Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inatarajia kupokea Euro 350 million (Sh1 trillion) kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU).
Lengo la fedha hizo ni kuziinua kampuni ndogondogo zinazotaka kuwekeza katika sekta ya uchumi wa buluu.
Baada ya fedha hizo kutolewa zitaleta ahueni kwa kampuni hizo zilizokuwa zikikumbana na changamoto za kupata mikopo benki, hivyo fedha hizo zitakwenda kuziba pengo.
Akizungumza wakati wa mkutano wa kutia saini makubaliano hayo Julai 6, 2024 mjini Unguja, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu, Zahor Kassim Kharousy amesema fedha hizo zitaziwezesha kukopa.
“Awali kampuni pamoja na wananchi waliokuwa wakiomba mikopo katika benki wengi wao walikosa kwa sababu ya kutofikia vigezo vilivyopo, hivyo faida ya fedha hizi zinaenda kuziba hilo na kuwafanya wakopesheke,” amesema Zahor.
Amesema benki hiyo itafanya mazungumzo na benki za Tanzania zikiwemo CRDB, NMB na KCB ili kuona namna bora ya kupunguza masharti.
Amesema Serikali itatumia fursa hiyo kuwashajihisha wananchi na kampuni kufanya biashara na kuzitumia fursa hizo katika benki kwani zipo kwa ajili yao.
Makamu wa Rais wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya, Thomas Ostros amesema fedha hizo zinakwenda kufungua milango kwa kampuni ndogondogo ili kuwekeza katika uchumi wa buluu.
Amesema fedha hizo zitagawanywa katika benki tatu za Tanzania za CRDB ambayo itapokea Sh430 bilioni, NMB itapokea Sh287 bilioni na KCB itapokea Sh58 bilioni na Sh229 bilioni zitapewa taasisi nyingine za fedha nchini.
“Msingi wa fedha hizo utaangalia wanawake zaidi ambao wanajihusisha na sekta ya uchumi wa buluu kwa ajili ya kujiendeleza,” amesema.
Thomas amesema biashara ndogondogo ni muhimili katika uchumi wa Afrika kwani wanatengeneza ajira kwa kuibua mambo mbalimbali lakini kwa upande wa benki ya uwekezaji inatumia fedha ili kuwainua wajasiriamali.
Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Emillio Rossetti amesema makubaliano hayo ni matokeo ya uwekezaji wa Benki ya Ulaya katika kuimarisha ushirikiano baina yao na Tanzania.
Amesema umoja huo upo katika kuwaimairisha zaidi wanawake ili kukuza vipato vyao.
Pia amesema Umoja wa Ulaya kati ya fedha hizo Sh1 trilioni, wao wamechangia Sh43 billioni na ina ushirikiano mzuri katika kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa.
“Ahueni itakayopatikana ni katika ulipaji na riba. Kama walikuwa wakikopa na kulipa miaka miwili kwa sasa wataongezewa muda wa kulipa miaka mingine zaidi. Hata hivyo, masharti hayo yatawekwa wazi baada ya kuanza rasmi ukopeshaji huo,” amesema.