JKT Tanzania imeendelea kuimarisha kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano ambapo inaelezwa imemalizana na beki wa kati, Abdulrahim Seif Bausi aliyekuwa Uhamiaji ya Zanzibar aliyewahi kutakiwa na Simba kabla ya maafande hao kuwapiga bao Wekundu waliombeba Abdulrazak Hamza na kumtambulisha juzi.
Beki huyo, ambaye ni mtoto wa nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kutamba na kuifundisha timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, Seif Bausi amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo.
Bausi ni mmoja ya wachezaji 11 waliopo katika Kikosi Bora cha Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) iliyomalizika hivi karibuni na pia mmoja ya wachezaji watano waliokuwa wakichuana kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu (MVP) iliyoenda kwa straika Suleiman Mwalimu Abdallah wa KVZ.
JKT ni kama imeizidi ujanja Simba, kwani nayo ilikuwa ikimsaka mchezaji huyo, lakini tayari imeishapigwa bao ndio maana ikamkimbilia Hamza aliyekuwa akicheza soka la kulipwa katika klabu ya Cape Town City ya Afrika Kusini huku akiwahi kuzitumikia KMC, Mbeya City na Namungo.
“Kwanza umri wake ni mdogo, hivyo tunatarajia ataonyesha uwezo wake, kwa sababu atakuwa na uchu wa kuonyesha kiwango chake tumewasajili kama John Bocco, Charles Ilanfya na wengine ni Said Ndemla na David Bryson ambao walitoka Singida Big Stars, kuna kocha Ahmad Ally,” kilisema chanzo chetu.