshaji wa huduma na asilimia 19 upatikanaji wa huduma za afya,” amesema Profesa Kitila.
Amesema wanatarajia maoni ya wadau wa afya yajikite zaidi kwenye namna ya ukamilishwaji wa matamanio ya Watanzania.
Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru amesema maoni hayo watayakusanya mpaka Agosti mwaka huu, wataanza kuyapanga kwa ajili ya utekelezaji na mwisho kupitisha.
“Michango ya wananchi milioni moja katika simu na midahalo mbalimbali watu wamesema wanataka huduma za afya, hapa leo tunasikiliza watoa huduma za afya wanajipanga vipi miaka 20 ijayo ili tuwe na Tanzania bora katika sekta hii,” amesema Mafuru.
Amesema mwongozo wa usimamizi wa matayarisho ya dira, ulipitishwa na Baraza la Mawaziri, na kwamba mchakato huo ukikamilika utakua sheria.
Mafuru amesema miongoni mwa mambo ambayo Watanzania wengi wameuliza ni kuhusu utekelezwaji wa dira hiyo, hivyo matumaini ya Tume ni kutekelezwa kwa dira hiyo na wataipeleka bungeni ipitishwe kuwa sheria,
Amesema walichojifunza wakati wa upokeaji maoni hayo, Watanzania wengi hawafahamu kuhusu dira na kwamba walikubaliana kuna haja ya kila mtu kufahamu dira ya Taifa.
Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema changamoto kubwa katika sekta ya afya ni ugharamiaji wa huduma za afya, huku akitaja changamoto kubwa kuwepo katika magonjwa yasiyoambukiza.
“Ugharamiaji wa huduma za afya ndiyo kila kitu, angalieni uchaguzi wa Marekani, Uingereza kampeni kubwa ni kuhusu bima ya afya na hifadhi ya jamii, kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza katika gharama za matibabu. Tukiwa na bima kwa wote tutafanikiwa,”
Changamoto ambayo tulikuwa nayo baada ya muswada kuwa sheria ilikiwa watu watachangia vipi, wale wasio na uwezo. Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan ameelewa tumepata chanzo mahususi sasa hivi kitagharamia watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wajawazito na tutaanzia kwa watoto wenye umri sifuri mpaka miaka miwili,” amesema Waziri Ummy.