RAIS Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuhakikisha kuwa shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini zinatekelezwa kwa kasi ili kuongeza ugunduzi wa rasilimali hiyo muhimu.
Mhe. Kikwete ameyasema hayo tarehe 06 Julai 2024 wakati alipotembelea banda la PURA katika maonesho ya 48 ya Saba Saba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
“Nimefurahi kwa mipango mizuri iliyopo ya kunadi vitalu. Hata hivyo, kasi ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini bado ni ndogo. Jitihada za ziada zifanyike kuongeza kasi hiyo” alieleza Kikwete.
PURA kwa niaba ya Serikali imeendelea na maandalizi ya kunadi vitalu vilivyowazi vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.
Miongoni mwa manufaa yatakayotokana na kunadi vitalu hivyo ni pamoja na kuvutia uwekezaji katika mkondo wa juu wa petroli utakaopelekea ongezeko la shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.
Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza jambo mara baada ya kusikiliza maelezo ya wataalamu katika banda la PURA ndani ya maonesho ya Saba Saba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Bw. Ebeneza Mollel kutoka PURA (kushoto) akitoa maelezo kwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mara baada ya kutembelea banda la Mamlaka hiyo katika maonesho ya 48 ya Saba Saba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.