BAADA ya vuta nikuvute kuhusiana na mkataba wa winga wa Simba, Aubin Kramo kuwa mgumu kuvunjwa, kwa sasa mchezaji huyo msimu ujao atacheza kwa mkopo katika kikosi cha Al Hilal ya Sudan.
Kramo tangu ajiunge na Simba msimu uliopita akitokea ASEC Mimosas ya kwao Ivory Coast hakuwahi kuitumikia kwenye mechi za mashindano kutokana na kukabiliwa na majeraha ya muda mrefu, japo makocha waliofundisha kikosi hicho kwa nyakati tofauti walikiri anajua mpira.
Hata hivyo, winga huyo ilielezwa ameshapona na angebakishwa kikosini kwa msimu ujao, kabla ya mambo kubadilika kwa kuelezwa Simba imeamua kumtoa kwa mkopo Sudan, baada ya kushindwana kuachana jumla kwa sababu ya mkataba alionao na klabu hiyo.
Mmoja wa vigogo wa Simba, aliliambia Mwanaspoti kuwa, pande zote mbili zimekubaliana na sasa Kramo atakuwa sehemu ya wakali wa Sudan ambao wataicheza Ligi Kuu ya Sudan huko Mauritania baada ya kushindwa kucheza nchini kwao kutokana na hali mbaya za kiusalama zinazochangiwa na machafuko.
“Mkataba wake ulikuwa na mambo mengi, ila kwa sasa atakwenda kucheza kwa mkopo, tunamtakia kila la kheri akawe na mwanzo mzuri,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Kramo licha ya kumuondoa katika mifumo bado alikuwa ni mchezaji wa Simba na alikuwa analipwa kama kawaida lakini sasa ni rasmi kuwa tumemalizana naye kwa makubaliano ya pande zote mbili.”
Mbali na Kramo anayeondoka Msimbazi kuwapisha majembe mapya yanayoendelea kushushwa na Simba ni pamoja na Sadio Kannoute, Pa Omar Jobe, Willy Onana na Babacar Sarr ambao wanaungana na Clatous Chama aliyetua Yanga, Henock Inonga aliyejiunga na FAR Rabat ya Morocco na Luis Miquissone aliyerejea UD Songo.