Dar es Salaam. Wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe likiendelea na uchunguzi kubaini chanzo kifo cha aliyekuwa mfamasia katika Kituo cha Afya Isansa wilayani Mbozi, Daudi Kwibuja, taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zimeibua mapya zikiwataja baadhi ya vigogo kuhusika.
Mwili wa mfamasia huyo ulikutwa kando mwa barabara ya Tunduma – Mbeya, eneo la Mlowo ukiwa umejaa majeraha ikidaiwa alifariki dunia Julai 3, 2024.
Katika taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoani humo, SACP Agustino Senga, uchunguzi wa awali ulionyesha aliuawa usiku wa Julai 3 kabla ya kuokotwa asubuhi yake.
Alieleza awali ilidhaniwa alikufa kutokana na ajali ya gari, lakini baada ya mwili kuchunguzwa umekutwa na majeraha ambayo hayafanani na ajali ya kugongwa na kuahidi kuendelea na uchunguzi.
“Majibu ya uchunguzi yatakapobainisha ameuawa, Jeshi la Polisi litahakikisha linawasaka waliohusika na sheria kushika mkondo wake,” alisema Senga.
Kamanda Senga akizungumza na Mwananchi leo Julai 6, 2024 amesema bado hakuna anayeshikiliwa licha ya kuwaita na kuwahoji baadhi ya watu wanaosadikiwa kuhusika na tukio hilo (hakuwataja majina) kisha kuwaachia huru.
Amesema kwa sasa maneno ni mengi mitaani na mitandaoni kila mmoja akieleza la kwake, hivyo Jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi wa kina akiomba wananchi kutoa ushirikiano.
“Hakuna aliyeshikiliwa, japo kuna ambao tuliwaita na kuwahoji kisha kuwaachia, maneno ni mengi ikiwamo bodaboda na mkewe kuhusishwa na tukio hili ila hatuwezi kufanyia kazi mambo ya mitaani na mitandaoni,” amesema.
“Tunachofanya ni uchunguzi wa kina kujiridhisha na ukweli na kuchukua hatua. Jeshi la Polisi linaomba wananchi kutoa ushirikiano kwani marehemu eneo la mwisho kuonekana ni baa inayoitwa Kona ya Mkoa,” amesema.
Taarifa iliyosambaa mtandaoni ilidai mkoani Songwe na hasa wilayani Mbozi kuna mtandao wa wizi wa dawa za binadamu zinazopelekwa na Serikali kwenye zahanati na vituo vya afya.
Inadaiwa mwaka jana kuna mzigo uliokamatwa katika moja ya zahanati na kesi ilifikishwa kituo cha polisi na mfamasia huyo alitakiwa kuripoti kituoni.
Inadaiwa dawa hizo zilikabidhiwa kwa watu wengine hivyo kupoteza ushahidi, lakini mfamasia huyo aliendelea kushikiliwa.
Inadaiwa baadaye alisimamishwa kazi pamoja na mwenzake, lakini mfamasia huyo alifuatilia haki yake akarejeshwa kazini Juni 7,2024 akapelekwa Kituo cha Afya Isansa.
Licha ya kurejeshwa kazini, inadaiwa aliazimia kuendelea kudai haki yake na kufichua wizi ndipo Julai 3, akiwa baa inaelezwa alipewa lifti na mtu kutokea hapo baa, kisha mwili wake kupatikana kando mwa barabara.
Kamanda wa Polisi Senga alipoulizwa na Mwananchi kuhusu taarifa hiyo ya mtandaoni alisema hajaipata.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Dk Alex Magelu anayetajwa katika taarifa ya mtandao alipoulizwa kuhusu madai hayo alisema hajui na hana taarifa zozote kuhusu kifo cha mtumishi huyo akielekeza aulizwe mkurugenzi wa halmashauri hiyo.
“Hizo habari za mitandao mnazitoa wapi? Mimi sijui kitu chochote muulize mkurugenzi,” amesema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbozi, Abdallah Nandonde alipotafutwa kwa simu iliita lakini haikupokewa.