Kikwete akoshwa na Sabasaba akumbukia utawala wake

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DIFT) kwa mwaka huu, yamekuwa ya kipekee kwa kuboreshwa miundo mbinu hususani ya barabara tofauti na miaka ya nyuma.

Kikwete ameeleza hayo leo Julai 6, 2024 alipotembea DIFT maarufu kama sabasaba na katika mazungumzo yake alikuwa akilinganisha hali anayoiona na miaka ya nyuma hususani wakati wa utawala wake.

“Kipindi changu wakati nakuja barabara zilikuwa za vumbi na maombi yangu yalikuwa ni kuhakikisha barabara zinawekwa lami, maana ilikuwa unakuja huna mafua lakini unaondoka na mafua,” amesema.

Pia amesema alikuwa anaangalia uboreshaji wa mabanda na bidhaa zinazoonyeshwa kuanzia kwa wageni hadi wazawa na hata wawekezaji wamekuwa wakieleza vitu kwa ufasaha tofauti na mwaka jana.

Akizungumzia kuhusu nishati safi, Kikwete amesema wakati anapokea uongozi matumizi ya umeme yalikuwa asilimia 10 na matumizi makubwa yalikuwa mjini na si vijijini.

Amesema waliamua kuanzisha mradi wa umeme wa vijijini ambao ulianzia kwa hayati Benjamini Mkapa na yeye alilikamilisha na alipokwenda kwenye ziara mkoani Mara,  alizindua umeme wa Rea na wakati huo umeme ukiwa kwenye vijiji 206 pekee.

‘’Wakati huo watu walikuwa wanahitaji umeme vijijini na wangeachiwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambao wanafanya biashara wao wanaangalia sehemu ambayo walikuwa na uhakika wa biashara,’’ amesema.

Ametoa wito kwa watoa huduma wa umeme na gesi,  kuangalia bei wanazotoa zisiwaumize watumiaji kwani inaweza kuwa sababu ya kurudi kwenye matumizi ya mkaa na kuni.

“Sijui kama takwimu zimebadilika Dar es Salaam walikuwa wanatumia magunia ya mkaa 40,000 kwa siku ni kwa kiasi gani miti imepotea hapo,” amesema Kikwete.

Kikwete ametumia zaidi ya saa tano kuzunguka mabanda mbaalimbali. Aliingia viwanjani hapa saa 5:30 asubuhi na hadi saa 11 :00 jioni alikuwa bado akizunguka katika mabanda mbalimbali kuangalia bidhaa, kununua na kuacha maoni katika baadhi ya sehemu alizotembelea.

Kila alipopita watu waliacha shughuli zao wakitaka kumsalimia, kupunga mkono huku naye akisalimiana na baadhi ya watu hasa watoto.

Miongoni mwa sehemu ambazo alionekana kuvutiwa nazo sana ni mabanda ya viwanda vya magari, pikipiki, teknolojia mbalimbali ikiwemo za kilimo kwa waliouza matrekta.

Alipofika katika banda la GF Trucks and Equipment alifurahi kuiona kampuni ya Hyundai inarudi katika soko huku akieleza kuwa ipo nchini tangu kipindi cha utawala wake.

Related Posts